Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hali ya Kisiasa ya Muungano wa Tanzania: Tulikotoka, tulipo na tuendako

$
0
0
HALI YA KISIASA YA MUUNGANO WA TANZANIA: TULIKOTOKA, TULIPO NA TUENDAKO 
Ndg.RASUL AHMED 

MHADHIRI IDARA YA SIASA NA UTAWALA, CHUO KIKUU DAR ES SALAAM

MADA ILIYOWASILISHWA KWENYE KONGAMANO LA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR KATIKA KUADHIMISHA MIAKA 50 YA MUUNGANO

19 APRILI, 2014

ZANZIBAR

  1. UTANGULIZI

 Mnamo tarehe 26 Aprili ya Mwaka huu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utatimiza miaka hamsini (50) ya uhai wake. Huu ni muungano wa kipekee kabisa ambao umevuta hisia ndani na nje ya bara la Afrika. Hisia hizo zinaweza kuwa zimeelekea kwenye maeneo mengi lakini kwa mtazamo wa haraka, yako maeneo mawili makuu: kuendelea kudumu kwa muungano huu na muundo wake. Muungano huu ni wa kipekee pia kwa kuwa  ulikuja kwa njia ya maridhiano baina ya pande mbili zilizoungana. Uzoefu wa nchi nyingi zilizoungana duniani ni kwamba hatua ya kuungana ilifuata matukio ya kupigana na kumwaga damu, yaani kwa mtutu wa bunduki.


Miaka hamsini ya Muungano ni safari ndefu iliyopitia na kushuhudia maendeleo, mageuzi, misukosuko na changamoto kadhaa za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiteknolojia nakadhalika. Tathmini iliyokamilika kuhusu Muungano ulipotoka, ulipo na unapokwenda ni ile inayotazama maeneo yote hayo kwa undani, yaani kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Mada hii lakini imejikita katika eneo moja tu la kisiasa. Bado neno kisiasa linabeba dhana pana ambayo inaweza kujumuisha masuala yenye sura za mifumo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia. Hivyo ipo haja ya kutoa ufafanuzi kuhusu dhana ya ‘Hali ya Kisiasa ya Muungano’ tunayomaanisha. Hali ya Kisiasa hapa itamaanisha masuala yafuatayo- muktadha wa kisiasa kabla na baada ya muungano kufikiwa; harakati za kisiasa zilizopelekea kuundwa kwa muungano; maendeleo, mafanikio, mageuzi, misukosuko na changamoto za mfumo wa kisiasa tangu kuzaliwa kwa muungano mpaka leo hii unapotimiza miaka hamsini.



Mfululizo wa mada hii upo katika sehemu kuu sita. Kufuatia utangulizi huu sehemu ya pili inatazama kipindi cha harakati za kuondokana na ukoloni mpaka uwepo wa nchi ya Tanzania. Sehemu ya tatu inaangalia safari ya muungano toka 1964 mpaka 1984 iliposemekana hali ya kisiasa ilichafuka visiwani Zanzibar. Matukio ya kipindi kigumu kisiasa kwa uongozi wa juu wa nchi yalijitokeza tena mwanzoni mwa miaka ya tisini kulipojitokeza kundi la G55. Sehemu ya nne inamulika matukio hayo na mengine muhimu ya kisiasa. Sehemu ya tano inaangaza matukio baada ya vuguvugu la G55 mpaka mjadala wa sasa wa katiba mpya. Hitimisho la mada linahusu mustakabali wa muungano wenyewe kwa kizazi hiki na kijacho.


  1. KABLA YA 1964: Harakati za Kujikomboa na Kuondokana na Ukoloni mpaka Kuwepo Tanzania

 Historia na makala za wanazuoni zinatuthibitishia kwamba mahusiano ya jamii za watu wa iliyokuwa Tanganyika na Zanzibar ilianza zama za kale, karne nyingi zilizopita. Mahusiano hayo ya kihistoria si tu yaligusa undugu au mahusiano ya kijamii (blood ties),  bali yameendelea kujitokeza katika njanja nyingi kama kibiashara, kiutamaduni na kwenye ulingo wa kisiasa. Wako wanazuoni waliodokeza kwamba Wahidimu na Watumbatu walitokea iliyokuwa Tanganyika[1]. Tanganyika na Zanzibar pia zinafanana kwa namna mipaka yake ilivyopatikana. Maeneo ya Tanganyika na Zanzibar yaliwekwa na wakoloni kama ilivyofanyika sehemu nyingine barani Afrika. Wakati mipaka ya Tanganyika ikiwekwa awali na wakoloni wa kijerumani, himaya ya Zanzibar iliwekwa ramani yake na wakoloni wa kiarabu kabla ya kupunguzwa na waingereza na baadaye wajerumani.

