STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 22 Aprili , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar kwa kuweza kufikia malengo yaliyowekwa ya kukusanya mapato katika kipindi cha miezi tisa iliyopita kuanzia mwezi Julai 2013 hadi Machi 2014.
Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 133.9 lakini imevuka lengo na kukusanya jumla ya shilingi bilioni 134.6 ambacho ni sawa na asilimia 100.51 ya lengo.
Kwa upande wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar ilipanga kukusanya jumla ya shilingi milioni 127.6 na imeweza kukusanya jumla ya shilingi milioni 110.5 ambazo ni asilimi 90.
Akizungumza katika kikao maalum cha kujadili utekelezaji wa mpango kazi na bajeti ya Wizara ya Fedha kwa kipindi cha miezi tisa kuanzia Julai 2013 hadi Machi 2014, Dk. Shein amesema kwa ujumla ameridhishwa na utendaji kazi wa Wizara hiyo na hasa taasisi zinazokusanya mapato kwani amesema bila ya kukusanya kodi ipasavyo, inakuwa vigumu kutekeleza majukumu ya serikali.
“Hatuwezi kuendesha serikali bila ya kuwa na fedha, fedha haziwezi kupatikana bila ya kuwa na mipango mizuri ya kuzikusanya, serikali zote duniani zinaendeshwa kutokana na kukusanya kodi”, alisema Dk. Shein.
Aidha, aliipongeza kamati ya ukomo ya bajeti kwa kuweza kuzigawa vizuri fedha zinazokusanywa kwa ajili ya kufanyiwa matumizi kulingana na vipaumbele vilivyowekwa na serikali.
“Naipongeza pia “ceiling committee” kwa kazi nzuri iliyofanya katika kuzigawa fedha zilizokusanywa kwa mujibu wa vipaumbele tulivyoviweka, tumekusanya vizuri na tumezigawa vizuri na hivyo utekelezaji katika kipindi cha miezi tisa umekwenda vizuri” aliongeza.
Rais wa Zanzibar amesema hali ya ukusanyaji wa mapato Zanzibar imekuwa ikiendelea kuleta matumaini hasa ikilinganishwa na miaka iliyopita ambapo alisema mwaka 2010/2011 ukusanyaji wa mapato ulikuwa kati ya shilingi bilioni 13 na 14 kwa mwezi ikionesha tofauti kubwa na sasa ambapo makusanyo yanafikia wastani wa shilingi bilioni 29 na 30 kwa mwezi.
Mapema akiwasilisha taarifa ya Wizara hiyo, Katibu Mkuu wizara ya Fedha Ndugu Khamis Mussa Omar amesema katika kipindi cha miezi tisa Julai 2013 hadi Machi 2014, Wizara ya Fedha kama zilivyo taasisi nyengine za Serikali imeweza kukusanya jumla ya shilingi 3,117 milioni sawa na asilimia 52.9 ya makadirio ya mwaka ya shilingi 5,891 milioni.
Aidha, amesema katika kipindi hicho hicho Idara ziliweza kutumia jumla ya shilingi 4,220.84 milioni kati ya shilingi 6,874.13 milioni zilizotengwa kwa kazi za kawaida kwa mwaka 2013/2014 ambazo ni sawa na asilimia 61.4 ya makadirio ya mwaka mzima.
Kwa upande wa kazi za maendeleo jumla ya shilingi 1,147.06 milioni zilitumika kwenye miradi mbali mbali ya maendeleo ikilinganishwa na shilingi 2,540.00 milioni zilizoombwa kwa robo tatu za mwaka ambazo ni sawa na asilimia 45.2 ya maombi au asilimia 13.6 ya makadirio ya mwaka.
Malengo ya msingi ambayo Wizara hiyo ilijiwekea katika kipindi cha miezi tisa iliyopita ni pamoja na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kufikia kiwango cha asilimia 20 ya pato la taifa, kwa kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato na kuendeleza elimu kwa walipa kodi.
Vile vile Wizara hiyo ilidhamiria kuendelea na udhibiti wa matumizi ya serikali na kuhakikisha kuwa kunakuwepo na thamani halisi ya matumizi yanayofanywa “value for money” katika utekelezaji wa shughuli na serikali pamoja na kuendelea kulipa mishahara na mafao ya wastaafu kwawakati mambo ambayo yote yametekekelezwa kama yalivyopangwa.
Wizara ya Fedha ilieleza taarifa hiyo imeendelea kufanya uhakiki wa mali za serikali sambamba na kuwaandalia wafanyakazi mazingira bora na hivyo kuweza kutoa huduma bora za kiufundi na kiutawala zinazosimamiwa na idara mbalimbali za Wizara hiyo.
Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi ni mfululizo wa vikao vya Wizara mbali mbali vinavyoafanyika Ikulu chini ya Uenyekiti wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein vinavyotathmini utekelezaji wa mipangokazi na bajeti kwa kipindi cha miezi tisa Julai 2013 hadi Machi 2014.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822