Bajeti ya Wizara ya Afya ambayo ilikuwa inajadiliwa katika Mkutano wa bajeti unaondelea imerejeshwa tena katika Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii , kwa ajili ya marekebisho zaidi.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho amesema, Baraza la Wawakilishi limefikia uwamuzi huo baada ya Wajumbe wengi kubaini mapungufu makubwa ya mgawanyo wa fedha katika bajeti ya Wizara hiyo mwaka huu.
Spika Kificho ametowa ufafanuzi huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari huko ofisini kwake Chukwani.
Amesema Wajumbe hao sio tu wamebaini kiasi kidogo cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya wizara hiyo mwaka huu, bali pia maeneo ambayo sio kipaumbele cha Wizara yametengewa fedha nyingi ukilinganisha na maeneo ya kutoa huduma ambayo yametengewa kasma ndogo mno kiasi ambacho kitanguza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa jamii kwa kiwango kikubwa.
Kwa hatua hiyo Mheshimiwa Spika ameagiza bajeti hiyo irudi katika Kamati husika ili ikae tena na Wizara ya Afya pamoja na Watendaji wa Wizara ya Fedha kwa lengo la kurekebisha mapungufu hayo kabla ya kuendelea kujadiliwa tena ndani ya Baraza Jumanne ijayo.
Tukio hili linaonyesha jinsi Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walivyo makini katika kuhakikisha bajeti ya Serikali inakuwa kwa maslahi ya wananchi na si vinginevyo.
Hivi karibuni, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walipatiwa mafunzo kuhusu uchambuzi wa Bajeti kupitia mradi wa Kuimarisha Vyombo vya Kutunga sheria (LSP) na umakini huo wa Wajumbe katika kuijadili Bajeti ya Wizara ya afya unathibitisha namna mafunzo hayo yalivyosaidia katika kuwajengea Wajumbe uwezo katika eneo hilo la kujadili na kupitisha bajeti.