Na Mwandishi wetu
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, amekemea tabia ya baadhi ya watu wanaotorosha kwa magendo miche ya mikarafuu na kuipeleka nje ya nchi.
Alisema kitendo hicho hakikubaliki na ni janga kubwa ambalo halina budi kupigwa vita kwa nguvu zote.
Alisema hayo jana katika siku ya upandaji miti kitaifa, iliyofanyika katika barabara ya Cheju-Unguja Ukuu mkoa wa kusini Unguja.
Aidha alisema serikali itaendelea kuwapa motisha wakulima wa mikarafuu ili kuinua uchumi na maisha yao na kuinua pato la taifa kwa jumla.
Ili kuhakikisha zao la mikarafuu linaimarika, alisema serikali inaendelea kutoa miche bure na vivutio vyengine, ili kuhakikisha wakulima wanafaidika na jasho la kazi yao .
Aliwataka wananchi kupanda mikarafuu pamoja na mazao mengine yakiwemo ya viungo na matunda kwa sababu haiba na mandhari njema ya Zanzibar yataendeela kuwa mazuri iwapo upatikanaji wa matunda mbali mbali na viungo utaendelea kushamiri.
Alisema uzinduzi uliofanywa katika katika barabara ya Jendele hadi Unguja Ukuu ni muendelezo wa kampeni ya upandaji miti katika barabra na maeneo mengine ya jamii.
Lengo alisema ni kuhakikisha miti inapandwa katika barabara zote za Unguja na Pemba na kuhakikisha barabara zinakuwa katika mandhari nzuri kama ilivyo katika baadhi ya maeneo kama vile Bungi.
Alitoa wito kwa skuli na vyuo kupanfiwa program maalum ya kupanda na kutunza miti kwa wingi.
Aliwaasa wananchi kuacha tabia ya kukata miti katika viwanja wanavyokusudiwa kujengwa nyumba zao badala yake wahakikishe nyumba wanazojenga zinazungukwa na miti kwa kuihifadhi iliyopo na kupanda mingine.
“Wakati mzuri wa kupanda miti ili istawi na kukua ni nyakati za misimu ya mvua, hivyo tuzitumie mvua hizi kupanda miti kwa wingi kama itakavyo wezekana,” alisema.
Alisema serikali kwa kushirikiana na jamii pamoja na vikundi vya kuhifadhi mazingira imedhamiria kupanda miti katika maeneo mbali mbali ikiwemo hayo ya barabara.
Alisema jumla ya kilomita 50 za barabara tayari zimepandwa miti katika Wilaya zote za Unguja na Pemba .
Alisema ulimwengu umehamanika kutokana na matatizo makubwa yanayosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa hivyo uhifadhi wa mazingira ni sehemu ya suluhisho la kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira ambazo zinasababisha mabadiliko ya hali ya hewa yasiyotarajia.
Alisema juhudi kubwa hazina budi kuchukuliwa katika kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu na thamani ya miti kijamii, kiuchumi na kimazingira na kuonya kwamba majanga mengi ya kimazingira yataendelea kutokea ikiwa jamii itaendelea kukata miti hiyo ovyo na bila ya utaratibu.