Khamisuu Abdallah na Khamis Amani
Watu wawili wamekamatwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Amani Abeid Amani Karume, wakisafirisha dawa za kulevya pipi 155 zenye uzito wa 2.12kg kutoka Zanzibar kuelekea Hongkong.
Watu hao walitambulika kwa majina ya Emmy Ambukage Mwaipaje (39) na Ubwa Amani Muhamed (40) wote wakaazi wa jijini Dar es Salaam .
Vijana hao baada ya kukamatwa na dawa hizo walipandishwa katika mahakama ya mkoa Vunga kusomewa mashitaka yao yanayowakabili.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka zilizowasilishwa mahakama tofauti, Aprili 17 mwaka huu majira ya saa 10:00 za jioni washitakiwa hao walikamatwa uwanja wa ndege wa Ameid Amani Karume wakiwa na dawa za kulevya aina ya heroine.
Kosa la kusafirisha dawa za kulevya ni kinyume na kifungu 15 (1) (b) (1) sheria namba 9 kama ilivyofanyiwa marekebisho kunyume na kifungu namba 11 cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Emmy ambae alipandishwa katika kizimba cha hakimu Hamisuu Saaduni Makanjira na kusomewa shitaka lake na Mwanasheria wa Serikali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), Anuar Khamis Saaduni, ilidaiwa mwanamama huyo bila ya halali akiwa anasafiri kutoka Zanzibar katika uwanja wa ndege wa Abeid Amani Karume kwenda Hong Kong alipatikana na pipi 79 sawa kilogram 1.04 ambazo ni dawa za kulevya aina ya heroine.
Katika mahakama ya Hakimu Essaye Kayanje ambae ni Naibu Mrajis, ambako alipandishwa mshitakiwa Ubwa na kusomewa shitaka lake na Mwanasheria wa Serikali Omar Sururu, ilidaiwa alipatikana na pipi 76 swa na kg 1.08 ambazo ni dawa za kulevya aina ya heroine.
Kosa la kupatikana na dawa za kulevya ni kinyume na kifungu 15 (1) (a) sheria namba 9 ya mwaka 2009 kama ilivyofanyiwa marekebisho kinyume na kifungu namba 11 cha sheria namba 12 ya mwaka 2011 sheria za kuzuia dawa za kulevya.
Washitakiwa hao wote walikataa mashitaka yao mbele ya mahakama hizo huku waendesha mashitaka wakidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba kupangiwa tarehe nyengine kwa ajili ya kutajwa.
Mahakimu wa mahakama hizo walikubalina na maombi ya upande wa waendesha mashitaka huku Hakimu Hamisuu akiihairisha kesi ya mshitakiwa Emmy hadi Mei 7 mwaka huu huku hakimu Essaya akiihairisha kesi ya mshitakiwa Ubwa hadi Juni 8 mwaka huu na kuamuriwa washitakiwa hao kurejeshwa rumande.