Jambo lingine muhimu kulizungumza japo kwa muhtasari ni kwamba vuguvugu la harakati za kujikomboa na kuondokana na minyororo ya ukoloni kwa pande zote mbili ilishika kasi miaka ya 1950. Kipindi hiki kilishuhudia wanaharakati mashuhuri wa pande hizi mbili wakikutana visiwani Zanzibar na kwingineko Afrika kwa lengo kuu moja la wakati huo-ukombozi wa jamii zao. Itakumbukwa kwamba hata kabla ya mahusiano ya vyama vya Afro Shirazi Party (ASP) na Tanganyika African National Union (TANU) hayajafanywa rasmi baadae miaka ya 1960, viongozi wanaharakati walipata fursa ya kukutana katika mikusanyiko kama ya PAFMECA (Pan-African Movement for East and Central Africa) iliyofanyika sehemu tofauti za Afrika mashariki na kati. Kwa mfano mkutano wa PAFMECA uliofanyika Mwanza mwaka 1958  ulihudhuriwa wanasiasa mashuhuri wakiwemo kutoka visiwani Zanzibar[2]. Mkutano wa pili wa PAFMECA ulifanyika Zanzibar  April 1959 na msisitizo uliendelea kushawishi vyama vya ASP na ZNP kuunganisha nguvu na juhudi hizi zilichangia kuanzishwa Kamati ya Ukombozi (Freedom Committee) japo haikudumu kwa muda mrefu[3].


Pilika zilizopelekea  kujipatikana uhuru wa Tanganyika mnamo Disemba ya 1961; harakati, mbinu za kujiongezea ufuasi katika chaguzi; giliba za kisiasa wakati wa Zama za Siasa Zanzibar, na hatimaye Mapinduzi ya 1964 visiwani yameelezwa kwa mitazamo tofuati katika makala kadhaa. Si nia ya mada hii kurudia kwa ukamilifu masimulizi ya matukio yaliyotufikisha kwenye uhuru wa Tanganyika wa 1961 na mapinduzi ya Zanzibar ya 1964. Ifahamike kwa ufupi tu kwamba yale mawasiliano ya viongozi wa vyama ya TANU na ASP yaliendelea pia baada ya mapinduzi na kupelekea kuungana 1964. Sehemu inayofuata inatazama lengo la kuungana na mengine yaliyojitokeza katika miongo miwili ya kwanza ya Muungano (yaani 1964-1984).


  1. 1964-1984: Sherehe za Kuchanganya Udongo wa Nchi Mbili mpaka ‘Kuchafuka kwa Hali ya Kisiasa Visiwani’

Kama ilivyobainishwa hapo awali mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari 1964, viongozi wa  Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Julius K. Nyerere na Sheikh Abeid A. Karume walianza mazungumzo yaliyolenga kuziunganisha nchi hizo mbili. Mbali na kutetea au kukosoa namna mazungumzo ya viongozi hawa yalivyoendeshwa, kumbukumbu za kihistoria zinatuonyesha mazungumzo yao yaliendeshwa kwa faragha kutokana na unyeti wa suala lenyewe na mazingira ya wakati huo ya vita baridi. Hatimaye Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume walifikia makubaliano ya kuziunganisha nchi zao na kuamua kusaini Mkataba wa Muungano kati ya Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar (The Articles of the Union between the Republic of Tanganyika and the People’s Republic of Zanzibar) (utaitwa “Mkataba wa Muungano”). Mkataba wa Muungano ulitiwa saini huko Zanzibar tarehe 22 Aprili 1964. Sherehe rasmi za Muungano zilifanyika mnamo tarehe 26 Aprili 1964, moja ya matukio ikiwa ni kuchanganywa kwa udongo ikiashiria kuungana kwa nchi mbili.


Makala nyingine za wachambuzi na wasomi, zimejaribu kuchambua malengo halisi ya vinara hawa wawili wa muungano. Kama kweli walifanya maamuzi kwa msukumo ama wa kiusalama wa ndani au wa nje, ama miskumo wa kiumajumui wa Afrika ama vyote kwa nafasi na viwango tofauti, bado ni mjadala unaoendelea. Tunaweza kuafiki kwamba kumekuwa na uthubutu wa wasomi zama hizi kubainisha katika maandiko yao kauli zilizoonyesha hisia za wakati huo, hususan baada ya waasisi hawa kuondoka duniani. Kauli kama “Koti likikubana livue”[4]inayodaiwa kutolewa na Mzee Karume; “If I could tow that island out into the middle of the Indian Ocean, I’d do it”[5]iliyodaiwa kutolewa na Mwalimu Nyerere, zimekuwa zikirudiwa haswa katika miongo miwili iliyopita. Lakini madhumuni ya kuungana yaliwekwa wazi kwenye utangulizi wa Mkataba wa Muungano kama ifuatavyo:


Whereas the Governments of the Republic of Tanganyika and of the People's Republic of Zanzibar, being mindful of the long association of the peoples of these lands and of their tics of kinship and amity, and being desirous of furthering that association and strengthening these tics and of furthering the unity of African peoples, have met and considered the union of the Republic of Tanganyika with the People's Republic of Zanzibar[6].

