Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Msiwaite Majina Mabaya Wazee.

$
0
0
Na Khamis Amani
VIJANA nchini wameombwa kuwaenzi wazee katika harakati zao mbali mbali ili waweze kufanikiwa katika maisha yao, na sio kuwatenga na kuwapachika sifa mbaya za uchawi.

Wito huo umetolewa na Diwani wa Wadi ya Kwahani, Machano Mwadini Omar, katika ziara ya kuwatembelea wazee wanaoishi ndani ya wadi hiyo.

Alisema, wazee ni rasilimali muhimu katika harakati mbali mbali za kimaisha ikiwemo maendeleo, hivyo wanapaswa kuthaminiwa kutokana na mchango wao mkubwa wanaoutoa.

"Bila ya wazee familia ama jamii haiwezi kufanikiwa, kwani wazee ni rasilimali muhimu sana inayopaswa kuthaminiwa na ndio nguzo muhimu katika maisha yetu ya kila siku," alisema Diwani huyo.

"Wazee ni watu wenye hekima ni nguzo muhimu ya kuthaminiwa kwani bila ya msaada wa wazee maisha yanaweza kukuendea kombo," aliongeza.

Alisema, mambo mengi yanayofanywa na vijana pekee huwa hayana umaliziaji nzuri lakini msaada wa wazee katika mambo yao ndio yanayopelekea kufanikiwa, kutokana na hikima walizonazo ambazo ni adimu kupatikana kwa vijana.

Hivyo alifahamisha kuwa, kufanikiwa kwa maisha ya mtu mmoja mmoja ama jamii ni kuwathamini wazee pamoja na kupokea msaada wanaoutoa.

Alikemea tabia iliyojengeka hivi sasa ya kuwatuhumu wazee uchawi, hali ambayo inaweza kusababisha chuki na uvunjifu wa amani miongoni mwa jamii.

"Wazee hawa ndio waliotuzaa, kutulea na hadi kufikia hapo tulipofikia iweje leo tuwatuhumu uchawi tukiwa wakubwa na akili zetu tusiwatuhumu wakati ule wa udogo tulipokuwa tukiwatumainia kwa kila kitu, hilo ni jambo baya turudini kwa Mwenyezi Mungu," alitanabahisha.

Alisema ujana usiwe ni chanzo cha kuwachukia wazee ambao nao walipitia njia hiyo na kila mtu ikifika wakati wake utamfikia na kuomba kuishi na wazee kwa salama na amani.

Nao wazee wa wadi hiyo,walimshukuru Diwani huyo kwa kuwatembelea na kuwafariji hasa katika kipindi hichi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Walisema, kiongozi mzuri ni yule anayejali maisha ya anaowaongoza kwa kupita kuwajuulia hali hata kama asitoe kitu chochote kwani utu ni bora kuliko kitu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>