Na Fatma Kassim, Maelezo
BODI ya Chakula Dawa na Vipodozi, imeangamiza bidhaa chakula zenye uzito wa tani 25 baada ya kubainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Bidhaa hizo ni pamoja na maziwa ya kopo aina ya NAN tani 7.4, soda za kopo, chama tani tano, tende tani 10, mchele tani 1.1 na vyakula mchanganyiko tani moja ambapo uangamizaji huo ulifanywa Kibele mkoa wa kusini Unguja.
Mkuu wa ukaguzi wa bodi hiyo, Aisha Suleiman, alisema bidhaa hizo zimekamata kufuatia ukaguzi unaofanywa bandarini, madukani na maghala yanayohifadhia bidhaa hizo.
Alisema soda hizo zimeingizwa nchini zikiwa na tarehe iliyotengenezwa na hazina tarehe ya kumala muda wa matumzi jambo ambalo linaweza kuhatarisha afya za watumiaji.
Alisema mchele ulioangamizwa ni sehemu ya tani 26 za mchele uliorejeshwa nchini Pakistan baada ya kuonekana haufai kwa matumizi ya binaadamu.
Alisema gharama zote za uangamizaji wa vyakula hivyo kwa mujibu wa sheria ya bodi, zinatolewa na wenye mali .
Aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa bodi hiyo endapo watatilia shaka bidhaa za aina yoyote ile zikiingizwa nchini au zikiwa madukani kwa kuuzwa.