Kwa ufupi, sababu kubwa mbili za kuungana kwa mujibu na utangulizi huo ni ushirikiano wa muda mrefu wa kirafiki na udugu miongoni mwa watu wa nchi hizo mbili, na pia nia ya kutaka kuuendeleza uhusiano huo na kuzidisha umoja wa Kiafrika.


Katika kipindi cha miongo miwili ya kwanza tangu mkataba wa muungano kusainiwa  mambo mengi yaliyogusa uendeshaji wa muungano wa Tanzania yalitokea. Kisiasa nchi ilipitia mabadiliko ya kikatiba kutoka katiba ya muda ya 1965 iliyodumu mpaka 1977, kuuwawa kwa Sheikh Abeid Amani Karume (April 7 1972), pamoja na kuungana kwa vyama vya ASP na TANU na kuunda chama kimoja, Chama cha Mapinduzi (CCM).  Kipindi hichi cha chama kushika hatamu kilishuhudia kuanza kwa zoezi la kuongeza mambo ya Muungano baada ya jumuiya ya Afrika Mashariki kuvunjwa. Rais wa Zanzibar wakati huo Aboud Jumbe alianzisha mchakato wa katiba ya Zanzibar (Katiba ya Zanzibar ya 1979).  


Hiki pia ni kipindi ambapo muungano ulipata mtihani wake mkubwa: ni dhahiri kulijitokeza dalili  za kutoridhika na muundo wa muungano hasusan kwa upande wa visiwani. Hii ilitafsiriwa na uongozi wa juu wa chama tawala wakati huo kama ‘kuchafuka kwa hali ya kisiasa visiwani’[7]. Kwa sasa tunafaida ya kuangalia matukio ya wakati ule kwa utambuzi baada ya jambo kutokea (with hindsight). Kwa wakati ule dai la tafsiri ya mkataba wa muungano kama je lilidhamiria serikali mbili au tatu lilichukuliwa kama tukio la ‘kiuhaini’[8]. Mwanazuoni maarufu nchini, Issa Shivji anasema uongozi wa chama tawala chini ya Mwalimu Nyerere, ulipoteza fursa adimu ya kushughulikia kidemokrasia ujumbe wa utaifa uliojitokeza wakati ule na badala yake ‘mjumbe alifukuzwa’[9]. Matukio yalihitimishwa na mkutano maalum wa halmashauri kuu ya CCM liyojadili kuchafuka kwa hali ya kisiasa na mwishowe Aboud Jumbe alijiuzulu nyadhifa zote. Kilikuwa ni kipindi cha taharuki. Kusema ukweli, siasa zimebadilika leo hii wanasiasa wanalizungumza suala la muundo wa muungano hadharani kwenye mikutano ya hadhara, na kwenye bunge wakirekodiwa na vyombo vya habari. Bado lakini suala la muundo linazungumzwa zaidi kwa mtindo wa ushabiki wa kivyama. Tutalirejea suala hili sehemu ya tano ya mada hii.


  1. 1985-1993: Baada ya ‘Kuchafuka Hali ya Kisiasa’ mpaka Kundi la 55

Baada ya hali tete ya 1983-84 kudhibitiwa chama tawala kiliona umuhimu wa kuweka jitihada rasmi za kushughulikia matatizo na madai mbalimbali, kwa mfano kwamba Zanzibar inaburuzwa katika kufikia maamuzi yanayohusu Muungano na kwamba haipati haki sawa kiuchumi[10]. Miongoni mwa jitihada hizo ni Tume ya Chama cha Mapinduzi ikiongozwa na Dk. Salmin Amour iliundwa 1984. Pia Tume ya Rais ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1991 iliyoongozwa na Edwin Mtei iliundwa. Kamati zingine zilizoundwa ni Kamati ya Baraza la Mapinduzi (Kamati ya Amina Salim Ali- 1992) na Kamati ya Shelukindo (1994).


