Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi akiufungua Mkutano Mkuu wa Vijana Chipikizi wa CCM Wilaya hiyo hapo Ukumbi wa CCM Jimbo la Kitope uliopo Kinduni.
Picha na Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMKR
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema Vijana wa Umoja wa Vijana Chipukizi wa CCM ndio tegemezi kubwa katika kuona Taifa la Tanzania linaendelea kuongozwa katika misingi ya amani na utulivu.
Mama Asha ambae pia ni mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Kaskazini “B “ alisema hayo wakati akiufungua Mkutano Mkuu wa Umoja wa Vijana Chipukizi wa CCM Wilaya ya Kaskazini B uliofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya CCM Jimbo la Kitope iliyopo Kinduni.
Alisema iwapo taifa halitajizatiti katika kuwaanda vijana kwa ajili ya Uongozi wa hapo baadae mifarakano inayoendelea kuandaliwa hivi sasa kwa kisingizio cha dini inaweza kujaleta balaa katika jamii hapo baadae.
Mama Asha alifahamisha kwamba mifarakano hiyo licha ya kwenda kinyume na maamrisho ya hiyo dini yenyewe lakini pia inapingana na ile azma ya waasisi wa Taifa hili ya kuwaandalia mazingira mazuri ya maamuzi wananchi kwa kuleta ukombozi.
“ Waasisi wetu walipigania kujikomboa na madhila ya wakoloni ambayo baadhi ya watu wanakuwa vibaraka vya kushawishi kurejeshwa kwa mfumo huo ambao utasababisha kuwanyima wananachi walio wengi uwamuzi wa kujiamulia mambo yao wenyewe “. Alitahadharisha Mjumbne huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini “ B “.
Katika kuunga mkono harakati zao Vijana hao wa Chipukizi Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Kaskazini B Mama Asha Suleiman Iddi amechangia Shilingi Milioni 1,000,000/- kwa ajili ya Wajumbe wote 150 wa Mkutano Mkuu wa Chipukizi Wilaya ya Kaskazini B.
Mama Asha pia alikabidhi mchango wa shilingi Laki 200,000/- kwa Kikundi cha Dufu cha Kijiji hicho, Shilingi Laki 200,000/- kwa Kikundi cha maigizo pamoja na kuahidi kutoa sare kwa Wajumbe wote 150 wa Mkutano huo Mkuu wa Chipukizi Wilaya.
Naye kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Se
if Ali Iddi alichangia jumla ya shilingi Laki 500,000/- kusaidia kufanikisha Mkutano huo Mkuu wa Vijana wa Chipukizi Wilaya ya Kaskazini “ B”.
Akitoa Taarifa fupi ya Umoja wa Vijana Chipukizi Wilaya ya Kaskazini B Mwenyekiti wa Umoja huo Ali Khamis alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ndani ya unoja huo kuwa ni pamoja na uanzishwaji wa kikundi cha kujitolea kilichojikubalisha kunadi ilani ya CCM wakati wote.