Sehemu ya mbele ya Nyumba ya Bwana Salim Ahmed Salim iliyoporomoka Mtaa wa Vuga mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja.Hata hivyo hakuna mtu aliyejeruhiwa kutokana na athari hiyo.
Athari ya nyumba iliyobomoka hapo Mtaa wa Vuga ilisababisha usumbufu wa watumiaji wa Bara bara itokayo Vuga kuelekea Shangani au Serena na kulazimika kufungwa kwa bara bara hiyo.
Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar , Jeshi la Polisi pamoja na Mamlaka ya Usafiri zimekumbushwa kuendelea kuzuia uingiaji wa gari kubwa zenye uzito wa zaidi ya Tani Mbili katika eneo la Mji Mkongwe ili kunusuru majengo yaliyono ndani ya mamlaka hiyo.
Kumbusho hilo limetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipofanya ziara fupi kukagua athari ya nyumba iliyoporomoka ukuta na Dari yake juzi usiku iliyopo Mkabala na Skuli ya Sekondari ya Tumekuja Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema ukaidi wa baadhi ya madereva wa gari kubwa kupitisha Gari gari zao katika eneo hilo umesababisha uchafuzi wa mandhari na haiba ya Mji mkongwe wa Zanzibar ambao hivi sasa uko katika urithi wa Kimataifa.
“ Jeshi la Polisi wakati huu litahitajika kuwa na kazi ya ziada katika kuhakikisha agizo lililotolewa na Mamlaka ya Mji Mkongwe wa Zanzibar linatekelezwa ipasavyo “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akimpa pole Mmiliki wa Nyumba hiyo Bwana Salim Ahmed Salim kwa hasara aliyoipata alimtaka kuwasiliana na Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Mji Mkongwe wa Zanzibar katika juhudi zaujenzi wa nyumba hiyo utakaozingatia mpango halisi wa uhifadhi wa Mji huo.