Kujiuzulu kwa Mzee Jumbe na kurejea kwa hali ya utulivu visiwani hakukumaanisha hoja ya kubadili muundo wa muungano ilipotea kabisa. Hoja hii iliibuka tena pale Tume ya Nyalali ilipopendekeza muundo wa shirikisho la serikali tatu. Si nia ya makala hii kurejea namna pendekezo hilo lilivyofikiwa na maoni na hoja yaliyokusanywa tume hiyo. Malalamiko ya upande wa Tanzania bara, kama yalikuwa sio dhahiri basi yaliwekwa bayana na kundi la wabunge 55 lililojulikana kama ‘G55’ ambalo mwaka 1993 lilitoa hoja bungeni ya kuundwa serikali ya Tanganyika. Hii ilikuwa baada ya taarifa za  Zanzibar kujiunga na umoja wa OIC (Organization of Islamic Conference). Mwalimu kama mmoja wa waasisi wa muungano alitafuta wasaa wakuzungumza na wabunge hao akivaa kofia ya ‘Mkulima toka Butiama’[11]. Pamoja na kufanikiwa kuwasilishwa bungeni baada ya marekebisho kadhaa bado hoja ya kundi hili ilizimwa. Je kuzimwa kwa hoja ya G55 kulileta athari gani katika jitihada za kushughulikia malalamiko kuhusu muungano? Swali hili linajibiwa sehemu inayofuata.


  1. 1994-2014: Baada ya Vuguvugu la G55 mpaka Mjadala wa Katiba Mpya

Wakati vuguvugu la G55 linaibuka na kufifia, Jamhuri ya Muungano ilikwishwa ingia rasmi katika mfumo wa siasa za vyama vingi hapo mwaka 1992. Pamoja na kufungua uwanja kwa ushiriki wa siasa za ushindani na kuongeza uhuru wa kutoa maoni, kurejea kwa mfumo huu kuliambatana na mabadiliko, mafanikio na changamoto kadhaa kwa utawala wa nchi na hivyo muungano, vyama vya siasa, wanasiasa, wananchi na wadau wengine wa mfumo wa kisiasa nchini. Tunaweza kuyaorodhesha baadhi kama ifuatavyo:

  • Kushuka kwa kasi kwa uvumilivu wa kisiasa na matokeo ya uvunjivu wa amani;
  • Kushamiri kwa siasa za migawanyiko na viashiria vya kuyumba kwa utengamano ndani ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano;
  • Kuongezeka jitahada  za kitaasisi kushughulikia ‘Kero za Muungano’;
  • Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki;
  • Mazungumzo yaliyopekea kufikiwa Miafaka Mitatu ya Zanzibar.

Sasa tuangalia japo kwa ufupi baadhi ya masuala yaliorodheshwa hapo juu. Moja ya misingi muhimu sana katika mfumo wowote wa kisiasa unaruhusu siasa za ushindani ni uvumilivu wa kisiasa. Katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa Hali ya Siasa Zanzibar uliofanyika tarehe 22 na 23 Desemba, 2009 mjini Zanzibar uliokuwa na mada kuu ya “Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa Zanzibar: Zanzibar Tuitakayo”, Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume alitoa ufafanuzi kuhusu dhana ya uvumilivu wa kisiasa kama ifuatavyo:


Kwa mtazamo wangu, uvumilivu wa kisiasa ndio msingi mkuu wa amani na maendeleo ya taifa. Uvumilivu wa kisiasa unatokana na ukweli kwamba palipo na wengi pia kuna mawazo tofauti. Tofauti ndio sifa kubwa inayowatambulisha binadamu. Kila mmoja wetu huumbwa akiwa na haiba na hulka inayomfanya atofautiane na mwenzake. Tofauti hizi za haiba na hulka huendena na tofauti za mawazo na mitazamo. Tofauti za kila mmoja wetu ni muhimu katika kujenga demokrasia. Tofauti hizi wengine huziita migogoro[12].


Karume anaendelea kufafanua kwamba “Yaliyotokea baada ya uchaguzi kwa majirani zetu Kenya, au hata Zimbabwe, ilikuwa ni dalili za kufifia kwa uvumilivu wa kisiasa”[13]. Ufafanuzi huu uliojitosheleza unahusisha dhana ya uvumilivu wa kisiasa na mambo mawili muhimu sana kwa mustakabali wa taifa: amanina maendeleo. Ieleweke kwamba dalili za kufifia kwa uvumilivu wa kisiasa kulikoendana na upanuzi wa ulingo wa kisiasa kumejitokeza si tu nchi za jirani. Hata hapa kwetu siasa za vyama vingi, mbali ya kuwa jukwaa murua la kuwakilisha na kushughulikia matakwa na kero za wananchi, zimetumika vibaya pia na kupelekea matukio kadhaa ya uvunjivu wa amani. Baadhi ya changuzi, bara na visiwani, zimeshudia matukio ya vurugu kubwa kabisa. Matukio ya  vurugu katika siasa  pia yameathiri maendeleo ya sehemu husika kwa kuwa nguvu na akili zinaelekezwa katika kusuluhisha na kuondoa vurugu badala ya kuelekezwa katika shughuli za maendeleo. Vurugu za kisiasa zilizopelekea baadhi ya wananchi kukimbilia nchi jirani mwaka 2001 zilitia doa taswira ya muungano wetu kama ‘kisiwa cha amani’ kwa jumuiya ya kimataifa.


