Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Balozi Seif akagua maendeleo ya uimarishaji wa mashamba ya Mikarafuu ya serikali

$
0
0
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Wizara ya Kilimo na Mali asili Zanzibar imeshauriwa kuzingatia utaratibu muwafaka wa kukodisha mashamba ya Mikarafuu ya Serikali yaliyo chini ya Wizara hiyio kwa kutumia mfumo wa mnada ili kuwaondoshea wasi wasi wananchi wanaojitokeza kutaka kukodishwa mashamba hayo.
 
Ushauri huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa kisiwani Pemba kwa ziara ya siku mbili kukagua maendeleo ya uimarishaji wa Mashamba ya Mikarafuu ya Serikali, miradi ya kilimo mchanganyiko pamoja na baadhi ya
miradi ya kiuchumi na Maendeleo Kisiwani humo.
 
Balozi Seif alisema yapo malalamiko kadhaa yanayoendelea kutolewa na baadhi ya wananchi wanao nia ya kodi Mashamba ya Mikarafuu ya Serikali kufuatia mfumo unaotumiwa wa utoaji wa tenda wakati wa ukodishwaji huo jambo ambalo hutoa fursa kwa watu maalum kuitumia fursa hiyo.
 
Alisema mfumo wa mnada ni mpango ulio wazi unaotoa fursa kwa Mwananchi yeyote kukodi mashamba hayo kwa mujibu wa uwezo aliokuwa nao bila ya kuleta usumbufu , lawama au upendeleo wowote.
 
“ Mnada ni mpango wa wazi katika ukodishaji wa mashamba au kitu chochote kwa vile huondoa lawama na manung’uniko miongoni mwa watu wenye nia ya kutaka kukodi mashamba ya Serikali “. Alisema Balozi Seif.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar kwa jitihada zake za kuimarisha mashamba ya Serikali yaliyo chini ya Wizara hiyo akalitolea mfano Shamba la Serikali la Makuwe liliopo Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba.
 
Balozi Seif akielezea faraja yake kutokana na uendelezwaji wa mashamba hayo na kuiagiza Wizara hiyo kuhakikisha kwamba kasma wanayoipata katika uendelezaji wa mashamba hayo inaelekezwa katika uimarishaji huo.
 
Alisema hatua hiyo ni vyema ikaenda sambamba na utolewaji wa kipaumbele kwa wananchi wanaojitolea kwa makusudi kuyafanyia usafi wa mazingira mashamba wanayokodishwa na Serikali.
 
Alisisitiza kwamba Serikali bado inaamini kwamba bei ya zao la karafuu katika masoko ya Kimataifa itaendelea kuwa juu kutokana na hatua za baadhi ya Nchi na Mashirika kuweka nafasi maalum ya kutaka kununua Karafuu za Zanzibar katika msimu ujayo.
 
Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar Nd. Afan Othman Maalim alisema shamba hilo la Makue lenye ukubwa wa Ekari 200 lilitengwa maalum na Serikali kwa lengo la kuendeleza mazao ya Biashara, Viungo pamoja na uoteshaji wa vitalu kitaalamu vya miti mbali mbali ili kusaidia wakulima.
 
Nd. Afan alisema Wizara hiyo tayari imeshaotesha miti ya Mikafaruu ipatayo mia sita kwa awamu ya kwanza na 400 awamu ya Pili ndani ya shamba hilo lenye uwezo wa kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi Milioni 35,000,000/- kwa msimu mmoja endapo litakuwa katika hali nzuri.
 
Hata hivyo Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili alisema ili kufikia lengo hilo usafishaji maalum wa shamba hilo kwa hatua ya kwanza wenye gharama ya shilingi Milioni 15,000,000/- unahitajika.
 
Naye Afisa mdhamini Wizara ya Kilimo na Mali Asili Pemba Dr. Suleiman Sheikh alisema shamba la Kilimo la Makuwe mbali ya kutegemewa kwa uzalishaji wa karafuu lakini pia hujikita katika uzalishaji wa mazao ya Viungo.
 
Dr. Suleiman alisema moja kati ya mapato makubwa yanayoingia Serikalini kupitia vianzio vyake mbali mbali ni pamoja na mashamba ya Serikali hasa yale yaliyo chini ya Wizara hiyo.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika ziara yake hiyo pia alipata fursa ya kukagua shamba darasa  la Skuli ya Wakulima wa Kilimo cha mpunga liliopo Kibokoni Vitongoji Wilaya ya Chake chake.
 
Akitoa Taarifa fupi  ya Mradi wa Kilimo cha Mpunga kwenye skuli ya wakulima wa mpunga kinachoendelezwa na Kibokoni Saccos Meneja wa Mradi huo Said Yussuf Kombo alisema mradi huo umekuwa ukitoa mafunzo kwa wakulima wanafunzi wapatao 533 kutoka maeneo mbali mbali ya Kisiwa cha Pemba.
 
Ndugu Said Yussuf alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba skuli za wakulima nchini  ndio njia pekee zinazoibua kilimo cha kisasa na tayari yapo mafanikio makubwa kwa baadhi ya wakulima waliopata mafunzo kupitia skuli hizo.
 
Meneja mradi huyo wa skuli ya wakulima Kobokoni Vitongoji alieleza kwamba mradi huo umekuwa ukiendesha mafunzo ya kilimo kwa majaribio ya mazao ya mpunga, mahindi kwa kutumia mbolea ya mavi ya mbuzi.
 
Naye kwa upande wake mwakilishi wa Taasisi ya misaada ya zana na vifaa vya miradi mbali mbali ya kiuchumi na kijamii yenye makao makuu yake Nchini Italy Bwana Yahya Sawafy alisema mradi huo umekuwa ukiendeshwa kwa ubia kati ya taasisi hiyo kwa kushirikiana na Saccos ya Kibokoni.
 
Sheikh yahya alisema juhudi za kitaalamu zimeshachukuliwa kupitiaMtaalamu wa Taasisi hiyo aliyefika Kisiwani Pemba kulipima eneo hilo kwa lengo la kujenga mazingira yatakayowezesha uzalishaji wa eneo hilo uwe wa kitaalamu zaidi.
 
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi Seif alisema taaluma wanazopatiwa wakulima sehemu mbali mbali za Zanzibar zifikie wakati wa Visiwa hivi kuzalisha mpunga utakaotoa mchele wenye hadhi ya hali ya juu.
 
Alisema utafiti wa mbegu mbali mbali utakaofanywa na wakulima, wataalamu wa kilimo kwa kushirikiana na taasisi za kitaifa na kimataifa ndio njia ya msingi itakayofanikisha azma hiyo.
 
Aliwahimiza wakulima hao kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa kilimo ili wafikie kiwango cha kuzalisha mazao yenye kiwango hatua ambayo itapunguza nguvu kubwa walizokuwa wakizitumia kwenye ukulima cha asili.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>