Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Kiwanda cha Sukari Chahujumiwa Tena

$
0
0
Na Asya Hassan
EKARI mbili za miwa zilizotarajiwa kuzalisha sukari mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu katika kiwanda cha sukari Mahonda, zimeteketezwa kwa moto na watu wasiojulikana.

Tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 5:00 asubuhi ambapo moto huo uliteketeza ekari hizo zikiwa na thamani ya tani 70 za miwa zilizotarajiwa kuzalisha tani saba za sukari.

Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Krishinar Narayan, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika shamba hilo liliopo Zingwezingwe Mahonda wilaya ya kaskazini 'B' Unguja.

Alisema kitendo kilichofanywa na watu hao hakileti taswira nzuri na ni cha hujuma kwa kiwanda hicho kwani kiwanda kimepanga kuzalisha sukari kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi wa Zanzibar.

Alisema ekari zilizoteketezwa zina thamani ya dola za Marekani 32,200.

Akizungumzia ukubwa wa miwa hiyo, alisema miwa iliyoteketezwa ilikuwa na umri wa miezi 10 ambayo ilikuwa inatarajiwa kuvunwa mwishoni mwa mwezi Julai.

"Miwa iliyochomwa ilikuwa tayari mwisho wa mwezi huu ivunwe, lakini kutokana na kuungua miwa hiyo haifai tena,” alisema.


Alisema tukio hilo sio la kwaza kutokea katika kiwanda hicho kwani mwanzo lilitokea mwishoni mwa mwaka uliopita na kuteketeza ekari 18 za miwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, kunaonekana kuna njama maalum za kuhujumu uzalishaji wa sukari.

Alisema lengo la kiwanda ni kuhakikisha Zanzibar inaondokana na uingizaji wa sukari, lakini lengo hilo halitafanikiwa kama wananchi wataendeleza hujuma.

Kwa upande wa Meneja wa ulinzi, Adam Zakaria, alisema mlinzi wao akiwa katika harakati za kufanya doria katika mashamba hayo aliona moshi mkubwa ukitoka katika shamba hilo na baada ya kusogelea aligundua kuwa ulikuwa moto.

Alisema moto huo ulikuwa mkubwa na walipofika katika eneo hilo waliona kulikuwa na alama za watu kukata majani lakini hakuwaona.

Alisema mara baada ya kufanikiwa kuzima moto waliiona gari aina ya keri ambayo ilikuwa inakwenda kuchukua majani na ndipo walipomkamata dereva na kumuhoji na kuwaelekeza watu waliokata majani hayo.

Alisema watuhumiwa wapo kituo cha polisi Mahonda kwa upelezi zaidi.


Nae Ofisa zimamoto wa kiwanda hicho, Haji Jumbe Haji, alisema baada ya kuuona moto huo waliwasiliana na kikosi cha zimamoto na uokozi lakini walipofika walikuta moto huo ushazima kutokana na mvua iliyonyesha nyakati za mchana. 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>