Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

JK. Uhusiano Wetu na Rwanda Unapitia Kipindi Kigumu.

$
0
0
Na Mwandishi wetu
RAIS Jakaya Kikwete amekiri kwamba katika kipindi cha miezi miwili sasa hasa tangu mwishoni mwa mwezi Mei uhusiano baina ya Tanzania na Rwanda unapitia katika wakati mgumu.

Alisema kauli ya viongozi wa Rwanda dhidi yake (Kikwete) na Tanzania ni ushahidi wa kuwepo hali hiyo.
Hata hivyo, aliwahakikishia Watanzania na Wanyarwanda kwamba serikali na wananchi wanapenda kuwa na uhusiano mzuri na ushirikiano wa karibu na Rwanda kama ilivyo kwa nchi nyengine jirani.

Katika hotuba yake ya kila mwisho wa mwezi, Rais Kikwete alisema kama majirani kila mmoja anamuhitaji mwenzake, hivyo lazima uwepo uhusiano mwema na ushirikiano mzuri.

“Napenda kusisitiza kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza tutakuwa wa mwisho kufanya kitendo au vitendo vibaya dhidi ya Rwanda au nchi yoyote jirani au yoyote duniani. Hatuna sababu ya kufanya hivyo kwani ni mambo ambayo hayana tija wala maslahi kwetu,” alisema.

Alisema ukweli ni kwamba wakati wote Tanzania imekuwa na mambo ya kukuza na kujenga ujirani mwema na kufanya mambo yatakayosaidia kuimarisha uhusiano kwa maslahi ya nchi.

“Hiyo ni moja ya nguzo kuu ya sera ya mambo ya nje ya Tanzania. Huo ndiyo ukweli kuhusu uhusiano wetu na nchi ya Rwanda kabla na hata baada ya sintofahamu iliyojitokeza sasa,” alisema.
Alisema kwa Tanzania hakuna kilichobadilika wala kupungua katika uhusiano na ushirikiano na Rwanda.

“Mambo yapo vile vile, kwa upande wangu, binafsi, sijasema lolote kuhusu Rwanda pamoja na maneno mengi ya matusi na kejeli yanayotoka kwenye vinywa vya viongozi wa Rwanda dhidi yangu,” alisema.

Alisema sio kwamba haambiwi yanayosemwa au hajui kusema au hana la kusema, bali hajafanya hivyo kwa sababu haoni faida yake.

“Kwangu mimi sioni kama kuna mgogoro wa aina yoyote, busara inatuelekeza kuwa tusikuze mgogoro usiokuwepo. Waingereza wanasema “two wrongs do not make a right” alisema.

Rais Kikwete alisema uhusiano na Rwanda ulielekea kupata mtikisiko baada ya yeye kutoa ushauri kwa serikali ya Rwanda kuzungumza na mahasimu wao.

“Ushauri ule niliutoa kwa nia njema kabisa kwani bado naamini kuwa kama jambo linaweza kumalizwa kwa njia ya mazungumzo njia hiyo ni vyema itumike, isitoshe, ushauri ule niliutoa pia kwa serikali ya Kongo na ya Uganda,” alisema.

Alisema katika mkutano huo Rais Yoweri Museveni aliunga mkono kauli yake na Rais wa Rwanda hakusema chochote.“Baada ya kurudi nyumbani ndipo tukaanza kuyasikia maneno tuliyoyasikia na tunayoendelea kuyasikia,” alifafanua.

Kuhusu majambazi na wahamiaji haramu, alisema hawatakuwa na pa kukimbilia baada ya siku 14 alizotoa za kujisalimisha zitakapomalizika na kwamba vikosi vya ulinzi na usalama vitawasaka popote walipo.

Alisema operesheni hiyo itafanyika katika mikoa ya Kigoma, Kagera na Geita kwa wakati mmoja.
“Msisubiri operesheni iwakute, wala wasifikirie kuwa hili ni jambo la kupita. Safari hii itakuwa endelevu,” alionya.

Alisema kamwe hawezi kukubali hali aliyoikuta mkoani Kagera ikaachwa kuendelea kwani italeta madhara makubwa zaidi siku za usoni.

“Haiwezekani raia katika nchi yake, akose uhuru na usalama wa kutembea peke yake mpaka asindikizwe na polisi. Na baya zaidi hata polisi nao wanashambuliwa na kuuawa watakavyo majambazi. Uhalifu huu lazima ukomeshwe, uishe na usijirudie tena,” alisema.

Pia alisema haiwezekani watu kutoka nchi jirani kuingia nchini, kuishi na kufanya shughuli na kutoka watakavyo.

Alisema serikali haizuii watu kuingia na kuishi nchini lakini wafuate sheria na taratibu za uhamiaji.
“Nchi yetu ina sifa na ukarimu huo, hakuna uthibitisho mkubwa zaidi ya ule wa mwaka 1982, Rais Julius Nyerere wakati ule alipowaruhusu wakimbizi wanaopenda kuwa raia wa Tanzania wafanye hivyo,” alisema.

Alisema ameagiza watendaji wa vijiji na serikali wanaoshutumuwa kuwakumbatia wahamiaji haramu na wao wajumuishwe katika operesheni hiyo na watakaobainika kujihusisha watachukuliwa hatua, na kuwataka maafisa wa uhamiaji na TAKUKURU watimize wajibu wao.

Rais Kikwete amewataka Watanzania kuendelea kushirikiana na kuishi kwa upendo, umoja na mshikamano kama ilivyo kawaida yao.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles