Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

SMZ kufanya utafiti wa mifugo

$
0
0
Na Husna Mohammed
 WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdillah Jihad Hassan, amesema serikali inakusudia kuimarisha shughuli za utafiti katika masuala ya mifugo sambamba na kutoa elimu kwa wafugaji.

Alisema hayo jana katika kikao cha baraza la wawakilishi kinachoendelea mjini hapa wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2014/2015.

Alisema sekta ya mifugo itaimarishwa ikiwa ni pamoja na kuvipatia dawa na vitetendea kazi vituo vitatu vya utafiti.

“Tutafanya utafiti wa kuangalia uzalishaji wa kuku chotara wa nyama na kabila ya kiasili ya kuchi, kufanya utafiti juu ya vikwazo vya ufugaji mbuzi katika kijiji cha Kiuyu Mbuyuni,” alisema.

Aidha alisema wataimarisha utoaji wa elimu kwa wafugaji katika nyanja za utunzaji, uzalishaji, usarifu wa bidhaa za mifugo na masoko kwa kuwawezesha wasaidizi mabwana mifugo 20 kuwafikia wafugaji wapatao 20,000.

Alisema katika mwaka huo wa fedha wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mifugo na matumizi bora ya mazao ya mifugo kwa kuanzisha mashamba yapatayo 40 ya malisho katika eneo la Kizimbani.

“Tutalima na kupanda jumla ya eka tano za majani katika kituo cha malisho huko Kizimbani na shamba la Chamanangwe kisiwani Pemba pamoja na kuchangia gharama za ujenzi wa mitambo 10 ya biogesi,” alisema.


Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa jumla ya shilingi 11,591,053,000 kwa ajili ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Kwa upande wake, Kamati ya Mifugo, Utalii, Uwezeshaji na Habari,imesikitishwa na wizara hiyo kwa kutoweza kutayarisha sera ya uvuvi na mazao ya baharini.

Mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Amina Iddi Mabrouk, akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, katika kikao cha baraza la wawakilishi, alisema kamati imesikitishwa na kutotayarishwa kwa sera hiyo jambo ambalo linaonesha serikali ni nzuri ya kupanga lakini inakosa umakini wa kutosha wa utekelezaji wa mipango yake.

“Kazi hii haikufanyika kwa madai ya kukosa nyenzo ambapo kamati imeelezwa kwamba kazi hii inatarajiwa kutekelezwa katika mradi wa SMART Fish,” alisema.

Sambamba na hilo kamati hiyo pia imesema imesikitishwa kwa kutoongezeka makusanyo ya leseni za uvuvi wa ndani na nje  na kufikia kiwango sawa cha makusanyo kama ya mwaka jana.

Aidha kamati hiyo iliitaka wizara kuongeza nafasi za uzalishaji wa ajira 120 kwa vijana kupitia mradi wa kuendeleza wafugaji wadogo.

Kamati hiyo pia ilitoa wito wa kutekeleza sekta ya mazao na mifugo kwa kuimarisha utoaji wa huduma za mifugo kwa jamii pamoja na kuimarisha mazingira ya utendaji kazi kwa kutumia mikakati mbalimbali.

Akichangia hotuba ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwakilishi Asaa Othman (Wete), alisema  sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto kubwa juu ya wafugaji na wajasiriamali kukosa mitaji ambayo itawawezesha kufikia malengo waliojiwekea.

Alisema wafugaji ni lazima wabadilike kwa kupatiwa taaluma bora ya ufugaji kwani kufanya hivyo kutapelekea kupunguza maradhi.

Akizungumzia suala la utumishi, alisema ni vyema wafanyakazi kupatiwa mafunzo endelevu ya kikazi ili kwenda na wakati wa sayansi na teknolojia.

Nae Mwakilishi wa jimbo la Kojani, Mhe. Hassan Hamad, alisema sheria ya uvuvi ya nambari 7 ya mwaka 2010 kwa mahitaji ya sasa imepitwa na wakati na inahitaji marekebisho makubwa.


Mwakilishi wa nafasi za wanawake, Kazija Kona, alisema wakati umefika sasa kwa serikali kuwaendeleza vijana wa kizanzibari katika sekta ya uvuvi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>