Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,Dkt.Ali Mohamed Shein(katikati) akizungumza na Uongozi wa Idara Maalum za SMZ katika mkutano wa utekelezaji mpango kazi wa robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja leo asubuhi
Baadhi ya makamanda wa Idara maalum za SMZ wakimsikiliza Waziri wa Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ,Mhe,Haji Omar Kheri (hayupo pichani) alipokuwa akiwasilisha taarifa ya utekelezaji mpango kazi wa robo tatu ya mwaka Julai-Machi 2013/2014,mbele ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe,Dkt.Ali Mohamed Shein,katika ukumbi wa mikutano Ikulu Mjini Unguja leo asubuhi.[Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]
STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 07 Mei , 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuongeza kasi ya utekelezaji wa majukumu yao ili huduma kwa wananchi ziweze kupatikana kwa mujibu wa malengo yaliyowekwa.
Rais wa Zanzibar alisema hayo wakati alipokuwa akihitimisha mjadala wa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpangokazi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ katika kikao kilichofanyika jana Ikulu.
Alisema wakuu wa Mikoa na Wilaya ndio wenye dhamana katika Mikoa na Wilaya hivyo wanawajibika kwa matokeo yeyote ya utendaji kazi katika Mikoa na Wilaya zao.
“simamieni shughuli zenu kwa kuwasimamia watumishi walio chini yenu na ni lazima kufanya hivyo ili wasifike wakati wakajiona kuwa wao ni watu wasioguswa na wasiohojiwa”aliewaleza viongozi hao na kuongeza kwa kusisitiza kuwa “’performance’ ya Mkoa ni Mkuu wa Mkoa na hivyo hivyo kwa Wilaya ni Mkuu wa Wilaya”
Dk. Shein alisisitiza kuwa Ofisi hiyo ni Ofisi muhimu yenye majukumu makubwa yanayogusa maisha ya kila siku ya wananchi hivyo kuimarisha utendaji na uwajibikaji katika ngazi za mikoa na wilaya ni suala la kipaumbele ili kukidhi matarajio ya wananchi kwa Serikali yao.
Katika mnasaba huo aliwataka wakuu wa Mikoa na Wilaya kufuatlitia kwa karibu kila kitu kinachofanyika katika Ofisi zao na mikoa na wilaya wanazoziongoza na kujiweka tayari wakati wote kujibu hoja za wananchi.
Dk. Shein alieleza kuwa ingawa Ofisi hiyo inafanya vizuri lakini aliwakumbusha watumishi wake wajibu na dhima kubwa waliyonayo ya kuwatumikia wananchi ambao ndio waliyoiweka madarakani Serikali.
“lazima tujitahidi kuongeza bidii katika kazi kwa kuwa hii ni Serikali ya wananchi iliyochaguliwa kwa faida ya wananchi sisi tunatekeleza tu matakwa ya demokrasia”Dk. Shein aliwasisitizia viongozi na watendaji wa Ofisi hiyo.
Katika kikoa hicho Mhe Rais alihimiza uwajibikaji katika kusimamia utekelezaji wa Sheria mbalimbali zikiwemo sheria ndogo ndogo za Mabaraza ya Miji Halmashauri.
Alisema kushindwa kwa vyombo na taasisi husika kusimamia sheria ni dosari kubwa ambayo inazorotosha utendaji wa shughuli za serikali hivyo kuanzia sasa hapana budi kwa kila mhusika kufanya juhudi za makusudi kusimamia utekelezaji wa sheria zinazomhusu.
Hata hivyo alitaka tahadhari ichukuliwe wakati wa kutekeleza sheria hizo kuepuka malalamiko ya wananchi kunyanyaswa au kubugudhiwa pasi na sababu za msingi na kuhimiza taasisi na vyombo vinavyosimamia sheria nchini kutoa elimu zaidi kwa jamii kuhusu sheria hizo.
Kuhusu suala la soko la Mwanakwerekwe Dk. Shein alieleza kutoridhika kwake na ucheleweshwaji wa utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu soko hilo na kumtaka waziri kuhakikisha kuwa maagizo hayo yanatekelezwa ndani ya wiki mbili bila kuchelewa.
Mapema akitoa maelezo ya awali Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Haji Omar Heri alieleza kuwa katika kipindi cha Oktoba 2013 ilipoundwa Wizara hiyo hadi mwezi Machi 2014 Ofisi imeweza kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio.
Aliyataja baadhi ya majukumu ya Ofisi yake kuwa ni pamoja na kusimamia Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali za Ofisi, Kubuni kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na Kufanya usajili na kuwapatia vitambulisho Wazanzibari wakaazi.
Kwa upande wa majukumu ambayo Ofisi yake tayari imeweza kuyatekeleza waziri alieleza kuwa ni pamoja na kuandaa mapendekezo ya muundo wa majukumu ya Ofisi, kukamilisha marekebisho ya rasimu ya Sera ya Serikali za Mitaa ikiwa ni pamoja na kuchapisha Sera hiyo katika lugha ya kiswahili na kiingereza.
Kwa upande upande wake Katibu Mkuu Baraza la Mapinduzi ambaye pia ni Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee alirejea wito wake kwa Wizara na Idara za Serikali kuzingatia uwiano wa shughuli zao katika Ofisi za Unguja na Pemba.
Dk. Abdulhamid alizikumbusha pia Halmashauri nchini juu ya umuhimu wa kuzingatia sheria za matumizi ya fedha za Serikali kwa kuepuka kuidhimisha matumizi nje ya bajeti kwa kisingizo tu kuwa zimevuka malengo ya ukusanyaji mapato.
Alibainisha kuwa endapo kutakuwa na haja ya kuongeza matumizi taratibu hazina budi kufuatwa kwa mapendekezo kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa kupewa idhini.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822