Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

JK, umma ukiamua ndio umeamua

$
0
0
Na Salim Said Salim
 
KAULI ya hivi karibuni ya Rais Jakaya Kikwete juu ya mchakato wa kutafuta Katiba mpya ya Tanzania inaonekana kuwaumiza kichwa watu wengi wa Visiwani na kuwa mada ya mjadala kila pembe ya mji wa Unguja.
 
Baadhi ya watu wanamuona kuwa ni kiongozi asiyeeleweka, wengine wanamuhisi mwepesi wa kuyumba na anafuata upepo au upepo ndio unaoamua safari yake ielekee wapi kama zilivyo safari za majahazi ya Bagamoyo, Unguja, Lindi na Mtwara.
 
Kwa mtazamo wa baadhi ya watu, Rais Kikwete wanamuona asiyeweza kutofautisha kati ya kofia ya chama chake na ile ya urais. Wanamuona hajui ni hadhira gani ahutubie kwa kofia ya urais na ipi kwa kofia ya chama chake cha CCM.
 
Hotuba yake ya ufunguzi wa Bunge Maalumu la Katika mjini Dodoma, imewashangaza watu wengi kwa namna alivyojivika usemaji wa mwisho wa nchi ielekee wapi katika kupata katiba.
 
Wanadhani alipaswa kuheshimu ushauri wa wananchi waliotoa maoni yao yaliyoratibiwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba.
 
Lakini wapo wanaoona Rais Kikwete ametaka kuonyesha kuwa hatofautiani na marais waliopita, waliojenga utamaduni wa kuunda tume na baadaye kudharau ripoti zinazotolewa, kama vile kazi iliyofanywa haina maana kwa vile mapendekezo yake hayaifurahishi CCM.
 
Kauli ya Rais Kikwete alipozungumza na wazee katika Ikulu ndogo ya Wilaya ya Muheza, Tanga, kwamba anawaachia wajumbe wa Bunge la Katiba kuamua muundo wa Muungano unaofaa, kama ni serikali mbili au tatu ndiyo umewakoroga zaidi watu.
 
Kama Rais Kikwete anaamini hayo aliyoyasema Muheza, kwanini alitoa muongozo wa Bunge la Katiba liamue vipi badala ya kuwaachia wabunge kufanya hivyo na hatimaye umma kuamua?
 
Hivi sasa baadhi ya watu wanaliona Bunge la Katiba kama kiini macho cha kuwadanganya Watanzania kuwa nchi inayo demokrasia ya kweli na kumbe ni demokrasia ya chama kimoja, ambapo hata msingi muhimu wa demokrasi wa kura ya siri umepigwa mwereka na CCM kama vile ni mfumo wa kidikteta na kifashisti.
 
Rais Kikwete aliwaambia wazee wa Muheza kama wajumbe  watapendekeza mfumo wa serikali tatu ruksa kwani ndiyo mapendekezo yao, hivyo hayawezi kupingika kwa namna yoyote.
Watu wanajiuliza, hivyo rais anao uwezo gani kisheria unaompa mamlaka ya kusema serikali mbili au tatu ndiyo ruksa?
 
Hivyo kweli Rais Kikwete haelewi kuwa hii nchi ni ya Watanzania na ni wao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya mfumo wa serikali wanaoutaka na ni wajibu wa serikali inayoheshimu umma kuridhia?
 
Linalonishangaza zaidi ni kusikia Rais Kikwete akisema mfumo wa serikali tatu una changamoto zake, lakini ninachotaka nimueleze ni kuwa wakati mfumo wa serikali tatu unazo changamoto kwa watu wengi wa Zanzibar (na Bara kwa kiasi kikubwa) mfumo wa serikali mbili si una changamoto, bali ni moto, unaunguza na kubabua.
 
Wazanzibari wamelalamikia mfumo huu kwa muda mrefu na kumbukumbu zinaonyesha namna ambavyo chama tawala kilivyowafukuza uanachama na kuwavua uraia baadhi ya watu kwa vile wamehoji kama kuna haja ya kuendelea na mfumo wa serikali mbili.
 
Kwa taarifa yake Rais Kikwete, Wazazibari na mimi nikiwa mmoja wao, siamini kabisa kauli za viongozi wa Muungano kwa vile kinachosemwa sio kinachotendwa. Sisemi ni waongo, lakini kauli zao zina mushkeli.
 
Labda haya yafuatayo yatampa Rais Kikwete na Watanzania wengine mwanga wa kuelewa kwanini Wazanzibari wanasema wanataka kusema kwaheri serikali mbili:
 
Wazanzibari walitaka wauone mkataba halisi wa Muungano. Waziri Mkuu Fredrick Sumaye aliahidi Bunge (angalia kumbukumbu za Bunge) kwamba hiyo nakala ingeonyeshwa. Hadi leo haionekani na hapana dalili ya kupatikana. Hili linawapa watu shaka.
 
