Na Salim Said Salim
WATANZANIA waliopo Bara na Visiwani na majirani zetu wanaofahamu lugha ya Kiswahili, wamejifunza mengi katika awamu ya kwanza ya Bunge Maalumu la Katiba liliomalizika Dodoma hivi karibuni.
Miongoni mwa mafunzo hayo ni namna ambavyo viongozi wetu wengi wa serikali na vyama vya siasa wanavyoweka mbele maslahi yao na ya taasisi zao badala ya nchi.
Jingine ni namna ambavyo baadhi ya hao tunaowaita wanasiasa walivyobobea katika matumizi ya lugha ya matusi, kashfa, kejeli na vijembe.
Yapo matamshi yaliosikika Dodoma ambayo watu wengi walikuwa hawajawahi kuyasikia katika maisha yao, au kushuhudia yakitamkwa hadharani na katika kikao kinachotarajiwa kuwa cha heshima. Ndiyo maana washiriki wa kikao hiki cha Bunge la Katiba wanaitwa waheshimiwa.
Lakini kubwa zaidi ni ustahamilivu wa hao tunaowaita waheshimiwa na hata kuvumilia kwa utulivu matusi ya nguoni na mwilini yakiporomoshwa kama inavyotiririka mvua ya masika na kusababisha mafuriko yanayotengeneza bwawa la matusi na kashfa.
Unapoitafakari hali iliyojitokeza Dodoma, jawabu unalolipata ni kuwa kikao kile kilikuwa kama darasa la kujifunza matusi au kubadilishana uzoefu wa maneno machafu na yanayonuka.
Wajumbe kadha walijikita katika kubwabwaja matusi ya nguoni na mwilini badala ya kujadili kwa mapana na marefu rasimu ya pili ya katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba (sio yake au familia yake, bali ni mawazo yaliyotokana na Watanzania).
Hata kina mama ambao kwa kawaida tulivyowafahamu kwa miaka mingi hapa nchini huwa watu wenye lugha nzuri, nao walifanya ghasia za aina yake za kuchangia kwa nguvu zao zote katika kutengeneza hili bwawa la matusi.
Hapo kwanza ilionekana walioshika bendera ni wajumbe kutoka Zanzibar, lakini hata wale kutoka Bara nao waliingia katika ghasia hizi.
Mfano ni wa Hawa Ghasia (sijui jina ndiyo lilimponza!), naye alifika hadi kumwambia mmoja wa watu wanoheshimika sana nchini kwa umri wake, urefu, elimu na madaraka aliyoyashika katika nchi hii, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, afunge mdomo wake. Sijui kama anajua maana ya matamshi haya.
Kwa wengi wetu tuliowahi kukaa na kufanya kazi kwa karibu na Jaji Warioba, tumegundua huyu ni muungwana, mtu asiyekuwa na jeuri wala kejeli, na amekuwa siku zote akiheshimu wakubwa na wadogo licha ya umri wake mkubwa, urefu wake, elimu yake na madaraka aliyoyapata katika nchi hii na nje.
Lakini ukweli lazima usemwe, nao ni kuwa Jaji Wariona ana matatizo yake. Nayo ni kuwa ni mtu mkweli na asiyependa unafiki na ndiyo maana licha ya siku zote kupendelea Tanzania kuwa na mfumo wa serikali mbili, ndiyo maana hakutaka kuchakachua wala kuchafua maoni yaliyotolewa na wananchi kwa Tume ya Katiba.
CCM nayo pia ilifanya makosa kumpa Jaji Warioba kazi ya kukusanya maoni ya wananchi katika mchakato wa katiba, kama ilivyofanya siku za nyuma kutoa kazi kama hiyo kwa Jaji Francis Nyalali, Jaji Robert Kisanga na wengine.
Kwanini kazi ya kusema uongo apewe mtu anayesema kweli?
Mafunzo mengine tuliyoyapata ni kwamba uvumilivu wa viongozi wetu ni mkubwa sana na hungojea hadi maziwa yamwagike ndipo panapofanyika ubabaishaji wa kuyazoa.
Kwa mfano, kwanini Rais Jakaya Kikwete au mwanasiasa mkongwe Ngombale Mwiru walisubiri hadi jahazi limeshazama ndio waonekane kufanya juhudi za kutaka kuliokoa badala ya kufanya hivyo lilipokuwa linakwenda mrama?
Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ambaye amekuwa akitamba kuwa mwanasiasa, mwanasheria na mwanamichezo (Simba FC) mwenye kujali viwango, naye anastahili kulaumiwa kwa kuvumilia matusi hadi yalipofika na kusababisha wajumbe wengine kutoka kwenye ukumbi wa Bunge la Katiba.