Sambamba na kufifia uvumilivu wa kisiasa, siasa za migawanyiko zimeendelea kushamiri. Tunapendelea kutumia dhana ya siasa za migawanyiko kuliko dhana iliyotawala kauli za viongozi wa kiserekali na kisiasa haswa katika mwongo  uliopita, yaani mpasuko wa kisiasa. Nimewahi kuandika katika makala mengine kwamba si sahihi kutumia misimamo ya wapigaji kura katika sanduku la kura kila uchaguzi unapofanyika kama kielelezo cha mpasuko wa kisiasa. Nikitumia mfano wa Pemba nilieleza kwamba, “Kwa ujumla, kuna mwelekeo wa kueleza uamuzi wa wapiga kura wa Pemba kupigia kura chama cha upinzani kama kielelezo cha mpasuko wa kisiasa Zanzibar. Wakati mwelekeo huo unatoa picha fulani ya hali ya sasa, lakini unaonekana kupuuza hoja kuwa wapiga kura wa Pemba wameonyesha mtazamo wao dhidi ya mfumo wa siasa, wakionyesha kutaka mabadiliko ya kisiasa. Pia, imeonekana kuwa jamii zimekuwa zikishirikiana kwa amani, ikimaanisha kuwa uhasama wa kisiasa haujajikiita sana kwenye masuala ya jamii kama ilivyo kwenye siasa”[14].


Kwa hivyo, dhana ya siasa za migawanyo inatufaa zaidi kwa kuwa ni pana kiasi cha kujumuisha sio tu mizozo inayotokana na mitazamo tofauti ya wanasiasa na wafuasi wao, bali pia migawanyiko inayotokana na usimamizi mbovu na/au wa kiupendeleo wa sheria zilizopo hata kupelekea kuibua hisia za ubaguzi wa uraia. Hili ni moja ya nyufa zilizojitokeza katika miaka ya hivi karibuni ya muungano wetu. Kumeendelea kujitokeza mwenendo unaobidi ufuatiliwe kwa taadhari wa kusisitiza utofauti wa utanzania na uzanzibari. Kisa alichowahi simulia aliyekuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Augustino Ramadhani, kitatusaidia kufafanua hili. Bila kumumunya maneno Jaji Ramadhani anaeleza:


Mimi ni Mzanzibari nimezaliwa Zanzibar, baba na mama wamezaliwa Zanzibar, babu zangu na bibi zangu wa pande zote mbili wamezaliwa na kuzikwa Zanzibar. Ninaambiwa kuwa kwa asili, baadhi ya hao waliotangulia walitoka Masasi. Lakini simjui yeyote Masasi.



Niliteuliwa kuwa Makamu wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuwa ni Mzanzibari. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imeweka kuwa kama Mwenyekiti wa Tume anatoka upande mmoja wa Muungano basi Makamu atoke upande mwingine. Mwenyekiti, Jaji Makame, anatoka Bara hivyo niliteuliwa kuwa Makamu kwa kuwa mimi ni Mzanzibari.


Labda nielezee utata ambao unatusonga bila kujifahamu. Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, mimi sikujiandikisha kupiga kura Zanzibar kwa kuogopa hitajio la ukaazi wa miezi 36 kabla ya uchaguzi. Hivyo mimi nilijiandikisha Dar es Salaam. Kwa bahati chaguzi za Bara na Zanzibar hazikufanyika siku moja, na kwa kuwa nilikuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Zanzibar nilisimamia upigaji kura Zanzibar. Baadaye niliweza kupiga kura Dar es Salaam. Vinginevyo, ningekosa haki yangu ya msingi ya kupiga kura. Lakini si hivyo tu, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar alihimiza wengine kujitokeza kupiga kura, na alishiriki kuandaa mipango murua ya uchaguzi, lakini yeye mwenyewe hakupiga kura Zanzibar!



Sasa kama kwetu Zanzibar ninabaguliwa na kuambiwa kuwa mimi ni Mzanzibara, niende wapi? Sisi sote wenye asili ya bara na wale wenye asili ya Arabuni, tuliojikuta tumezaliwa Zanzibar, na wale ambao ndio wenyeji asilia wa Visiwa hivi, sote tu Wazanzibari na tuna haki sawa katika undeshaji wa Serikali[15].


Pamoja na ufafanuzi uliowahi kutolewa na Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Idi Pandu Hassan, kuhusu utofauti uliopo kati ya Mtanzania na Mzanzibari[16],masimulizi ya Jaji Ramadhani yanatoa picha kwamba tunaweza kuwa na sheria kwa nia nzuri lakini matatizo yakawa kwenye utekelezaji wake. Kwa mtazamo wake, Makame Mahamud Khamis anaona sheria zinazokidhi haja zipo lakini watendaji wengi huzitafsiri na kuzitekeleza kwa kuweka mbele utashi  wao wa kisiasa zaidi[17].


