Na Matrida Mwenzegule
Wakati Waziri wa Nishati na Madini, Sospeter Muhongo, akitanganza kiama kwa wazee na wasio na elimu za kutosha wizarani kwake, Waziri wa Nchi,Ofisi ya Waziri Mkuu na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, ametangaza kifo cha walarushwa kupunguza kero wizarani kwake.
Katika hotuba yake kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo mjini hapa, Ghasia alimwagiza katibu Mkuu wa wilala hiyo, Jumanne Sagini, kuanza mchakato wa kuwatambua watumishi wote wanaotuhumiwa kwa rushwa na kuhujumu mamlaka za serikali kwa masilahi binafsi.
Katika baraza hilo lililokutana kwa lengo la kuboresha utendaji na uwajibikaji, Ghasia pia aliwataka wafanyakazi kuacha kulalamika badala ya kuwajibika.
Alisema wizara imegeuka jaa la malalamiko dhidi ya wizara zikiwemo kero mbalimbali za rushwa, watumishi wabovu kubebwa bila tija, uwajibikaji mbovu hasa katika kuwatendea haki watumishi jambo linalochangia kurudisha nyuma maendeleo.
Aliwataka wafanyakazi wa wizara hiyo kutumia mabaraza ya wafanyakazi kujadili mambo mbalimbali yanayohusu masilahi na ustawi wa wafanyakazi na kuishauri manejimenti ya utumishi ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Alilitaka baraza hilo pia kujadili namna rasilimali zinavyotumika vibaya kwa maslahi ya wachache.
Alisema wakitumia mabaraza hayo vizuri malalamiko ya wafanyakazi katika wizara hiyo yatapungua na kuongeza uwajibikaji wa kazi katika wizara hiyo.