Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Uonevu, udhalilishaji huu ukome Zanzibar

$
0
0
Na Salim Said Salim
 
MARA nyingi katika safu hii na katika mikutano mbalimbali nimeelezea hali ya kusikitisha ya ukiukwaji wa haki za binadamu unaofanyika sehemu mbalimbali za Zanzibar.
Siku za nyuma wengi waliohusika na vitendo hivi vya ukiukaji wa haki za binadamu walikuwa askari polisi na wale wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Hata hivyo, kwa kiasi kikubwa askari wengi wa vikosi hivi wanaonekana siku hizi kujirekebisha na kuheshimu raia.
Lakini karibu wote waliohusika na kunyanyasa na kudhalilisha watu siku za nyuma hawajaguswa, kama vile kuwawajibisha kisheria ni kutowatendea haki. Kwa maana nyingine, kupiga na kutesa watu kulihesabiwa kama shemu ya kazi zao.
Kwa bahati mbaya viongozi wanaohusika na kuhakikisha kuwa haki za raia zinalindwa, wanajifanya hawajali.
Baadhi yao wanapoelezwa hujifanya kama wametia pamba masikioni na hata kueleza kuwa hawana taarifa ya matukio hayo yanayofanyika mchana kweupe na kulalamikiwa kila pembe ya visiwa vya Zanzibar.
Katika miaka michache iliyopita na hasa wakati wa utawala wa Rais mstaafu, Salmin Amour (2000-2010), kama ilivyokuwa baada ya mapinduzi ya 1964, ilikuwa kawaida kukuta watu wamelazwa barabarani wanatandikwa mijeledi.
Udhalilishaji huu ulifanywa hasa na vijana waliojulikana kama Janjaweed waliokusanywa katika makambi kutisha watu na kutumika kupiga kura kiholela (waliowakusanya wanajijua).
Ilikuwa kawaida kwa vijana wa Janjaweed, kuingia katika nyumba za watu na kufanya vitendo vya kinyama na vilivyokosa sura ya ubinadamu.
Miongoni mwa eneo walilokuwa wakipenda kufanyia ushenzi huu ni Mtaa wa Daraja Bovu ambao watu wake wengi ni wenye asili ya Kisiwa cha Pemba.
Kwa bahati nzuri na watu walifurahi kuona baadhi ya hao wanaoitwa wakubwa na wasiostahiki kuguswa, kama aliyekuwa msaidizi wa mwanasheria mkuu na sasa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Makungu na Abeid, mtoto wa Rais mstaafu, Amani Karume, nao walipocharazwa mikong’oto barabarani.
Hapo tena wakubwa walionekana kutofurahishwa, na ushenzi huu ukasitishwa haraka.
Siku hizi askari wa Baraza la Manispaa la Mji wa Zanzibar ndio wanaoongoza kwa vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu na kutesa watu hadharani.
Hakuna anayewakemea sembuse kuwawajibisha kisheria kwa vitendo hivi vya kinyama.
Katika siku za nyuma, vijana hawa pamoja na wale wanaodaiwa kuwa wa vikosi vya ulinzi vya SMZ, walikuwa wakifunika nyuso zao (kama Ninja) na kupiga watu.
Baadhi yao walibeba mapanga, nondo na bunduki kama vile walikuwa wanasaka nguruwe mwitu.
Mwenendo huu wa ukiukaji wa haki za binadamu na unyanyasaji usiovumilika katika jamii ya watu wanaojiita wamestaarabika na wanaongozwa na utawala wa haki na sheria, niliulalamikia kwa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein katika mkutano wake na waandishi wa habri alioufanya Ikulu, Zanzibar.
Dk. Shein, aliniambia kuwa hana taarifa za watu kuvaa mavazi ya kininja na kupiga watu ovyo, kwa nilivyomuelewa kwa muda mrefu kiongozi huyu, si mtu mwenye kupenda kunyanyasa au kudhalilisha watu.
Lakini wakati mwingine nimekuwa nikitanzika juu ya kauli za shaka alizokuwa akizitoa kiongozi huyu. Kauli hizo zilinifanya nifikiri labda amebadilika.
Siku hizi, labda kwa kuamini wakubwa wanafurahia kuona watu wanapigwa na kuteswa, wanafanya ushenzi huu bila ya woga mbele ya hadhara ya watu wengi, kama katika soko kuu la mji wa Unguja, tena mchana kweupe.
Hivi karibuni sikuamini niliyoyaona Darajani, kituo cha zamani cha daladala kilichopo mbele ya soko kuu.
Hapo nilishuhudia kijana mmoja akikojolea maji yaliyotuwama na wenzake wawili walimuendesha kichura kijana mmoja katika maji hayo huku wakimpiga makofi na magongo.
Watu wengi; wanaume, wanawake na watoto walikuwa wanaangalia, lakini hawakuwa na ubavu wa kufanya lolote kwa kuhofia na wao kuadhibiwa.
Hapo nilielezwa na watu waliokuwepo hapo kuwa zoezi hilo la kuwaendesha watu kichura na kupora bidhaa za wamachinga katika soko hilo lilianza muda mrefu.
Baadhi ya askari wa manispaa walikuwa na viporo vya bidhaa walizowanyang’anya wafanyabiashara ndogo ndogo na kugawana kama mali ya kurithi.
Nilipomuomba askari polisi mmoja aliyekuwpo hapo kuingilia kati kusimamisha uhuni huo kwa vile yeye ni mmoja wa wale tuliowakabidhi jukumu la usalama wa raia na mali zao, aliniambia nilikuwa ninamtafuta ubaya, na aliondoka hapo haraka.
Pole pole nilisogea kuwaomba vijana ambao niliambiwa baadhi yao ndio wale waliokuwa katika vikundi vya Janjaweed na sasa wameajiriwa na manispaa na kumuomba mmoja wao aache ukatili ule, alinitishia kuwa angelinifanyia hivyo hivyo.
Nilipomwambia asingeweza hata siku moja kuthubutu kunidhalilisha, tulikuwa na mjadala mkali na hatimaye waliwaachia mateka wao huku wakiniteremshia matusi ya nguoni ambayo sitayasahau.
Hapo hapo tena nilimpigia simu Mkurugenzi wa Manispaa ambaye ni mtu ninayemjua kwa uungwana wake kumueleza kilichokuwa kinaendelea. Lakini jibu nililopata lilinishangaza.
Kwa kweli mwenendo wa hawa askari wa manispaa na wengine wanaoshirikiana nao unatoa sura mbaya kwa SMZ na manispaa.
Wageni wanaofika Zanzibar na kuona hali hii hawapati tafsiri yoyote nyingine isipokuwa hapana haki wala sheria Zanzibar.
Kama watu wanaokamatwa na askari wa manispaa walikuwa wametenda kosa, basi vipo vyombo vilivyopewa mamlaka ya kuwahukumu na sio kutokea watu kuwatesa na kupora mali zao.
Viongozi wa SMZ wanapaswa kuelewa kuendelea kuwalea hawa wahuni wanaowadhalilisha watu na kuwatesa ni mchezo wa hatari.
Nchi nyingi zilizofuga wahuni wa aina hii kama Haiti (Tomtom Makut) wakati wa utawala wa Dikteta Papa Doc na Ethiopia (Kabele) zama za utawala wa Dikteta Megistu Haile Mariam sasa wanasikitikia kuruhusu wahuni wale kufanya maovu kwani mwendo ule umekuwa tabu hadi leo kuudhibiti.
 