Ni vyema kufahamu pia kwamba ni katika kipindi hiki (miongo miwili hii ya mwisho) ‘kero’ nyingi za muungano zimerekodiwa lakini pia jitihada kadhaa zimefanywa na Serikali ya Muungano kushughulikia kero hizo. Ni kwa kiasi gani kero za muungano zimepatiwa ufumbuzi thabiti ni suala jingine lenye mjadala mzito. Mwaka 1998 Serikali ilianzisha Sekretarieti ya Muungano kwa lengo la kuratibu na kufuatilia utekelezaji wa masuala ya muungano na yasiyo ya muungano[18]. Katika kipindi cha mwaka 2000-2010 pekee vikao vipatavyo 1000 vya ushirikiano vimefanyika kujadili masuala ya kisekta ya kubadilishana uzoefu, ujuzi, utaalamu, sera, mafunzo na ushiriki katika masuala ya kimataifa[19]. Ni kipindi ambacho pia tume na kamati nyingi ziliundwa kwa minajili ya kushughulikia kero za muungano kama baadhi ya tume na kamati hizo zilivyorodheswa kwenye jedwali la kiambatisho A. Kipindi hiki pia Serikali ya Muungano imetoa mwongozo wa namna ya kuishirikisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika masuala yote ya kimataifa.


Tathmini ya jumla ni kwamba, kwanza, kamati na tume nyingi zimeundwa. Hii ni ishara kwamba nia ya kushughulikia imekuwepo ingawa ni dhahiri vikao vya tume na kamati hizi vimewagharimu walipa kodi wa Tanzania. Ni wakati muafaka wa kuzimaliza kero zilizopo kabla ya matatizo mengine hayajajitokeza siku za usoni. Pili, inaonekana bado watanzania wanaamini katika njia ya mazungumzo katika kusuluhisha mizozo na migogoro ya kisiasa. Duru kadhaa za mazungumzo zilizopelekea muafaka wa kwanza mpaka wa tatu visiwani Zanzibar ni thibitisho kwamba meza ya mazungumzo imeendelea kuwa nyenzo muhimu ya kutuliza jazba na mihemko ya kisiasa. Lakini lazima tuzingatie angalizo kwamba si vyema kuendelea na mtindo wa kusubiri misuguano itokee ndio tutafute suluhu. Utaratibu mzuri na wa gharama ndogo ni kuzuia hali na mazingira ya misuguano kutokea.


  1. Hitimisho: Mustakabali wa Muungano

Tunapohitimisha mada hii baada ya kupitia safari ndefu ya kihistoria ya miaka hamsini, ni vyema kutafakari mustakabali wa muungano mwenyewe. Je kuna nuru kwenye njia iliyombele kwa muungano wetu kuelekea (sio miaka mitano ijayo) bali kuelekea miaka hamsini ijayo? Katika nukta hii sina budi kunuku maneno ya  Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel John Sitta, katika dibaji ya kitabu kiitwacho “Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara: Tulikotoka, Tulipo na Tunakokwenda,” anasema “Sisi raia wa Tanzania tunatamani tuendelee kuwa taifa linaloongozwa na utu, umoja, heshima, uzalendo na maendeleo ya wote bila ubaguzi wa kukusudia au kutokukusudia. Safari ya miaka hamsini (50) imeanza kutupa tahadhari kuhusu tabia mbovu za ubinafsi, uzembe na kupungua kwa utu unaoheshimu kila mmoja wetu”[20]. Angalizo la tahadhari ni suala la kuzingatia kwa kuwa viashiria vya kupungua kwa moyo wa utu, umoja na uzalendo vimejidhihirisha.

Katika tathmini yake ya hali ya muungano baada ya miaka kadha ya utekelezaji wa makubaliano ya muungano, Gaudens Mpangala, anabainisha kwamba wakati siasa na harakati za miaka ya 1950 na 1960 zililenga kumng’oa mkoloni na kuondoa matabaka kati ya wafanyakazi na wakulima wadogowadogo kwa upande mmoja, na matajiri na wamiliki wa ardhi kwa upande mwingine, kipindi hiki cha mfumo wa vyama vingi harakati zimekuwa na sura ya kisiasa zaidi, kugombea madaraka au kulinda madaraka[21]. Mtazamo huo unaungwa mkono na msomi wa sheria, Harrison Mwakyembe ambaye anaona mafanikio ya muungano yanapimwa kwa vigezo finyu vya vyeo badala ya kiwango cha utatuzi wa kero wananchi[22].


