Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
KILELE cha sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ‘nusu karne’ ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zilizofanyika uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam jana zimefana na kuwa za aina yake.
Uwanja huo ulipambwa kwa mapambo mbalimbali ikiwemo picha za viongozi, Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapnduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, bendera za Taifa, pamoja na maumbo mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na vijana wa halaiki, ambao walikuwa kivutio kikubwa kwa hadhira, huku rangi za bendera za mataifa tafauti ambayo yalihudhuria sherehe hizo zikipamba sherehe hizo.
Aidha nembo maalum ya sherehe hizo ambayo ina picha za waasisi wa Muungano, marehemu mwalimu Julius Kambarage Nyerere na marehemu mzee Abeid Amani Karume, zilienezwa uwanja mzima na kugaiwa kwa wananchi wote walioingia uwanjani, ambao pia walipewa bendera za Taifa.
Mgeni rasmi katika sherehe hizo, ambae pia ndie mwenyeji, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete aliingia uwanjani saa nne na nusu asubuhi kwa gari la wazi akiongozwa na mapikipiki ya askari trafiki waliopambwa kwa mavazi meupe, alizunguka uwanja mzima kusalimiana na wananchi ambao nao walimpongeza kwa shangwe kubwa.
Baada ya kumaliza mzunguko wa kusalimia wananchi, Rais Kikwete alipigiwa wimbo wa Taifa, pamoja na mizinga 21 salama kwa heshima yake kabla ya kukagua gwaride rasmi la vikosi vya ulinzi na usalama.
Baadae vikosi vya ulinzi na usalama vilipitia mbele ya Rais kutoa heshima kwa mwendo wa pole na baadae vikaingia vikosi vilivyopita kwa mwendo wa kasi na kuonesha ukakamavu wa kijeshi.
Pia kwa upande wa Tanzania walikuwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mohammed Gharib Bilal, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Mawaziri na watendaji wengine wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Viongozi wengine wa Zanzibar walioshiriki sherehe hizo ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, pamoja na Mawaziri na watendaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wananchi kutoka mikoa yote mitano ya Zanzibar.
Wake wa viongozi wa kitaifa wakiongozwa na mke wa Rais mama Salma Kikwete, pamoja na wake wa waasisi wa muungano mama Fatma Karume na mama Maria Nyerere nao walishiriki hafla hiyo kubwa na ya aina yake.
Onesho la mbwa wa polisi waliofunzwa kupambana na ghasia nalo lilikuwa kivutio, pamoja na ukakamavu uliooneshwa na askari wa magereza katika kukabiliana na ghasia zitapotokezea katika magereza.
Miongoni mwa vivutio vikubwa na vya kipekee ni wanajeshi wa miemvuli ambao walitua uwanjani baada ya kutoka katika ndege zilizopita uwanjani hapo ikiwa katika urefu wa futi 4500 kutoka usawa wa bahari, wakiwa na silaha pamoja na bendera ya taifa, jambo ambalo ni jipya kwa wengi wa hadhira hiyo ambao wamekuwa wakiona mambo hayo kupitia michezo ya televisheni na sinema.
Katika kuonesha mvuto wa askari hao wa miemvuli, Rais Kikwete aliwapa heshima maalum ya kupanda jukwaani na kusalimiana nao kwa kuwapa mikono.
Makomandoo nao walionesha uwezo wao wa kupambana na adui kwa kutumia mikono kama ndio silaha pekee, jambo ambalo lilifurahiwa na kuwavutia wengi, wakiwemo viongozi na wananchi.
Vifaa vya kijeshi vikiwemo vya kivita kama ndege za kivita ambazo zilipita chinichini, pamoja na vifaru, mizinga na magari mengine ya kivita navyo vilikuwa miongoni mwa vivutio vikubwa vya sherehe hizo.
Miongoni mwa wageni mashuhuri walioshiriki sherehe hizo ni Mfalme Mswati wa tatu wa Swaziland, Rais Joyce Banda wa Malawi, Rais Uhuru Kenyata wa Kenya na Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Makamu wa Rais wa Zambia, waziri wa Serikali za mitaa, Bernito De Souza. Makamu Mwenyekiti, Umoja wa Afrika, Erastus Mwencha.
Pia alikuwepo Mfalme wa Lesotho, Majest Letsie III, Waziri Mkuu wa Rwanda, Pierre Habumuremyi, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Mentho Anthonio, Waziri Mkuu wa Misri na Makamu wa Rais wa Nigeria, Mohammed Namad.
Wengine ni kutoka Oman, Dk. Rawiya Al-Busaidy waziri wa Elimu ya Juu, Waziri wa Angola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Comoro, Said Hassan, kutoka Ushelisheli, waziri Tibeto, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom, Waziri wa Mawasiliano wa Algeria, Abdelqadir Messahel, Mabalozi Maalum kutoka Ghana, Kingsley Saka Abdulkarim na kutoka Eritrea.
Makamu Mwenyekiti wa Bunge la China , Chen Chanqin nae alihudhuria kilele hicho, ikizingatiwa kuwa sherehe hizo zinakwenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya mahusiano kati ya China na Tanzania .
Viongozi wengine wa Mashirika ya kimataifa walioshiriki ni Jumuiya ya Afrika Mashariki, Benki ya Maendeleo ya Afrika, Balozi wa Ufaransa, Balozi wa Korea Kusini, Brazil Balozi wao.
Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania , walihudhuria sherehe hizo na kuiwezesha dunia nzima kukutana katika maadhimisho hayo, hali inayoashiria mahusiano mema kati ya Tanzania na dunia.
Marais wastaafu waliohudhuria sherehe hizo ni Benjamin Mkapa, Dk. Amani Abeid Karume, Mwai Kibaki wa Kenya na Dk.Sam Nujoma wa Namibia .
Wanafunzi 3547 kutoka skuli za Tanzania Bara na Zanzibar walifanya maoneso mbalimbali ya halaiki ambayo yalionesha maumbo ya tokea kuasisiwa kwa muungano huo na mafanikio yaliyopatikana ambapo hadhira ilipata burudani ya kutosha na kufurahia umahiri wa watoto hao.
Muungano wa Tanzania umeendelea kuwa wa kipekee ulimwenguni kutokana na ukweli kwamba, nchi nyingi za Afrika ziliungana lakini hazikuweza kudumu kwa muda mrefu ikiwemo, Ghana, Guinea na Mali ziliungana lakini muungano wao ulivunjika baada ya miaka michache na kila nchi kurudi kivyake, Senegambia imevunjika na kurudi Senegal na Gambia, Ethiopia na Eritrea, Somalia na Sudan. Mwengine ni ule wa Ethiopia na Eritrea ambao baadae ulivunjika na kuzusha vita baina yao na uhasama unaoendelea hadi leo.
Huko Ulaya kuna nchi kama Czchekoslovakia ambazo sasa zimeachana na kuwa Jamhuri ya Czech na Slovakia , Shirikisho la Sovieti ambalo limesambaratika likiwa na nchi nyingi, Ujerumani ambayo hata hivyo imeungana tena hivi sasa baada ya kuwa Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi, pamoja na Korea ambayo sasa ni Korea mbili ya Kusini na Kaskazini.
Uwanja wa uhuru ulishindwa kuhimili idadi ya watu waliofika kushuhudia sherehe hizo, hivyo kulazimika baadhi ya watu kuruhusiwa kuingia katika uwanja wa Taifa ulio pembeni na kuona sherehe hizo, huku nje ya viwanja kukiwekwa screen maalum kwa walikosa nafasi kuingia ndani.
Akitoa salamu za shukurani, mbali ya kupongeza vikosi, wasanii na wote waliofanikikisha sherehe hizo na wageni waliohudhuria, alisema watanzania wana kila sababu ya kusherehekea sherehe hizo huko hotuba ya Rais kwa sherehe hizo aliitoa juzi jioni, ambapo usiku wa juzi kulikuwa na mkesha wa sherehe maalum za fashifashi Mjini Zanzibar.
Hata hivyo viongozi wa Mataifa mbalimbali waliohudhuria sherehe hizo walipewa nafasi na mwenyeji wao Rais Jakaya Kikwete kutoa salamu kwa Watanzania, ambapo wote waliipongeza Tanzania na kuiombea iendelee kuwa na amani, umoja na utulivu katika muungano wao.
Aidha katika upekee wa sherehe hizo na kutoa nafasi kwa wananchi wengi zaidi kushiriki, jumla ya wananchi 4000 ikiwa 2000 kutoka Zanzibar na 2000 kutoka Bara walipita kiwanjani hapo kwa maandamano yaliyoongozwa na farasi, pamoja na watu 50 waliozaliwa tarehe 26 Aprili na baadae wapanda pikipiki na waendesha baskeli walipita katika maandamano hayo.
Viongozi na Makamanda wa Vikosi vya ulinzi na Usalama waliovalia sare maalum, pamoja na wapiganaji wao nao walitoa mvuto maalum katika sherehe hizo adhimu.
Mbali ya vikundi vya ngoma za asili kutoka Bara na Zanzibar , sherehe hizo zilipambwa kwa wimbo maalum ulioimbwa na mchanganyiko wa wasanii wa nyimbo mbalimbali kutoka Bara na Zanzibar ambao uliwavutia wengi.
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa na mafanikio mengi kwa wananchi wao pande mbili hizo kiuchumi, kijamii na kiusalama, ambapo pia umewekwa utaratibu maalum wa kutatua changamoto zinazojitokeza katika muungano huo ndio maana ukadumu hadi leo.
Katika hatua za kuuimarisha muungano huo wa Tanzania , hivi sasa inaendelea na mchakato wa kutayarisha katiba mpya ili iendane na hali halisi na mazingira ya sasa, ikiwa ni miaka 50 tokea kuasisiwa muungano huo.
Kabla ya kilele hicho maadhimisho hayo yalishuhudia kufanyika shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na makongamano, matembezi ya hisani, michezo ya kitaifa na kimataifa nchini kote, hali iliyoonesha muamko wa wananchi kushiriki maadhimisho hayo.
Ukiachia sherehe hizo kutangazwa na kuoneshwa moja kwa moja na baadhi ya vituo vya televisheni na redio hapa nchini, waandishi wa habari wa magazeti na vyombo vyengine vya kitaifa na kimataifa, nao walikuwa mstari wa mbele kuchukua habari na picha ili kuwafikishia wananchi kupitia vyombo vyao, jambo lililoonesha uzalendo na uwajibikaji wa vyombo vya habari kwa mambo ya kitaifa.
Kauli mbiu ya sherehe hizo za nusu karne ya muungano ni ‘Utanzania wetu ni Muungano wetu, Tuulinde, Tuuimarishe na kuudumisha’ ukiwa na lengo la kuuimarisha na kuudumisha zaidi muungano huo.