Na Joseph Ngilisho, Arusha
MKUU wa Mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo ameagiza watendaji na madiwani wa halmashauri ya jiji la Arusha kuwasaka na kuwakamata wazazi wote,waliowatelekeza watoto wao na kuwafanya waishi maisha ya mtaani, na wengine kulelewa kwenye vituo vya watoto yatima.
Mulongo aliyasema hayo jana wakati akipokea msaada wa watoto yatima kutoka kwa Mwakilishi wa ubalozi wa Falme za Kiarabu (UAE),ambapo
vitu mbalimbali zikiwemo nguo ,viatu na sketi zilikabidhiwa ikiwa ni sehemu ya kulitambua kundi hilo katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Alibainisha kuwa hivi sasa idadi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu imeongezeka na kufikia 7,200 hali aliyoielezea kwamba inatokana na mifarakano ya familia na kuwalazimu watoto hao kuzikimbia familia zao.
Aidha alisema watu wamekuwa wataalamu wa kuzaa na kusahau majukumu ya kulea,hivyo kuwataka watendaji na madiwani kuwasaka wazazi ambao wamewatekeleza watoto wao na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria ili wachukuliwe hatua zaidi.
Aidha alisema atawachukulia hatua kali baadhi ya wamiliki wa vituo hivyo watoto yatima ambao wengi wao wamekuwa wakivitumia kwa kujinufaisha kutokana na misaada mbalimbali ya wahisani.
Aliwataka wahisani pamoja na watu mbalimbali nchini kuhakikisha wanawasaidia watoto wenye mahitaji wa elimu, malazi na mavazi hali ambayo itasaidia kupunguza wimbi la ongezeko la watoto wasio na wazazi.
Naye mwakilishi wa Falme za Kiarabu, Bader Nahdi alisema watoto yatima wanapaswa kuangaliwa na kupewa misaada kwani wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa elimu.
Aidha alisema wao kama wawakilishi wa balozi ya kiarabu wametambua kuwa watoto hao wana changamoto nyingi ambapo alisema wengi wao wanatoka sehemu mbalimbali nchini Tanzania na ni kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ugomvi kati ya wazazi na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wa mstahiki meya wa jiji la Arusha, Gaudience Lyimo alisema yeye pamoja na ofisi yake watahakikisha wanafuatilia kwa ukaribu kuhusu suala la watoto hao na kuwapatia misaada kwani watoto hao ni sawa na wengine.