Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Maalim Seif : Kuungua kwa studio za Radio Al-Noor Fm, ni pigo kwa waislamu

$
0
0
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia mmoja kati ya misahafu mitatu iliyonusurika kuungua moto, kufuatia kuungua kwa studio za Radio Al-Noor tarehe 09/04/2014. Mbele yake ni Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency Sheikh Nadir Mahfoudh.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiangalia mmoja kati ya misahafu mitatu iliyonusurika kuungua moto, kufuatia kuungua kwa studio za Radio Al-Noor tarehe 09/04/2014. Mbele yake ni Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency Sheikh Nadir Mahfoudh.

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency Sheikh Nadir Mahfoudh, baada ya kutembelea studio za kituo hicho zilizoungua

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akiagana na Mkurugenzi wa Radio Al-Noor Sheikh Mohd Suleiman baada ya kutembelea  studio za kituo hicho zilizoungua. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency Sheikh Nadir Mahfoudh, na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Mhe. Abdallah Mwinyi. (Picha na Salmin Said, OMKR)
 
 
Na Hassan Said OMKR
 
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kuungua kwa studio za Radio Al-Noor Fm, ni pigo kwa waislamu wa Zanzibar na Taifa kwa ujumla.
 
Amesema kituo hicho ni muhimu katika kutoa taaluma mbali mbali zikiwemo zile zinazohusiana na  maadili ya kiislamu, jambo ambalo pia linaisaidia serikali katika kurejesha maadili mema kwa jamii.
 
Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo wakati akitembelea studio hizo zilizoko katika jengo la msikiti wa “Masjid Sahaba”, Mtoni Kidatu Zanzibar.
 
Amesema Radio hiyo imekuwa ikitoa fursa kwa masheikh na wanataaluma kuweza kusambaza taaluma hizo kwa jamii, na kwamba wananchi wamekuwa wakijifunza na kunufaika kutokana na matangazo yake.
 
Ametoa pole kwa uongozi wa Radio hiyo na wasikilizaji wote wa Radio Al- Noor, kutokana na kuungua kwa radio hiyo, na hatimaye kukosekana kwa matangazo yake.
 
Mhe. Maalim Seif ametoa wito kwa waislamu wenye uwezo kuichangia radio hiyo ili iweze kurejesha matangazo yake kwa haraka, ambapo yeye binafsi ameahidi kuchangia shilingi milioni tano kwa ajili ya kusaidia kurejeshwa kwa huduma hiyo ya matangazo.
 
Akizungumzia kuhusu kutokuungua kwa misahafu mitatu iliyokuwa ndani ya studio namba tatu ambayo takriban vifaa vyote vilivyokuwemo viliungua na kuharibiwa vibaya, Maalim Seif alisema kitendo hicho ni cha miujiza, na kwamba ni katika uwezo wa Mwenyezi Mungu kuendelea kukilinda kitabu chake cha Qur’an.
Nae Mkurugenzi wa Radio hiyo Sheikh Mohd Suleiman, amesema tukio hilo ni mfululizo wa matukio kadhaa ya aina hiyo yaliyowahi kukikumba kituo hicho tangu kilipoanzishwa miaka mitano iliyopita.
 
“Ukweli inasikitisha kwamba matukio ya aina hii yamekuwa yakijirejea katika kituo chetu kwani siku za nyuma iliwahi kuungua studio nambari moja, baadae ikaungua studio nambari mbili na sasa imeungua studio nambari tatu na nyengine zote, ingawaje shoti ya mara hii imekuwa kubwa zaidi kuliko zote zilizowahi kutokea katika kituo chetu”, alifahamisha Mkurugenzi huyo.
 
Amesema tukio hilo lililotokea usiku wa tarehe 09 mwezi huu, limepelekea kuungua kwa studio nne za kurushia matangazo pamoja na vifaa vyake vinavyokisiwa kugharimu shilingi milioni themanini (80), ambapo studio namba tatu pekee inafikia gharama ya shilingi milioni 52.
 
Chanzo cha kuungua kwa studio hizo kinasadikiwa kutokana na hitilafu za umeme, ambapo Mkurugenzi huyo alisema mripuko ulitokea maara baada ya kuwashwa kwa umeme ambao ulikuwa umezimwa.
 
Kituo cha Radio Al-Noor  ni miongoni mwa taasisi kadhaa za kiislamu zinazoendeshwa na jumuiya ya Al-Noor Charitable Agency, chini ya Mkurugenzi Mkuu Sheikh Nadir Mahfoudh.
 
Akizungumzia tukio hilo Sheikh Mahfoudh amesema ni tukio la kusikitisha, lakini wana matarajio ya kurejea kwa huduma za matangazo katika siku chache zijazo, na kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuwapunguzia gharama za umeme, ikizingatiwa kuwa Radio hiyo haijiendeshi kibiashara.
 
Wakati huo huo Maalim Seif amemtembelea mtangazaji wa Radio hiyo aliyelazwa katika hospitali kuu ya Mnazi Mmoja ustadh Aboubakar Fakih ambaye alijeruhiwa baada ya kujitupa kutoka kwenye ghorofa, baada ya kutokea mripuko mkubwa kwenye jengo hilo.
 
Maalim Seif pia aliwatembelea na kuwajuilia hali wagonjwa wengine waliolazwa katika wodi hiyo nambari nne gharofa ya pili ya wagonjwa waliopatwa na ajali mbali mbali.
 
Kwa mujibu wa daktari wa zamu wa hospitali hiyo dokta Said Omar, mgonjwa huyo ambaye amepata majeruhi katika miguu yake yote miwili pamoja na mkono wa kulia, hali yake inaendelea vizuri.
 
Hata hivyo amesema atalazimika kubakia hospitalini hapo kwa kipindi kisichopungua miezi miwili, na kuelezea matumaini makubwa na kuweza kupoa na kuendelea na shughuli zake.
 
 

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>