Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

JK akagua kiwanda kikubwa cha saruji duniani

$
0
0
Na Mwandishi wetu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametembelea kiwanda kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote duniani cha Dangote Cement Obajana Plant kinachomilikiwa na tajiri mkubwa zaidi wa Afrika, Aliko Dangote, ambaye pia anajenga kiwanda kikubwa cha saruji mjini Mtwara.

Akiandamana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda, kwa siku nzima, Rais Kikwete alitembelea kiwanda hicho kilichoko katika eneo la Obajana, jimbo la Kogi, kilomita 400 kaskazini mashariki mwa mji maarufu wa kibiashara wa Nigeria, Lagos.

Rais Kikwete ambaye alikuwa nchini Nigeria kuhudhuria kongamano ya uchumi Duniani-Afrika (WEFA) mwaka huu, aliamua kutumia siku yake ya mwisho ya ziara yake ya siku tatu nchini humo, kwa kutembelea uwekezaji mkubwa wa mwekezaji ambaye ameanza ujenzi wa kiwanda cha saruji cha Mtwara ambacho kitakuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji kuliko kingine chochote katika Tanzania, kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani za kimetriki milioni tatu kwa mwaka.

Rais Kikwete ambaye alipokewa kwenye uwanja wa ndege wa kiwanda hicho na Dangote mwenyewe, na kuanza ziara yake kwa kutembelea machimbo ya kiwanda hicho ambayo yako kilomita tisa kutoka kiwandani ambako malighafi ya kiwanda hicho husafirishwa kwa madaraja na mikada maalum hadi kiwandani.

Alimwambia Rais Kikwete kuwa kwa sasa kiwanda cha Obajana kinazalisha tani za kimetriki milioni 10.25 kwa sasa kwa mwaka na hivyo kukifanya kiwanda hicho kuwa kiwanda kikubwa zaidi cha saruji duniani kilichoko katika eneo moja na kuwa baada ya upanuzi unaoendelea kufanywa kwenye kiwanda hicho, uwezo wake wa uzalishaji utaongezeka na kufikia tani za kimetriki 13.0 kwa mwaka ifikapo mwakani 2015.

Dangote alimwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilicho kwenye eneo la kilomita za mraba saba kitakuwa kimegharimu kiasi cha dola za Marekani bilioni 2.5 wakati upanuzi wake utakapokamilika.


Kwa sasa kiwanda hicho kina biashara ya dola za Marekani bilioni mbili kwa mwaka.

Bilionea huyo alimwambia Rais Kikwete kuwa kiwanda hicho kilichoanza kujengwa mwaka 2003 na kukamilishwa 2006 na hatimaye kuzinduliwa na Rais Olusegun Obasanjo Mei 12, mwaka 2007, wiki mbili kabla ya kustaafu urais wa Nigeria, kinaajiri watu 800 kwa wakati mmoja na hivyo kuwa miongoni mwa waajiri wakubwa zaidi katika Nigeria.

“Mheshimiwa Rais, ili kuelewa vizuri mchango wa kiuchumi na kijamii za kiwanda hiki na viwanda vyetu vingine katika maeneo mengine ya Nigeria, unahitaji kukumbuka kuwa kabla ya kuanza kujenga kiwanda hiki, Nigeria nzima ilikuwa na uwezo za kuzalisha tani za kimetriki za saruji milioni 1.5 tu, wakati huo chini ya miaka 10 iliyopita,” alisema.

"Tunataka kufikia hatua ya kuhakikisha kuwa eneo la Afrika Magharibi na hata bara letu la Afrika linaacha kabisa kuagiza saruji nje ya bara letu na  tutafikia huko,” alisema.
Mbali na kiwanda cha Obajana, kampuni ya saruji ya Dangote inazalisha saruji katika maeneo mengine mawili ya Nigeriaambalo uzalishaji wa jumla wa maeneo hayo matatu ni tani za metriki 20.25 kwa mwaka.

Alipoulizwa na Rais Kikwete kama wanategemea kwa namna yoyote umeme wa taifa, Dangote alijibu kwa furaha, 

“hatujaunganishwa kwenye gridi ya taifa na tunadhani hili ni jambo zuri kwa sababu hatua tulizochukua zinatuhakikishia umeme wakati wote na kwa kiwango ambacho tunakihitaji. Tunatumia gesi ama diseli yetu wenyewe. Na wala siyo umeme tu, hata miundombinu ya eneo hilo kiliwemo daraja hili kubwa linalounganisha eneo la machimbo na kiwanda, tumejenga sisi,” alisema.

Alisema mbali na kujenga miundombinu ya umeme wake, kiwanda hicho pia kimejenga bwawa lakelenyewekwa ajili ya huduma ya maji kusaidia uzalishaji wa saruji bila kutegemea huduma ya maji ya serikali.

Aidha, bwawa hilolinatoa huduma ya maji kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho.

Mbali na shughuli za kiwanda, kampuni ya Dangote inashiriki kwa karibu shughuli za jamii inayozunguka kiwanda ambacho kwa sasa imeanzishwa miji midogo saba katika eneo lililokuwa pori lenye nyumba 50 za wenyeji tu kabla ya shughuli za kiwanda hicho kuanzishwa.

Alimwambia Rais Kikwete kuwa kampuni yake inatoa misaada katika sekta za elimu, maji na umeme kwa wananchi ambao wanazunguka kiwanda ambacho tokea kuanzishwa kwake kimevutia mabenki 13 ambayo yameanzishwa matawi yake katika eneo la kiwanda.

Alisema mbali na kutoa huduma nyingine za kijamii, kampuni ya saruji ya Dangote inajenga taasisi kubwa ya elimu ya DangoteAcademy ambayo itatoa elimu na mafunzo ya kiufundi kwa ajili ya kuandaa wafanyakazi wa kiwanda hicho na watoto wa jamii inayozunguka kiwanda hicho.

Alisema kampuni yake inafanya jitihada kubwa kuhakikisha Rais Kikwete anakifungua kiwanda cha saruji cha Mtwara kabla ya kustaafu mwishoni mwa mwaka ujao.

Mbali na Nigeria na Tanzania, Dangote ana viwanda ama anajenga viwanda vya saruji na shughuli za saruji katika nchi 14 za Afrika ikiwamo Ethiopia, Zambia, Msumbiji, Kenya, Senegal na Sierra Leone, Afrika Kusini, Congo (Brazzaville), Cameroun, Ghana, Liberia na Ivory Coast.

Aidha Dangote ambaye anakubaliwa kuwa tajiri mkubwa zaidi katika Afrika kwa thamani ya dola za Marekani bilioni 25 yeye na kampuni yake ya Dangote Group pia ina shughuli za uzalishaji wa sukari, uzalishaji wa chumvi, utengenezaji wa magunia, uzalishaji maji, uzalishaji wa vyakula vya aina mbali mbali, uzalishaji wa mafuta ya kupikia na utengenezaji wa nyanya.


Kwa sasa anaendelea na ujenzi wa kiwanda cha mbolea na kile cha kuzalisha bidhaa za petrol na kemikali.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>