Msafara wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi ukielekea Kisiwa panza kukagua shughuli za Chama ndani ya kisiwa hicho kiliopo kusini mwa Mkoa wa Kusini Pemba.
Kikundi cha ngoma cha Mkuta ngoma cha jimbo la mkanyageni kikitopa burdani kwenye mkutano wa hadhara wa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Kisiwani Panza.
Mjumbe wa Halmashauri ya CCM Tawi la Mtondooni Kisiwani Panza Nd.Khamis Juma Othman akimfahamisha Balozi Seif hatua waliyofikia ya ujenzi wa Tawi lao .
Mwenyekiti wa Tawi la CCM Mtondooni Kisiwa Panza Nd.Nassor Juma Amir akipokea mchango wa shilingi Milioni 2,000,000/- kutoka kwa Balozi Seif kusaidia uendelezaji wa Tawi lao la CCM.
Picha na Hassan Issa wa – OMPR – ZNZ.
Na Othman Khamis Ame, OMPR
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema Chama cha Mapinduzi kina wajibu wa kuhakikisha kinashinda kwenye uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2015 ili kiendelee kusimamia uhimili wa amani ya Taifa iliyopo hivi sasa.
Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi pamojana Wana CCM wa Kisiwa Panza Wilaya ya Makoani Pemba mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Tawi la Chama cha Mapinduzi la Mtondooni Kisiwani humo.
Alisema ushindi huo utapatikana endapo wana CCM wenyewe na hasa Vijana watajitahidi kushikamana katika kuhakikisha kwamba kila mwanachama wa chama hicho atakuwa na kitambulisho kitakachompa fursa kamili ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo.
Balozi Seif aliwataka wana CCM hao kuwa makini wakati huu wa uhakiki wa Daftari la kudumu la wapiga kura na kumbanini mtu yeyote asiyestahiki kupiga kura kwenye eneo lao ili wamuekee pingamizi.
Aliwapongeza wana CCM hao wa Kisiwa Panza kwa uamuzi wao wa kuendelea kukiunga mkono chama hicho hasa katika kipindi hichi ambacho taifa liko katika mchakato wa kupata katiba mpya ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema umakini wao wa kuamini mfumo wa serikali mbili unaopendekezwa na Chama cha Mapinduzi unaongwa mkono na wazanzibari walio wengi katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba.
Katika kuunga mkono juhudi za wana CCM hao Balozi Seif alichangia shilingi Milioni
2,000,000/- taslim kwa ajili ya kuongeza nguvu za ujenzi wa Tawi hilo la CCM la Mtondooni Kisiwa Panza.
Akigusia suala la amani Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza Wananchi wote wa Kisiwa cha Pemba kwa kuendelea kuilinda amani iliyopo Nchini.
Alisema Serikali inaendelea na operesheni kufuatilia tukio la hivi karibu la kuripuka kwa bomu katika eneo la Darajani na kusababisha kuuawa kwa mtu mmoja asiye na hatia na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Vitendo hivyo viovu vinavyotishia wasi wasi kwa wananchi vinaweza pia kuleta athari kubwa katika kuboresha sekta ya utalii inayotegemewa sana hivi sasa katika kukuza uchumi wa Taifa.
“ Kwa kweli Serikali haitavumilia kuona vikundi vya baadhi ya watu vinasababisha au kuchangia katika kuchochea amani ya nchi. Vitendo hivi vinatishia kuporomoka kwa sekta ya Utalii “. Mahoteli mengi tumejenga sasa kwa muendelezo wa tabia hii atakuja kukaa nani ? Alisema Balozi Seif “.
Kuhusu suala la jengo la Skuli ya Sekondari ya Kisiwa hicho lililokamilika Balozi Seif aliwaeleza wana CCM na wananchi wa Kisiwa hicho kwamba atawasiliana na Waziri wa Elimu ili kuapatiwa vikalio skuli hiyo ili ianze kazi mara moja.
Alisema hatua ya kuanza kwa darasa hilo la sekondari itawaondoshea usumbufu na mashaka wanafunzi hao ya kuvuka mkondo wa bahari kila siku jambo ambalo ni hatari hasa wakati wa hali mbaya ya bahari.
Mapema katika taarifa yao iliyosomwa na Mjumbe wa Halmashauri ya Tawi la Mtondooni Kisiwa Panza Nd. Khamis Juma Othman alisema wananchi wa kisiwa hichobado wanakabilisha na ukosefu wa mikopo kwa ajili ya kuendeshea miradi yao ya maendeleo.
Nd. Juma alieleza kwamba wananchi wa kisiwa hicho wanakipongeza chama cha Mapinduzi kupitia serikali zake mbili kwa juhudi zake za kutekeleza ilani na chama hicho kwa vitendo.
Alisema juhudi zilizochukuliwa na Waziri wa sayansi teknolojia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Makame Mnyaa Mbarawa za kuwapatia huduma za maji safi na salama zimeleta faraja kubwa kwa wananchi hao.