Na Mwandishi wetu
Kikao cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar (BLW), kimeahirishwa kwa mara ya pili kutokana na idadi ya wajumbe kutotimia kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria, Zanzibar.
Kikao hicho kiliahirishwa na Naibu Spika, Ali Abdallah Ali jana saa kumi na moja jioni baada ya Mwakilishi wa Mji Mkongwe (CUF), Ismail Jussa Ladhu kutoa hoja kutokana na mahudhurio ya wajumbe kutokamilika.
Jussa alisema BLW Zanzibar linaendeshwa kwa kuzingatia kanuni na suala la kukamilika kwa idadi ya wajumbe wanaotakiwa limepewa uzito na chombo hicho na kumtaka Naibu Spika kutoa hoja kutokana na hali iliyojitokeza.
“Mheshimiwa Naibu Spika, chombo chetu kinaongozwa na kanuni, idadi ya wajumbe iliyopo ni ndogo kimuonekano na hesabu yake, naomba kutoa hoja na kupendekeza kikao kiahirishwe kutokana na upungufu huo,” alisema Jussa
Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, Naibu Spika aliungana na Jussa na kuahirisha kikao hicho hadi leo asubuhi.
Baraza hilo lilikuwa liketi jana jioni kama kamati ya matumizi kupitia na kupitisha vifungu vya matumizi ya Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ya Sh7.5 bilioni ambayo yaliwasilishwa na Waziri wake, Zaynab Omar Mohamed.
Mara ya kwanza kuahirishwa kwa kikao hicho kutokana na akidi ya wajumbe wake 82 kutokamilika ilikuwa Mei 26, mwaka huu. Hadi kikao hicho kinaahirishwa kulikuwa na wajumbe 26.
Baadhi ya wajumbe wa BLW Zanzibar wamekuwa wakitumia usafiri wa daladala kwenda na kurudi kutoka kwenye kikao hicho na wengine kutofika kwa muda mwafaka tangu kufanyika kwa mabadiliko ya vituo vya usafiri huo katika Manispaa ya Mji wa Zanzibar.
Wajumbe wa Baraza hilo kila mmoja hulipwa posho ya kikao ya Sh150,000 kwa siku mbali na mshahara wa Sh4.5 milioni kwa mwezi.
Chanzo: Mwananchi