Na Mwandishi wetu
Serekali imeelezea kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Balozi wa Malawi nchini, Flossie Gomile Chidyaonga,kilichotokea mwishoni mwa wiki iliyopita.
Balozi Chidyaonga alifariki akiwa njiani kupelekwa hospitali ya Aga Khan ya hapa Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, imesema Balozi Chidyaonga aliitumikia serikali ya Malawi katika nyadhifa mbalimbali.
Imesema kati ya mwaka 2006 hadi 2010 alikuwa Naibu Balozi wa Malawi nchini Uingereza na baadaye Kaimu Balozi hadi alipoteuliwa kuwa Balozi wa Malawi nchini Tanzanaia.
Taarifa hiyo imesema siku ya Jumatatu, alishinda vizuri na kufanya shughuli zake kama kawaida.
Hata hivyo, ilipofika usiku, alijisikia vibaya na kupelekwa hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam ambapo alipatiwa matibabu na kuwekwa mapunziko kuanzia saa 6 usiku hadi saa 12 asubuhi aliporuhusiwa na kupewa dawa za kutumia nyumbani.
Balozi Chidyaonga aliendelea kutumia dawa hizo na hali kuonekana kuimarika hadi siku ya Ijumaa ambapo aliamka vizuri hadi ilipofika majira ya saa 6 mchana, hali yake ilipobadilika na kukimbizwa tena hospitali ya Aga Khan ambapo alipokelewa daktari alisema amekwishafariki.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili na uchunguzi wa madaktari umeonesha marehemu amefariki kutokana na mshipa mkuu wa aorta kuvimba na kupasuka kulikosababisha damu kukusanyika kwenye mfuko wa moyo na hivyo kufanya moyo ushindwe kufanya kazi yake.
Leo mwili wa marehemu utachukuliwa kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kupelekwa ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere ambapo kutafanyika misa ya kumuombea marehemu na kutoa heshima za mwisho kuanzia saa 4:00 asubuhi.
Mwili wa Marehemu unatarajiwa kusafirishwa kwenda Blantyre, Malawi kesho na mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Jumatano.
Katika kipindi chote alichokuwa mwakilishi wa Malawi nchini, Balozi Chidyaonga alifanya kazi yake ya kukuza na kuendeleza ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kwa umahiri wa hali ya juu.