Zanzibar ilipojiunga na Jumuiya ya Kimataifa ya Nchi za Kiislamu (OIC) tuliambiwa Tanzania ingejiunga, hivyo Zanzibar ikalazimishwa kujitoa. Sasa ni miaka 20 na suala hili halizungumzwi.
 
Kila zikizungumzwa kero za Muungano tunasikia viongozi wapo mbioni kutatua. Miaka inapita na Wazanzibari hawaoni hizo mbio kufikia ukingoni. Au hao wakimbiaji wameanguka?
 
Kwa taarifa yake hata wawakilishi walionekana kukasirishwa sana na hii danganya toto na kufika hadi kutaka baadhi ya taasisi za Muungano, kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufunga ofisi zake Zanzibar.
 
Ukweli ni kwamba hata viongozi wengi wa CCM, wakiwemo wabunge na wawakilishi kutoka Zanzibar, wanaona kero hizi zimefurutu ada na wamesikika wakilalamika namna ambavyo Muungano unavyoendeshwa.
 
Unapotembelea taasisi za Muungano zilizopo Zanzibar, zaidi ya asilimia 90 ya waajiriwa, hata wafagiaji na madereva wanatoka Bara na hili limelalamikiwa, kama yeye alivyolalamikia Wapemba wanaolima vitunguu Bara.
 
Lakini pia wapo watu wa Bara ambao wanafanya kazi Visiwani ambazo sio vizuri kuzitamka hadharani, lakini hata maofisa wanaotarajiwa kuwa mfano wa utawala bora, kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanadaiwa "kilimo" cha aina yake Visiwani.
 
Rais Kikwete aliwahi kufanya kazi Zanzibar na anaelewa usemi maarufu wa Visiwani wa “funika kombe mwanaharamu apite”. Lakini pia ipo hatari kwamba unapolifunua kombe na mwanahalali akasimama huwa hatari zaidi.
 
Ni vizuri kwa Rais Kikwete na viongozi wengine kuchagua maneno wanayosema, badala ya kutoa hotuba ambazo zinaweza kujenga chuki za kuwagawa Watanzania.
 
Waasisi wa Muungano, Mwalimu Julius Nyerere (Tanganyika) na Abeid Amani Karume (Zanzibar) walichanganya mchanga kuimarisha umoja wa nchi mbili (ingawa wengine, kama Waziri Mkuu Mizengo Pinda hawataki kusikia Zanzibar ikiitwa nchi… nawapa pole kwa hili).
 
Sasa Watanzania wamechanganya damu kuimarisha umoja wao, lakini kuchanganya damu isiwe nongwa ya mkubwa kumpanda kichwani mdogo au mdogo kudeka kwa mkubwa wake. Usawa wa kweli lazima uonekane.
 
Hivi sasa nchi yetu ipo njia panda ya kutafuta katiba mpya. Sio vyema atokee mtu mmoja (hata awe rais, imamu au askofu) atuamulie jambo zuri analoliona yeye.
 
Hata miaka ya nyuma wananchi walikuwa wakipewa fursa ya kuamua mambo yao na pia kuna wimbo ambao ninaamini Rais Kikwete (kama walivyo vijana waliokuwa na klabu ya Saigon, Dar es Salaam) anaujua vizuri unaosema “amueni wenyewe wananchi”.
 
Kwa heshima na taadhima, namuomba Rais Kikwete akae pembeni kuwaachia wananchi kuamua na sio anasema wananchi wapo huru kuamua wanachokitaka ilhali anaweka chumvi au sukari kwenye chakula kinachopikwa.
 
Rais naye atakuwa na haki yake wakati wa kupiga kura ya maoni na angojee wakati huo kama wananchi wengine watakavyofanya wakati ukifika aitumie haki hiyo ya kikatiba.
 
Wajumbe wa Bunge Maalumu, lazima wawe na hekima na kuacha kutunishiana misuli au kuonyesha ujuaji. Busara ndiyo itatuvusha kwenda kwenye salama na amani.
 
Historia haitawasamehe duniani na akhera wale wanaotaka kuburuza wengine iwe kwa kutumia vitisho au rushwa ndani na nje ya Bunge.
 
Kauli za tunawajua wasaliti au tutapambana na wanaokwenda kinyume na msimamo wa chama zimepitwa na wakati. Watu siku hizi hawaogopi siasa zenye vitisho, bali wanaogopa kwenda kinyume na kufanya matendo ya haki na kudhulumu wananchi.
 
Kwa wale wanaofikiri wanaweza kutoa amri, kama vile wanaongoza gwaride la kijeshi, wajue wanaweza kufanya hivyo kwenye jeshi na sio uraiani. Umma unaongoza kwa hoja na hekima na sio amri ya “kushoto, kulia” au “kaa chini”. Umma ukiamua ndio umeamua.
 
Chanzo : Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles