Na Rose Chapewa, Mbeya
Mwanafunzin Sabrina Athuman (11) anayesoma darasa la nne skuli ya msingi Kagera jijini Mbeya, ametoweka nyumbani kwao tokea Aprili 26 mwaka huu katika mazingira ya kutatanisha.
Baba mlezi wa mtoto huyo, Jumbe Said Zungiza, akizungumza na gazeti hili alisema mtoto huyo alitoweka nyumbani kwao eneo la mama John kata ya Ilomba jijini hapa Aprili 26 mwaka huu majira ya saa 1:00 asubuhi bila kuaga.
“Kawaida huwa tunajua kuwa mtoto wetu siku za Jumamosi huwa anaenda skuli kwenye mitihani na kabla hajaenda kawaida huwa tunampa shilingi 500 ya mtihani lakini cha kushangaza siku hiyo tulishtuka kuona hayupo na kitendo cha kutoaga kilituchanganya ikabidi tuingie chumbani kwake lakini hatukufanikiwa kumuona mpaka sasa,”alisema.
Akizungumzia kuhusu mazingira ya kupotea kwa mtoto huyo, alisema mazingira aliyoondoka mtoto huyo yanazidi kuwapa wasiwasi kwani aliondoka asubuhi sana na kilichowafanya wazazi hao kushtuka ni baada ya kuamka kuona milango ya nje ipo wazi ndipo walipoanza kuita lakini hakuitika.
Kwa upande wake mama mlezi wa mtoto huyo, Riziki Jumbe, alisema Aprili 26 mwaka siku alipotoweka mtoto huyo nyumbani alikuwa amevaa suruali yenye rangi mchanganyiko ambayo ni nyekundu,kijani, bluu, pamoja hijabu nyeupe kichwani.
Aidha alisema rangi ya mtoto huyo ni maji ya kunde, mrefu mwemba na kwamba mara nyingi anapenda kutembelea maeneo ya Mswiswi kwa mjomba wake lakini huko hajaonekana.
Aliomba kwa yeyote mwenye taarifa za mtoto huyo awasiliane na baba mlezi kwa simu namba 0767810191 au 0715810191 na mama mlezi Riziki Jumbe kwa simu namba 0756684016.