Na Mwandishi wetu
ZANZIBAR bado inakabiliwa na tatizo la kuporomoka kwa maadili pamoja na utoro uliokithiri shuleni.
Jambo hilo linawapa changamoto jamii na serikali kutafuta njia ya kulitatua.
Huku ikiangaliwa kwa mtazamo tofauti juu ya nani mwenye jukumu la kurekebisha hali hiyo ambayo matokeo yake ni kukosa nguvu kazi imara ya baadae, jamii imekuwa ikiitupia lawama serikali kutokana kumong’onyoka kwa maadili pamoja na utoro shuleni.
Hata hivyo viongozi hao wa serikali wamekuwa wakijitetea kwa kusema jukumu la kujenga vijana ili wawe raia wame inaazia kwa wazazi wenyewe.
Katika makala hii naangazia nafasi ya wazazi na walezi katika kuzuia utoro shuleni ili wanafunzi waweze kupata elimu ambayo ni msingi wa kila mtu.
“Mshike mshike na mwenyewe nyuma,” ni msemo maarufu ambao hukumbusha kila mzazi kuchukua jukumu kulea mtoto wake katika misingi iliobora.
Lakini kwa bahati mbaya msemo huu inaonekana kutozingatiwa katika maana iliyokusudiwa hasa katika wakati huu wa sayansi na teknolojia.
Tatizo la utoro katika shule za Zanzibar limeonekana kama jambo la kawaida na sasa linakwenda sambamba na ajira za utotoni ambapo watoto wengi huacha au kutoroka shule na kujiingiza katika shughuli za kujipatia mapato.
Hivi karibuni kumekuwepo juhudi za kuwarejesha watoto shuleni ambao walitoroka au kukimbia pamoja na wale waliomo katika hali ngumu juhudi inayofanywa na Serikali ya Zanzibar (SMZ) kwa msaada wa Jumuiya ya Ulaya (EU).
Tangu mradi huo wa miaka mitatu uanze mwaka 2011 kumekuwepo mafanikio makubwa ambapo watoto 3000 wamerudishwa shule kupitia madarasa tofauti kutoka katika ajira ngumu walizokuwa wanafanyishwa.
Mradi huo unaotekelezwa kwa pamoja kati ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na wanaharakati wengine ambao ni KOKHAWA, PIRO na COWPZ.
Wanaharakati hao waliwatambua watoto wanaotoroka shule au wapo katika ajira kwa kushirikiana na Viongozi wa Vijiji (Masheha), ambapo mtoto hupewa elimu nasaha juu ya umuhimu wa kupata elimu na baadae kupatiwa vifaa vyote vya shule.
Mradi huo unaogharimu zaidi ya EURO 1,000,000, umejumuisha na kuzisaidia mitaji zile familia zenye umasikini mkubwa kwa lengo la kuwaendeleza watoto.
Hata hivyo licha ya juhudi zote hizo kufanyika, imeonekana baadhi ya wazazi na walezi wanakwamisha kupatikana kwa ufanisi wa hali ya juu kwa mradi huo, kutokana kwamba hawafuatilii maendeleo ya watoto wao shuleni.
Uchunguzi uliofanywa na Tanzania Daima umebaini kwamba baadhi ya wazazi hawajali maendeleo ya watoto wao, jambo ambalo huvunja moyo wafadhili.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Uzini Mkoa wa Kusini Unguja, Silima Haji Simai anasema kulikuwepo na utoro mkubwa kwa baadhi ya wanafunzi katika shule yake lakini baada kuja kwa mradi huo sasa hali inaonekana kwenda vizuri.
Anasema watoto zaidi ya 17 walikuwa wamekimbia kabisa shule, lakini baada ya juhudi zilizofanywa na TAMWA kupitia mradi wa kuwarejesha shuleni watoto waliotoroka kwa shirikiana na wazazi wa watoto hao, wote walirudi kuendelea na masomo.
