Na Miza Kona, maelezo
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wameishauri Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupiga marufuku biashara ya uingizwaji wa Kuku kutoka nje ya nchi ili kuwawezesha Wananchi wa Zanzibar kufanya biashara hiyo.
Wamesema kwa vile biashara hiyo imedumaza juhudi za Wazawa kujiajiri wenyewe hivyo ni vyema Serikali kupiga marufuku ili kutoa nafasi za ajira kwa Wazawa.
Wajumbe hao wametoa kauli hiyo walipokuwa wakichangia Bajeti ya Waizara ya Mifugo na Uvuvi katika kikao cha Bajeti kinachoendelea katika Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanizibar.
Mmoja ya Wajumbe hao Hamza Hassan Juma amesema kuiondoa Biashara hiyo hakutosababisha matatizo yoyote katika Sheria za kimataifa hasa ikizingatiwa kuwa Suala la uingizwaji wa Kuku lilipitia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amefahamisha kuwa licha ya Bunge kuidhinisha bishara hiyo siku za nyuma chini ya Waziri David Matayo lakini kwa upande wa Bara bishara hiyo haifanyiki.
“Wenzetu Bara ndio ambao walihusika kuidhinisha Biashara hiyo lakini cha kushangaza wao wameipiga marufuku kwa nini nasisi tusiiondoe ili kuwawezesha Wananchi wetu kujipatia ajira?” Alisema Hamza.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Viti Maalum Asha Bakari Makame ameiomba Serikali kukubali matakwa ya Wakalishi hao ili kuinua biashara ambayo inaweza kufanywa na Wazawa hasa kinamama.
Amedai kuwa Afya na ubora wa Kuku hao pia unatia mashaka hivyo ni vyema Wenyeji Wakaachiwa kufanya biashara hiyo ili kuzidi kuongeza fursa za ajira kwa Wazanzibari hasa kinamama.
Akijibu hoja za Wawakilishi hao Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdillah Jihad Hassan amesema biashara hiyo inafanyika kutokana na Wafanyabiashara Wazawa kutotimiza kiwango cha mahitaji ya Kitoweo cha Kuku kinachotakiwa Zanzibar.
Amesema kutokana na hoja hiyo na kwa vile sheria zinaruhusu Serikali iliamua kuwaruhusu wawekezaji kuingiza Kuku hao wanaotoka nje ya Nchi.
Kwa upande wake Wazir
i wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Mohammed Aboud Mohammed amesema Serikali haiwezi kupiga marufuku biashara hiyo bila kufanya tathimini ya kutosha.
Amesema kwa Vile Kuku hao huingizwa nchini kwa kufuata taratibu zote ikiwemo pia ya kujua ubora na Afya zao ni vyema Suala hilo likapatiwa muda kabla ya kufanyiwa uamuzi.
Kutokana na kuibuliwa hoja hiyo bila kupatiwa ufumbuzi Baraza limeghairishwa hadi Jumatatu ili kupatikana muda wa kutosha wa kujadili Bajeti hiyo.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR 26/07/2013