Muungano wa Tanzania umepitia mitihani na misukosuko kadhaa kufikia wakati huu ambapo mchakato wa kutengeneza katiba mpya  umeamsha hisia nzito hususan kuhusu muundo gani utumike kwa siku zijazo. Kama ilivyoonyeshwa katika mada hii, hoja kuhusu muundo wa muungano ilijitokeza kwa dhahiri miaka ya 1980 na kupelekea viongozi waandamizi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kujiuzulu. Hoja ilijitokeza tena kwenye mapendekezo ya Tume ya Nyalali ya 1991 na kufuatiwa na vuguvugu la G55 mnamo mwaka 1993, na hatimaye kwenye ripoti ya Tume Ya Jaji Kissanga ya 1999. Ni matumaini yetu sisi kama wachambuzi na pia wadau wa muungano wetu masuala yote  ya muungano yatapewa kipaumbele sawa na ufumbuzi wa kudumu wa matatizo na changamoto za muungano.


Tuungane na wale wasiopenda kuangalia uwepo au ustawi wa muungano kwa darubini finyu ya idadi ya serikali tuzitakazo. Suala la kujirudi hapa ni kwa kiasi gani tunapunguza au kuondosha siasa katika kuundesha muungano na badala yake kuuimarisha na kuutumia muungano wenyewe kutimiza matarajio na matakwa ya wadau wakuu wa muungano, yaani wananchi? Hili la pili likifanyika, litasaidia sana kuondoa dhana iliyojengeja miongoni mwa watanzania wa pande zote mbili za muungano, kwamba muungano ni wa viongozi wa kuchaguliwa na kuteuliwa badala ya wananchi wanaoona fahari kuitwa watanzania kujisikia kuumiliki muungano.


Mwisho kabisa, misukosuko kwa muungano wa aina yoyote ile ni jambo la kutarajia. Muhimu ni kutojisahau na kuipuuzia misukosuko hiyo mpaka iyumbishe misingi madhubuti ya muungano husika. Mmoja wa wapigania haki maarufu duniani, Mahatma Ghandi, aliwahi kusema hivi: Unity to be real must stand the severest strain without breaking. Tafsiri isiyo rasmi ya maneno haya ni kwamba umoja ili uwe wa kweli au halisi ni lazima ustahimili majaribu au misukosuko mikali bila kuvunjika. Je umoja wetu uliolelewa ndani ya muungano kwa kipindi cha miongo mitano (miaka hamsini) unaweza kuhimili mawimbi makali siku zijazo pasipo kupagaranyika? Jibu la swali hili laweza kuwa rahisi au gumu kutokana na mtazamo wa anayelitafutia majibu swali lenyewe.


Kiambatisho A: Tume na Kamati Zilizoundwa Kipindi cha 1994-2014





Na

Tume/Kamati

Mwaka

1

Kamati ya Shellukindo

1994

2

Kamati ya Jaji Mark Bomani

1995

3

Kamati ya Baraza la Mapinduzi kuhusu Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

1999

4

Kamati ya Rais ya Kupambana na Kasoro za Muungano ya Shamhuna

1997

5

Kamati ya Rais ya Kuchambua Ripoti ya Kisanga-Kamati ya Salum Juma

-

6

Kamati ya Rais ya Kuandaa Mapendekezo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Juu ya Kero za Muungano-Kamati ya Ramia

2000

7

Kamati ya Jaji Kisanga

1998

8

Kamati Kuhusu Masuala ya Simu- Kamati ya Kusila

-

9

Kamati ya Baraza la Mapinduzi Juu ya Sera ya Mambo ya Nje

-





Chanzo: kutoka vyanzo mbalimbali.



[1]Soma Othman, Haroub“Tanzania: The Withering Away oft he Union“, uk. 35); Bakari, Mohammed na Makulilo, Alexander, 2014, “Between Confusion and Clarity: Rethinking the Union of Tanganyika na Zanzibar after 50 Years“, African Review Vol. 40, No. 41, uk. 2-3.


[2]Mohammed Babu na Ali Muhsini walishiriki pia.


[3]Shivji, Issa G., 2008 “Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union“, OSSREA: Addis Ababa, pp. 28-31.


[4]Abdul Sheriff, 2014,“The Proposed New Constitution and the Union Question“, African Review, Vol. 41, No. 1,  p.84.


[5]Shivji, Issa G., 2008, Pan-Africanism or Pragmatism? Lessons of Tanganyika-Zanzibar Union, OSSREA: Addis Ababa, pp. 28-31.


[6]Preamble tot he Articles oft he Union.


[7] Minja, Rasul A., 2014,”Revisiting the Plight of the Union:Why Still Embracing Pragmatism and Political Expediency?”, African Review, Vol. 41, No. 1, uk. 185.