Anawataja umri wa watoto hao kwamba ni miaka 12 hadi 15 ambao awali walipowafuatilia wazazi wao na kubaini kwamba wameshindwa kuwalazimisha kwenda shule.
“Mtoto ukimpa vifaa na sare za shule ataweza kurudi shule lakini kama humfuatilii, basi anaweza kuacha njiani,” anasema Mwalimu Mkuu huyo.
Anafahamisha kwamba jamii imekuwa haishughuliki na hakuna ambaye anakwenda shule kuangalia maendeleo ya watoto wao.
“Hichi ndio chanzo cha utoro, mtoto ni mtoto anataka kuangaliwa kwa karibu wakati wote, lakini kama hafuatiliwi anaweza kuacha shule bila ya wazee wake kujua,” anasema Mwalimu Simai.
Anasema ni vema wazazi na walezi wafahamishwe juu ya umuhimu wa kufuatilia maendeleo ya watoto wao ili watoto na walimu wahisi kama juhudi za kuendeleza zipo.
Mratibu wa TAMWA kupitia mradi huo Sheikha, Haji Dau anasema wazazi kutofuatilia watoto wao ni miongoni mwa changamoto ambazo hukumbana nazo wakati wa kutekeleza mradi huo.
“Kiukweli watoto wengi wamerudi shule lakini suala la wazazi na walezi kutowafuatilia maendeleo ya watoto wao wakiwa shule, wanaweza kurudisha nyuma malengo yaliokusudiwa,”anasema Dau.
Katika mkoa huo wa Kusini, zaidi ya watoto 552 kati ya familia 1500 wamerudi shule na wamewapatia, mabuku, mikoba, na vifaa vyengine vya shule ikiwemo unifom.
Asha Hasham Maderewa mama wa mtoto ambaye awali aliacha shule kabisa na kujiingiza katika ajira za utotoni, anasema tangu mwanawe arudi shule amekuwa na utaratibu mzuri wa kumfuatilia maendeleo ya mtoto shuleni.
“Ninawaomba wazee wenzangu sasa tuanze juhudi ya kufuatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni ili kuwalinda na utoro wa mara kwa mara,” anasema Asha.
Anasema kama mtoto hujamfualia akiwa shuleni, anaweza akatoroka akaenda kujishuhulisha na mambo mengine bila wao kujua kitu ambacho mwisho wake ni kutoroka kabisa.
Hassan Ussi Vuai anasema wazazi wa kiume hawana utaratibu wa kuwafuatilia watoto wao na kuona jukumu hilo ni la mama tu.
“Sisi wanaume bwana tunaona kama wenye jukumu la kulea na kuangalia maendeleo ya watoto ni wanawake, jambo ambalo ni ridasha nyuma juhudi za kuondoa utoro shule,” anasema Vuai.
Mratibu wa Wanawake na Watoto katika Wazara ya Kazi Maendeleo ya Vijana Zanzibar, Mashavu Ramadhan Abdallah anawataka wananchi washikamane waondoe changamoto hiyo.
“Kama tutashirikiana basi tutahakisha watoto wote Zanzibar wataweza kupata elimu na kuondokana na utoro kutokana ufuatiliaji wa mienendo yao,” anasema Mashavu.
Hayo yote yanatia mkazo huo msemo ambao ulitumika hapo awali kwamba licha ya misaada inayopatikana kutoka kwa wafadhili, kuwepo na juhudi za kuondoa utoro shuleni.
Kama wazazi wataweza kuangalia watoto wao kwa umakini wanapokuwa shuleni basi hakika suala la utoro linaweza likawa historia katika Visiwa vya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Dunia hii ya Sayansi na Teknolojia kama watoto hawafuatiliwi maendeleo yao shuleni, wanaweza wakaenda katika maeneo ya starehe.
Kutokana na kilio ambacho watu wengi wamekieleza kwamba misaada inapatikana lakini ni vema wazazi waakaaza kufuatilia maaendeleo ya watoto wao shuleni.
Chanzo - Tanzania Daima