Tutake, tusitake namna ambavyo Bunge la Katiba lilivyoendelea katika awamu yake ya kwanza, limetutia aibu Watanzania. Kama hiki ni kigezo cha heshima ya muungano wetu, basi hatuna sabababu ya kujivunia muungano huu.
Hapa inafaa kujiuliza, kama waheshimiwa wetu wanaweza kukubuhu kwa matusi kama tulivyoona Dodoma, nini tutegemee kwa watu wa kawaida wa sokoni, pwani na kwengineko ambako lugha chafu ndiyo za kusalimiana na kubadilishana mawazo?
Wakati Bunge la Katiba limekwenda mapumzikoni, inafaa kwa kila mjumbe na kila Mtanzania kupima kama mwenendo tuliouona Dodoma una lengo la kutupatia katiba yenye heshima. Tokea lini matusi yakajenga kitu kinachoweza kuheshimika?
Katika mchezo kama soka, wakati wa mapumziko hutumika kwa kocha na wataalamu, kutoa ushauri wa njia nzuri zinazofaa kutumika ili kujipatia ushindi na kumaliza mchezo kwa raha na furaha.
Nasi katika suala la kusaka katiba mpya, tutumie wakati huu wa mapumziko ya Bunge kutafuta njia itakayotutoa kwenye bahari ya matusi na kwenda kwenye katiba itakayoheshimika na kuheshimiwa na kila Mtanzania.
Katika hili viongozi wa juu wa serikali na vyama vya siasa, wanapaswa kuelewa wanayo dhima ya kuwashauri wasaidizi wao na ikibidi kuwatia minyororo ili wabadilike na wakirudi Dodoma waijadili katiba kwa heshima na siyo kwa lugha chafu na inayonuka.
Kama lengo la awali la baadhi ya hawa wajumbe wa Bunge lilikuwa kuwaonyesha Watanzania kuwa ni wataalamu wa kutukana na kukashifu watu, basi wajue kazi hiyo wameshaifanya kwa ufanisi na uadilifu mkubwa.
Sasa wanatakiwa wajikite katika kuijadili rasimu ya katiba, lakini kwa kutilia maanani kile kilichokuwemo ndani ya rasimu ambacho kimetokana na mawazo ya wananchi katika mchakato wa kutoa maoni juu ya aina ya katiba ambayo Watanzania wanaitaka.
Kama wanataka kuendeleza matusi, ni vyema kwanza wakaifanya kazi iliyosababisha kuteuliwa wajumbe wa katiba na baadaye wakendeleza utaalamu wao wa matusi kwa kufungua shule au madarasa ya matusi. Labda kwa sasa waanze kutengeneza mtaala watakaotumia kufundisha hayo matusi na kuweka sifa za anayefaa kujiunga na madarasa hayo.
Lakini kwa upande mwingine Mwenyekiti Samuel Sitta na viongozi wa Serikali ya Muungano na Zanzibar waache utamaduni mbaya wa kukaa kimya pale wanaposhuhudia mashindano ya matusi.
Ni lazima wachukue hatua za haraka na sio kungojea maziwa yamemwagika na hapo tena kuyalilia.
Ni kweli wazee walituambia “akutukanaye hakuchagulii tusi”, lakini ni vyema angalau uwepo ustaarabu wa kuchagua wapi hilo tusi litolewe na kwa vyovyote vile sio pahala penye heshima kubwa kama Bunge la Katiba.
Kama baadhi yetu tumeamua kutupilia mbali, iwe katika Bahari ya Hindi au mbuga ya Serengeti, ustaarabu wa kuheshimiana tulioachiwa na wazee wetu, tusilazimishe na watu wengine nao kuutupa ustaarabu huu.
Kama Bunge la Katiba litarudia awamu ya pili kwa pande zote kushiriki – na tunaomba iwe hivyo, basi pawepo kuheshimiana na kuheshimu maoni ya wananchi na sio wachache kwa utashi wa maslahi yao binafsi au vyama vyao kutaka kuwatia wengine shemere na kuwaburuza.
Watanzania hawatarajii viongozi wao kuwaabudu, lakini wanayo matumaini na matarajio makubwa ya mawazo na maoni yao kuheshimiwa ili kujenga hatima ya nchi yao.
Tuachane na kulazimisha mambo kwa kutumia vitisho au matusi ya
nguoni na mwilini na sote kwa pamoja tuseme: “Amueni wenyewe wananchi.”
Chanzo - Tanzania Daima