Baadhi ya washiriki wa futari ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar Afisi Kuu iliyofanyika katika ukumbi wa Afisi hiyo uliopo Jimkana Mjini Zanzibar ambapo mgeni rasmi alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Baadhi ya Viongozi wa CCM walioshiriki futari ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo Jimkana.
Baadhi ya Viongozi wa CCM walioshiriki futari ya pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif hapo Jimkana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Zanzibar hapo kwenye ukumbi wa umoja huo Jimkana Mjini Zanzibar.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameitahadharisha Jamii nchini kujiepusha na tabia za baadhi ya watu wanaotumia dini katika ushawishi wa kuhatarisha amani ya Nchi.
Alisema uchezewaji wa amani hiyo endapo utavurugika watakaoumia na kupata shida na taabu ni wananchi waliowengi na kamwe hazitowagusa wale waliochangia ushawishi wa kuivuruga amani hiyo.
Balozi Seif alitoa kauli hiyo nzito mara baada ya futari ya pamoja iliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Afisi Kuu Zanzibar iliyofanyika katika ukumbi wa Umoja huo uliopo hapo Jimkana Mjini Zanzibar.
Alisema wananchi walio wengi wamekuwa wakishuhudia hotuba za uchochezi zilizokuwa zikitolewa katika baadhi ya misikiti na mmoja wa sheikh kutoka nje ya Zanzibar ambazo zinahatarisha amani ya Nchi.
Aliwatahadharisha wananchi hasa Vijana kuacha kununua au kutumia kanda zilizorekodiwa hivi karibuni na mhadhiri huyo na kusambazwa katika maeneo mbali mbali nchini.
“ Amekaanga mbuyu yeye na hivi sasa hayupo. Lakini hata Mama watoto wake hayupo, watoto wake hawapo na mama yake pia hayupo. Sasa kapanda chuki jamii inapaswa kujihadhari nayo chuki hiyo. Likitokea vurugu lolote lile tutakaoumia ni sisi na wala sio yeye aliyekaanga mbuyu hizo “. Alitahadharisha Balozi Seif.
Alifahamisha kwamba Taifa limekuwa katika hali ya amani kwa kipindi kirefu sasa hali ambayo ni muhimu katika kustawisha ustawi wa wananchi wote Mjini na Vijijini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alikumbusha kwamba bila ya amani wananchi wasingepata fursa ya kuendelea na shughuli zao za kimaisha za kila siku.
Alisisitiza kwamba wananchi wakati wote wana wajibu wa kukataa maovu sio katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani bali hata katika miezi mengine ya kawaida ili waendelee kuishi kwa amani na upendo.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Umoja wa Vijana wa CCM Afisi Kuu Zanzibar Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai alisema Zanzibar ina hazina kubwa ya Uislamu.
Alisema hazina hiyo ambayo nadra kupatikana katika baadhi ya Nchi haipaswi miongoni mwa waumini wakaichezea kwa kuwaalika mahadhiri wa nje ya Zanzibar kuja kufitinisha waumini.
Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar alimpongeza Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Sheni na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa kauli zao za kila wakati za kusisitiza umuhimu wa kuitunza amani wakati wote.
Vuai Ali Vuai alishauri na kuomba suala hili muhimu kwa ustawi wa Taifa hili lazima likaungwa mkono na vyombo vya Dola hapa Nchini.