Watu waliohusika na kuwashajiisha vijana wale wa Haiti na Ethiopia kufanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu leo wanawajibishwa kisheria, baadhi yao wakiwa vikongwe vinavyotumia mkongojo.
Kwa wale ambao sasa wanawaachia hawa wanaofanya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu Zanzibar, wasije kuhisi wanaonewa wakija kuwajibishwa kama wanavyofanyiwa sasa wenzao wa Haiti na Ethiopia.
Dunia ndiyo haibadiliki, lakini mambo yake yanabadilika na miongoni mwa mabadiliko tunayoyaona kila siku ni kwa watu kutoka kwenye utawala wa mabavu na kuelekea kwenye utawala wa kidemokrasia, haki na sheria. Tujifunze haraka kwa yanayotokea nchi nyingine.
Kwa bahati nzuri jamii ya Zanzibar ni ya watu wapole, lakini upole wa watu usionekane kama kipimo cha udhaifu.
Sheria za nchi na manispaa zinapaswa kusimamiwa, lakini kwa heshima na adabu na sio kutesa watu.
Tusingoje kwa wakubwa wengine au watoto wao kuteswa ndiyo tukaona mwendo huu ni mbaya, haufai kuvumiliwa na ndipo tuchukue hatua za kuukomesha.
Kila mtu, awe raia awe mgeni, anayo haki ya utu wake kuheshimiwa na haki yake kupewa. Wazee wetu wametuusia kwamba “mnyonge mnyongeni, lakini haki yake mpeni.”
 
Miongoni mwa haki za mnyonge ni heshima yake kama binadamu na utu wake, hata kama amevunja sheria ya nchi.
#
Sio vizuri na ni hatari kama nilivyoeleza kabla kufumbia macho ukiukaji huu wa haki za binadamu unaofanywa na askari wa manispaa, huku tukijigamba kuwa tunatandika mazingira ya utawala wa kidemokrasia, haki na sheria.
Kama hatuwezi kuwapa raia haki zao, basi tuhakikishe hatuwanyanyasi na kuwadhalilisha
 
Chanzo - Tanzania Daima

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>