Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Lengo ni kuharakisha kesi za kuhujumiwa watalii

$
0
0
Na Salum Vuai, MAELEZO
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar, imeshauriwa kuanzisha mahakama maalumu kwa ajili ya kushughulikia kesi zinazohusu vitendo vya kuhujumiwa  watalii na kuporwa mali zao.

Akizungumza wakati wa mkutano wa kujadili mafanikio na changamoto za sekta ya utalii hapa Zanzibar ulofanyika hoteli ya Marumaru mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Sekta ya Utalii Zanzibar (ZATI) Bobby Mackena, amesema wakati umefika wa kurekebisha baadhi ya sheria nchini.

Mackena alisema wakati umefika  kuunda mahakama hiyo kwa ajili ya kuharakisha kesi za watalii wanaohujumiwa na wahalifu.
Alifahamisha kuwa jumuiya yake imeandaa mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya kuyawasilisha serikalini, kutaka baadhi ya sheria zirekebishwe ili ziende na wakati. 

Katika mkutano huo ulioshirikisha wawakilishi wa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na vile vya sheria,  Mackena alisema baadhi ya sheria zilizopo sasa, ni kandamizi na zinawanyima fursa watalii wanaokumbwa na kadhia za kuvamiwa,  kushambuliwa na kuibiwa.

Alieleza kwamba kumekuwa na vikwazo vingi vinavyokwamisha au kuchelewesha kesi hizo, ikizingatiwa kuwa mara baada ya kuhujumiwa, mtalii hatamani tena kuendelea kuwepo nchini.


Alisema, sababu hiyo huzifanya mahakama zishindwe kuendelea na kesi hata kama mhalifu amepatikana, kwani sheria humtaka mtu aliyehujumiwa afike mahakamani kwa ajili ya kutoa ushahidi.

“Watalii huchukizwa na vitendo vinavyotishia usalama wao na mara baada ya kuhujumiwa hawapendi tena kubaki nchini na huamua kuondoka. Hili huchangia kufutwa kwa kesi zao mahakamani. Tunaomba sheria ibadilishwe,” alifafanua.

Kwa hivyo, alisema miongoni mwa mapendekezo ya ZATI ni kuiomba serikali kwa kushirikiana na Kamisheni ya Utalii kuunda mahakama maalumu itakayoshughulikia kesi hizo na kuzitolea hukumu kwa haraka zaidi ili kurejesha imani ya watalii juu ya kulindwa kwa usalama wao.

ZATI imependekeza mahakama hiyo maalumu iendeshwe kitaalamu na ikibidi kesi iweze kusikilizwa na kutolewa hukumu ndani ya saa 24 tangu kuwasilishwa hasa ikiwa na ushahidi uliokamilika.

Aidha alisema pale inapotokea mtalii aliyekumbwa na kadhia ya kuhujumiwa na kuporwa ameshaondoka nchini, serikali ifikirie uwezekano wa kuendesha kesi hizo kwa njia ya mawasiliano ya teknolojia kwa kutumia video ikimuunganisha muhusika na mahakama popote alipo duniani.

Naye Mwenyekiti wa ZATI Abdulsamad Said, alisema pamoja na mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya utalii nchini, lakini matukio ya kuhumuiwa wageni kwa silaha za moto, kudhuriwa na kuporwa, vinachangia kuwatia hofu watalii wanaokusudia kufika Zanzibar.

Alisema kutokana na maendeleo ya  teknoljia ambapo dunia yote imo viganjani, taarifa za matukio hayo zikiwemo za wageni na wenyeji kumwagiwa tindikali, zinasambaa haraka duniani na kusababisha uhaba wa watalii wanaotarajiwa.

Alisema iko haja ya kupanga mikakati madhubuti na ya uhakika itakayosaidia kupatiwa ufumbuzi wa haraka kesi hizo ili kuzuia kuporomoka kwa idadi ya watalii, na hivyo kushusha mapato ya taifa na wananchi wanotegemea sekta hiyo kujiajiri.

Hata hivyo, pamoja na changamoto nyingi ikiwemo ya ulinzi na usalama,  Mwenyekiti huyo wa zati, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais Dk. Shein, kwa kufanya kazi karibu na jumuiya yake, kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri ili kuhakikisha utalii unazidi kuimarika na kuendelea kuwa muhimili mkuu wa uchumi wa nchi.

Aidha aliishukuru serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuridhia maombi ya wanachama wa ZATI kutaka kupunguziwa kodi na ada nyengine zinazotozwa katika sekta hiyo, ambazo alisema ni kubwa kulinganisha na kupanda na kushuka kwa mapato yatokanayo na biashara ya utalii.

“Hivi karibuni tulimualika Waziri wa Fedha Mhe. Omar Yussuf Mzee katika mkutano wetu mkuu Zanzibar Beach Resort. Tunashukuru alisikia kilio chetu cha kodi na ushuru mkubwa, na ametutaka tuchague wawakilishi wetu kukaa na wataalamu wa ZRB na TRA ili kujadili namna ya kulifanyia kazi jambo hilo,” alifafanua Said.

Alisema jumuiya yake itaendelea kushirikiana na serikali pamoja na sekta nyengine binafsi, ili kuhakikisha kwa pamoja zinaweza kuvutia watali wengi zaidi na kuinua kipato cha wananchi na taifa kwa jumla.



Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>