Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dk. Shein asisitiza vipaumbele. Ni matumizi fedha za serikali

$
0
0
Na Said Ameir, IKULU
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, amesisitiza umuhimu wa Wizara na Idara za Serikali kuzingatia vipaumbele katika matumizi ya fedha za umma hususan yanapokuja masuala yanayowagusa wananchi.

Alisema hayo wakati wa mkutano wa kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpangokazi wa Wizara ya Afya katika kipindi cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2013/2014.

“Tunahitaji kuwa makini zaidi wakati tunapopanga matumizi ya fedha katika wizara na kwa wakurugenzi hawana budi kuhakikisha kuwa maeneo yao ya kipaumbele hasa yale yanayogusa wananchi moja kwa moja yanapewa umuhimu wa kwanza,” alisema.

Katika mkutano huo pia alisema serikali imedhamiria kuendelea kuongeza fedha za bajeti kwa matumizi ya kununulia chakula kwa wagonjwa wanaolazwa katika hospitali nchini.

Aliutaka uongozi wa hosptali hizo kuhakikisha kunakuwepo uangalizi mzuri wa matumizi ya fedha ili ziweze kuwafikia walengwa ipasavyo.


“Serikali tutaendelea kuongeza bajeti ya chakula kwa ajili wa wagonjwa lakini ni lazima viongozi wa hospitali wahakikishe fedha hizo zinatumika ipasavyo kuanzia manunuzi, upishi hadi kinavyowafikia wagonjwa,” alisema.

Aliongeza kuwa ni muhimu kwa hospitali nchini ikiwemo ya Mnazi Mmoja kuajiri wataalamu wa lishe kwani sio tu kutasaidia kupunguza gharama za chakula bali pia kuwapatia wagonjwa chakula wanachostahili kulingana na mahitaji ya afya zao.

Aliiagiza wizara hiyo kufanya utafiti wa matumizi ya tumbaku katika visiwa vya Unguja na Pemba ili kuona mwenendo wa utekelezaji wa sheria ya Zanzibar ya afya ya jamii ya mwaka 2012 pamoja na azimio la Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusu matumizi ya tumbaku.

Aidha aliuagiza uongozi wa wizara ya afya kutosita kufanya manunuzi ya dharura ya dawa au vifaa vya tiba pale inapotokezea haja ya kufanya hivyo ili kuokoa maisha ya wagonjwa badala ya kusubiri utaratibu mwingine ukiwemo wa kusubiri misaada.

Alisema mfumo wa biashara wa kisasa unarahisisha kufanya mambo mengi na kwa haraka, hivyo siyo vizuri kusubiri misaada kwa yale mambo ambayo yamo ndani ya uwezo wa serikali.

Rais wa Zanzibaralirejea wito wake wa kuzitaka taasisi za umma ikiwemo wizara ya Afya kujenga utamaduni wa kulipia huduma za umeme na maji zinazotumika kwenye taasisi zao ili huduma hizo ziweze kuwa endelevu.

“Tunapodaiwa ni lazima tulipe hakuna lugha nyengine ya kuzungumza kwa kuwa hiyo ni biashara na kwamba Shirika la Umeme Zanzibar lenyewe linanunua umeme kutoka TANESCO na lisipolipa tutakatiwa umeme na sote tutakosa huduma hiyo,” alisisitiza.

Awali akiwasilisha taarifa hiyo ya utekelezaji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk. Mohamed Saleh Jidawi, alisema kwa ujumla imeweza kutekeleza mengi ya majukumu yake katika kipindi husika kama yalivyoainishwa katika mpangokazi wa wizara hiyo pamoja na baadhi ya maagizo yaliyotolewa katika kikao kamahicho kilichofanyika mwezi Novemba 2013.


Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>