[8]Kama hapo juu, uk. 186.


[9] Tazama Shivji, 2008, uk. 246. Shivji anasema “...He go rid of the messenger“.


[10] Kamati ya Kuratibu Maoni Kuhusu Katiba (Kamati ya Jaji Kisanga), Ripoti ya Kamati, Kitabu cha Kwanza: Maoni ya Wananchi na Ushauri wa Kamati, 1999, uk. 46-47.


[11]Tazama Shivji, Issa G., 2006, Let the People Speak: Tanzania Down the Road to Neo-Liberalism, CODESRIA Book Series: Dakar, uk. 98.


[12]Amani Abeid Karume, 2011, “Hotuba ya Ufunguzi“, katika kitabu kiitwacho Zanzibar Tuitakayo: Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa, Vitabu vya Mpango wa REDET Na. 19, Dar es Salaam, uk. 1-2.


[13]Kama hapo juu.


[14]Soma Rasul Ahmed, 2007, “Pemba Kama Ngome ya Upinzani: Tafakuri Kuhusu Ustahimilivu wa Kisiasa na Kuimarika kwa Demokrasia“, Uchaguzi na Ukomavu wa Demokrasia Tanzania, Vitabu cha Programu ya REDET Na. 14, Dar es Salaam, uk. 242.


[15]Augustino S. L. Ramadhani, 2011,“Zanzibar Tuitakayo: Utamaduni, Historia na Uvumilivu wa Kisiasa,“ Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa, Vitabu vya Mpango wa REDET Na. 19, Dar es Salaam, uk. 13-14.


[16]Idi Pandu Hassan anafafanua: “Inaposemwa Mtanzania, inakusudiwa kueleza raia wa Tanzania amabaye anaweza kuwa ama anatoka Tanzania Bara au Zanzibar. Lakini anapotajwa Mzanzibari, ina maana ni lazima awe ni raia wa Tanzania mkaazi wa Zanzibar. Hapa ieleweke wazi kuwa kumtaja Mtanzania ni kutaja uraia au kwa maana nyingine utaifa; na kumtaja Mzanzibari inakusudiwa Mtanzania anayeishi Zanzibar au kwa maana ya mbali, mwenye asili na makaazi Zanzibar. Tofauti hii imeelezwa katika Sheria ya Mzanzibari Na. 5/1985... Hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Jamhuri ya Muungano na Sheria ya Zanzibar, kila Mzanzibari kwanza lazima awe Mtanzania ndipo baadaye aweze kuwa Mzanzibari. Kwa maana nyingine hakuna Mzanzibari asiyekuwa raia wa Tanzania, lakini wapo raia wa Tanzania ambao si Wanzanzibari. Hiyo ndiyo tofauti kubwa ya Mtanzania na Mzanzibari. Soma Idi Pandu Hassan, “Uzanzibari na Ukaazi, Msingi wake Kikatiba na Kisheria: Mtazamo wa Ndani“, Zanzibar Tuitakayo: Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa, Vitabu vya Mpango wa REDET Na. 19, Dar es Salaam, uk. 26.


[17]Makame Mahamud Khamis, 2011, “Uzanzibari na Ukaazi, Msingi wake Kikatiba na Kisheria: Mtazamo wa Nje“, Zanzibar Tuitakayo: Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa, Vitabu vya Mpango wa REDET Na. 19, Dar es Salaam, uk. 47-48.


[18]Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Makamu wa Rais, Taarifa ya Miaka Hamsini (50) ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Kudumisha Muungano na Hifadhi ya Mazingira, 1961-2011, Novemba 2011, uk. 30.


[19]Kama hapo juu.


[20] John M. Kasembo, chapisho la 2013, Miaka Hamsini ya Uhuru wa Tanzania Bara: Tulikotoka, Tulipo na Tunakokwenda, Limuru: Francisca Kolbe Press, uk. 16.


[21]Soma Gaudens P. Mpangala, 2011, “Tathmini ya Chaguzi katika Kipindi cha Mfumo wa Vyama Vingi Zanzibar“, Zanzibar Tuitakayo: Ujenzi wa Uvumilivu wa Kisiasa, Vitabu vya Mpango wa REDET Na. 19, Dar es Salaam, uk. 60-61 (Msisitizo wetu).


[22]Kwenye mada yake ingawa Mwakyembe alikuwa akifanya tathmini ya mapinduzi na muungano lakini maono yake ni somo tosha kwa viongozi na wadau wote wa Serikali ya Muungano. Tazama Harrison G. Mwakyembe, 2007, “Mapinduzi na Muungano,“ Muungano wa Tanzania: Mafanikio, Matatizo Yake na Jinsi ya Kuuimarisha, Vitabu vya Programu ya REDET Na. 15, Dar es Salaam, uk. 29.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>