Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiongoza Mamia ya Wananchi pamoja na Viongozi wa Serikali, Siasa na Dini wa Mji wa Dodoma na Vitongoji vyake katika Kuuaga Mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Tuppa. Nyuma yake Balozi Seif Alifuatiwa na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda na Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Anna Makinda.
Mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gariel Tuppa aliyefariki Dunia Juzi Tarehe 26/3/2014 ukiingizwa ndani ya Bunstani ya Nyerere Square kati kati ya Vitongoji wa Mji wa Dodoma kwa ajili ya Ibada Maalum ya Kuuaga.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar wa Pili kutoka Kulia akiwaongoza Mamia ya wakaazi wa Mji wa Dodoma katika kutoa heshima zao za mwisho kwa Mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gariel Tuppa ndani ya Viunga vya Nyerere Square Mjini Dodoma.Kulia ya Balozi Seif ni Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda,Mke wa Waziri Mkuu Mama Tunu Pinda na Spika wa Bunge la Muungano Mh. Anna Makinda na kushoto yake Balozi Seif ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehemu Nchimbi.
Mke wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gariel Tuppa Mama Tupa Gabriel wa Pili kutoka Kulia pamoja na wana Familia ya marehemu wakiwa kwenye Misa ya kuuaga Mwili wa Marehemu Mumewe ndani ya Bustani ya Nyerere Squre Mjini Dodoma.
Wana Kwaya ya Mtakatifu Sifiria Chini ya Muongozaji wao Fransis Patrik wakiendelea na nyimbo za Ibada katika Misa ya kuuaga Mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gariel Tuppa.(Picha na Hassan Issa OMPR)
Na Othman Khamis. OMPR
Mamia ya wananchi na Wakaazi wa Mji wa Dodoma na vitongoji vyake leo wameuaga rasmi mwili wa Mkuu wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gabriel Tuppa aliyefariki Dunia katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Marehemu John Gariel Tuppa alilazimika kupatiwa huduma za matibabu baada ya kuugua ghafla ugonjwa wa Shindikizo la Damu { Blood Pressure } akiwa katika Vikao vya kazi Wilayani Tarime.
Misa ya kumuombea Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara iliyoongozwa na Makamu Askofu wa Kanisa Katoliki la Mkoa wa Dodoma Father Chesco Msaga ilifanyika katika Uwanja wa Nyerere Suare kati kati ya Vitongoji vya Makao Makuu ya Serikali Mjini Dodoma.
Wakiwa katika hali ya majozi mamia ya wananchi hao wakiongozwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Waziri Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Pinda, Mawaziri wa Serikali zote mbili, Viongozi wa Dini tofauti wakiwemo pia wawakilishi wa mashirika na Taasisi za Kimataifa walipata fursa ya kuuaga mwili wa Maheremu John Gabriel Tuppa.
Wakiwasilisha salamu mbali mbali wawakilishi wa Serikali, Viongozi wa Dini na Taasisi tofauti za Kijamii walimueleza Marehemu John Gabriel Tuppa kwamba ni Kiongozi wa mfano atakayekumbukwa miaka kadhaa ijayo kutokana na mchango wake hasa katika masuala ya Kijamii.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa { TAMISEMI } Mh. William Lukuvi alisema miaka 20 ya Utumishi wa Marehemu John Gariel Tuppa ndani ya Manispaa ya Makao Makuu Mjini Dodoma { CDA } utaendelea kukumbukwa na wananchi walio wengi Mkoani humo.
Mh. Lukuvi alisema usimamizi wa Marehemu Tuppa wakati wa ustawishaji wa Makao Makuu ya Mji wa Dodoma umeuwezesha Mkoa huo kuwa na zaidi ya skuli za Msingi zipatazo 30 katika kipindi cha utumishi wake.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma Profesa Ame alimueleza Marehemu John Gabriel Tuppa kuwa ni Kiongozi anayependa kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi hasa wale wa mazingira duni na kuyatafutia ufumbuzi muwafaka.
Profesa Ame alisema mchango wa Marehemu Tuppa Daima utaendelea kukumbukwa na wana chuo hicho kikuu cha Dodoma kwa vile ushujaa wake kwa kiasi kikubwa umechangia kukihuisha Chuo hicho ambacho sasa kimekuwa tegemeo kubwa kwa Watanzania walio wengi.
“ Wakati tuko katika heka heka za kutaka kukisimamisha Chuo chetu Kikuu cha Dodoma kianze kazi zake hitilafu na changamoto zilizojitokeza katika uanzishaji wake ziliweza kupatiwa ufumbuzi chini ya umahiri wa Marehemu John Gabriel Tuppa wakati akiwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma “. Alisema Profesa Ame.
Naye Sheikh Kazungu kwa niaba ya Sheikh wa Mkoa wa Dodoma alisema mchango wa Mrehemu John Gabriel Tuppa hauna budi kuenziwa na wananchi wote waliowahi kufanya kazi naye kama ishara ya kuthamini mchango wake.
Sheikh Kazungu alifahamisha kwamba Marehemu Tuppa bila ya kujali itikadi za Kisiasa au madhehebu ya Dini tofauti alikuwa kiongozi wa mfano katika kuona matatizo ya Jamii yanatatuka.
“ Sisi waumini wa Dini ya Kiislamu tumeshuhudia mchango mkubwa wa Kiongozi huyu ambao umetupa faraja katika harakati zetu za Kidini za Kila siku. Marehemu Tuppa alikuwa haoni shida kutufuata kwa kutuelekeza, kutuonya au kutupa nasaha kwa mambo ambayo aliyaona yanaashiria matatizo katika imani zetu za Kidini “. Alifafanua Sheikh Kazungu.
Mwili wa Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara Marehemu John Gariel Tuppa umepelekwa nyumbani kwao Kilosa Mkoa wa Morogoro ambapo asubuhi ya Jumamosi itafanyika ibada ya kumuaga mara ya mwisho kabla ya kuzikwa rasmi.
Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda akiambatana na Viongozi mbali mbali wa Serikali, Kisiasa na madhehebu wa Dini Tofauti anatarajiwa kujumuika pamoja na Wananchi hao wa Kilosa katika mazishi hayo akiliwakilisha Taifa kwenye msiba huo mzito.
Marehemu John Gariel Tuppa ambaye aliwahi kufanyiwa vipimo vya tatizo lake lililosababisha kutokwa na mapofu na kuishiwa nguvu akiwa kikaoni Wilayani Tarime aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa katika Mikoa na Wilaya Tofauti hapa Nchini Tanzania.
Marehemu Tuppa aliyezaliwa mwaka 1950 ameacha Mjane mmoja na Watoto kadhaa. Mwenyezi mungu ailaze roho ya marehemu John Gabriel Tuppa mahali pema peponi. Amin.