Na: Hassan Hamad (OMKR).
Mkutano Mkuu wa sita wa CUF umeanza rasmi huku ukihudhuriwa na viongozi na wawakilishi wa vyama vya siasa na jumuiya kadhaa za Kimataifa.
Akifungua mkutano huo unaofanyika ukumbi wa Ubungo Plaza, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amesema mkutano huo unadhihirisha ukomavu wa demokrasia ndani ya Chama hicho.
Amewataka wajumbe watakaochaguliwa kuunganisha nguvu zao kuhakikisha kuwa chama hicho kinatimiza malengo yake ya kushika hatamu za uongozi na kuwatumikia wananchi kama kilivyoahidi kwenye sera zake.
Akizungumzia hali ya uchumi Prof. Lipumba amesema bado Watanzania wanakabiliwa na tatizo kubwa la ajira linalopelekea kupunguza kipato na ustawi wa wananchi.
Amesema iwapo rasilimali za nchi zitatumiwa vizuri na kuweka mbele maslahi ya Taifa, linaweza kupiga hatua kubwa ya maendeleo na kuwapunguzia wananchi ukali wa maisha unaoendelea kuwakabili.
Nae Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema uongozi mpya utakaochaguliwa una wajibu wa kushirikiana na wananchi na kuweka mikakati imara kwa lengo la kukiimarisha chama hicho kuweza kukabiliana na kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Akizungumzia maudhui ya mkutano huo Maalim Seif amesema pamoja na mambo mengine mkutano hu utapokea na kujadili kazi za chama kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita pamoja na kuchaguliwa kwa viongozi wakuu wa chama hicho ngazi ya Taifa.
Aidha amesema mkutano huo utapitia na kufanya marekebisho ya katiba ya chama hicho ili iende sambamba na wakati uliopo. Mkutano huo pia utawachagua wajumbe wa baraza kuu la uongozi pamoja na viongozi wa nafasi za wanawake.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, Freeman Mbowe ambaye amekiwakilisha chama chake katika mkutano huo, amewapongeza viongozi wa CUF kwa kuandaa mkutano huo ambao utaendeleza gurudumu la demokrasia ndani ya chama hicho na Taifa kwa ujumla.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Mhe. Mbowe amesema ushirika wa CHADEMA ndani umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) utakuwa wa kudumu na wala sio wa mpito kama unavyodhaniwa na baadhi ya watu.
Pia Mbowe amehimiza siasa za kistaarabu katika nchi, na kwamba siasa za ugomvi, chuki na uhasama zimepitwa na wakati.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Bw. Philip Mangula ametaka ushirikiano wa vyama vya siasa katika ngazi za Kitaifa uenezwe katika ngazi zote za uongozi ili kuimarisha demokrasia nchini.
Aidha amesifu mshikamano unaooneshwa na baadhi ya vyama vya siasa nchini kwa kuamua kuunganisha nguvu zao katika siasa.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwenyekiti wa chama cha ADC Bw. Said Miraji ambaye pia amehudhuria mkutano huo mkuu wa CUF amepongeza maendeleo yaliyopatikana ndani ya Chama hicho katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Pia ameelezea kufurahishwa na mfumo wa CUF wa kuendelesha chaguzi zake ambapo amesema chaguzi za chama hicho ziko huru dhidi ya vitendo vya rushwa.