Na Joseph Ngilisho,Arusha
SAKATA la msichana wa ndani mwenye umri wa miaka 16,aliyedaiwa kuuliwa na mama mwenye nyumba, aliyetajwa kwa jina la Valentina Maxmillan (37) mkazi wa en Moromboo jijini hapa,limechukua sura mpya baada ya mume wa mwanamke huyo,John Mwacha, kuibuka na kusema kwamba amemwachia Mungu suala hilo.
Taarifa za awali zinadai kwamba mke wa mfanyabiashara huyo (Valentina) aliimuua msichana wake wa ndani na kisha maiti yake kuipeleka usiku wa manane hospitali ya mkoa Mount Meru,kisha wao kurejea nyumbani na kuendelea kuangalia mechi ya kombe la dunia kwenye televisheni.
Mmoja wa majirani katika eneo anakoishi mtuhumiwa wa mauaji hayo, ambaye aliomba jina lake kutojatwa gazetini, alisema mwanamke huyo ambaye ni jirani yao amekuwa akimtesa msichana huyo kwa muda mrefu kwa kumpiga,kunyonyoa nywele na wakati mwingine kumnyima hata chakula na kusababisha afya ya msichana huyo kudhoofika.
Alisema siku ya tukio walisikia kelele na mtu akilia huku kelele hizo zikiambatana na sauti ikisema ‘leo ndio mwisho wako’,hata hivyo majira ya usiku wa manane mlinzi wa duka la vifaa vya ujenzi lililopo jirani na nyumba ya mtuhumiwa, aliona gari ndogo zikija katika nyumba hiyo kisha mlango kufunguliwa.
Naye mlinzi huyo (jina linahifadhiwa),alisema aliona gari mbili ndogo zenye rangi nyeupe zikija kwa nyakati tofauti.
“Gari ya kwanza ilifika na kukaa kwa muda kama dakika kumi ikaondoka nahisi walishindwa kupatana gari hiyo ikaondoka,baada ya dakika 20 ilikuja gari nyingine na baadae lango lilifunguliwa,niliona kitu kama furushi likiwa limefunikwa nguo huku baba mwenye nyumba ndiye aliyekuwa amebeba na kuweka kwenye gari,” alisema.
“Nilishangaa kusikia baadae asubuhi kuwa kumbe lile furushi lilikuwa lina maiti ya huyo msichana,” alisema.
Hata hivyo, mlinzi huyo alisema yeye binafsi hajui chanzo cha kifo cha msichana huyo na alikuwa hamfahamu kwani yeye amekuwa akifika eneo lake la kazi majira ya jioni na kuondoka asubuhi.
Habari zaidi zinaeleza kuwa baada ya kufichuka kwa tukio hilo ambalo lilifanywa siri na familia hiyo,mmoja wa majirani alitoa taarifa kituo cha polisi na askari polisi waliokuwa doria walifika nyumbani kwa mtuhumiwa.
Mmoja wa askari polisi aliyefika nyumbani kwa mtuhumiwa kwa lengo la kufanya uchunguzi,ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini,alisema baada ya kufika katika nyumba hiyo siku hiyo, majira ya usiku walitumia zaidi ya saa moja kugonga lango la kuingilia bila kufunguliwa licha ya kujitambulisha wao ni askari polisi.
Alidai kuwa baadae askari hao walitishia kuvunja mlango ndipo mtoto mmoja alifika na kufungua lango hilo,huku akiwaeleza askari hao kuwa mama yake hayupo,hata hivyo askari hao wakiwa na silaha waliamua kuingia ndani ndipo walipowakuta watuhumiwa hao wakiangalia mpira.
Askari hao waliondoka na watuhumiwa hadi kituo kidogo cha polisi Mbauda ambako walitoa maelezo na baadae kudhaminiwa baada ya kuwepo taarifa kuwa msichana huyo alifariki kwa kifafa.
Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu,mume wa mwanamke huyo,ambaye ni mfanyabiashara wa nguo za mitumba,John Mwacha,,alieleza masikitiko yake sambamba na kukanusha madai yanayoelekezwa kwa mkewe kuwa alimuua kikatili msichana wake wa kazi.
Kamanda wa polisi mkoani Arusha,Liberatus Sabas,alithibitisha tukio hilo na kuelezaa kuwa mwili wa marehemu ulisafirishwa kuelekea nyumbani kwao wilayani Muleba,mkoani Kagera kwa mazishi.