HOTUBA MAALUM YA WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA KWANZA WA RAIS MHE. FATMA ABDULHABIB FEREJ YA MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA UPIGAJI VITA MATUMIZI NA USAFIRISHAJI WA DAWA HARAMU ZA KULEVYA DUNIANI- JUNE 26, 2014
--------------------------------------------------------------------------------------
Ndugu Wananchi
Assalamu Aleykum,
Hatuna budi kutanguliza shukurani zetu Kwake Yeye Mwenyezi Mungu Subhaallah Wataala Aliyetukuka Mwingi wa Rehma kwa kutupatia rasilimali adhimu ya kuwa katika hali ya afya, uzima, amani na utulivu katika jamii yetu. Aidha napenda nichukue fursa hii kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kutujaalie Rehema na Baraka zake katika maisha yetu yote na nchi yetu kuendelea kuwa na amani, utulivu na masikilizano – AMIN.
Nichukue nafasi hii pia kuvipongeza vyombo vya habari nchini kwa mchango mkubwa vinavyotoa katika kuelimisha jamii katika masuala mbali mbali ambayo naamini yanachangia katika kuleta ustawi na maendeleo kwa taifa letu kwa ujumla.
Ndugu Wananchi,
Ni wakati mwengine tena Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa Kulevya inaungana na jamii ya kimataifa katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upigaji Vita Matumizi na Usafirishaji wa Dawa Haramu za Kulevya (International Day Against Drug Abuse and Illicit Trafficking) ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 26 ya mwezi wa Juni ya kila mwaka duniani kote.
Siku hii adhimu ilipitishwa rasmi katika azimio nambari 42/112 la Umoja wa Mataifa mnamo mwezi wa Disemba 1987 likiwa na lengo kuu la kutanabahisha juu ya athari mbali mbali zinazoambatana na tatizo la dawa za kulevya, kusisitiza mshikamano duniani kote na kuongeza nguvu na ushirikiano kwa jumuiya za kitaifa na kimataifa ili kushinda vita dhidi ya dawa za kulevya na kuiweka jamii kuwa huru na matumizi ya dawa hizo. Siku hii huratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalopambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu Duniani. (United Nations Office on Drugs and Crimes – UNODC).
Ndugu Wananchi,
Kwa mnasaba wa maadhimisho haya, Shirika la Umoja wa Mataifa la Dawa za Kulevya na Uhalifu huja na ujumbe au kauli mbiu ya maadhimsho haya ambayo kwa mwaka huu inasema “ Ujumbe wa Matumaini: Matumizi ya Dawa za Kulevya Yanakingika na Yanaweza Kutibika ’’ ( A message of Hope : Drug Use Disorders is Preventable and Treatable).
Ujumbe au kauli mbiu hii ya kimataifa inalenga katika kuwepo mwitiko maalum na wa makusudi katika kuongeza juhudi na mikakati juu ya utoaji wa taaluma za awali za kinga zinazolenga kuinusuru jamii kutojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na kwamba matokeo ya matumizi ya dawa hizo yanaweza kupatiwa huduma muafaka za tiba.
Ndugu Wananchi
Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Dawa za Kulevya na Uhalifu ya mwaka 2013 (World Drug Report 2013) inayotolewa kila mwaka imeeleza kwamba tatizo la dawa za kulevya limeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za watu, usalama na ustawi wa maendeleo ya jamii kwa ujumla , kurejesha nyuma uchumi na hali ya utulivu wa kisiasa duniani kote, taarifa hiyo inasisitiza kwamba ni lazima juhudi za makusudi kuchukuliwa katika kukabiliana na hali hiyo.
Aidha, taarifa hiyo ya UNODC imeongeza kwamba matumizi ya dawa za kulevya na maambukizi ya virusi vya UKIMWI bado ni changamoto na tishio katika masuala ya kiafya kwa mataifa mengi duniani hususan kwa yale maeneo ambayo maambukizi yamekuwa yakichangiwa na makundi maalum ikiwemo watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano.
Aidha kumekuwa na matokeo ya kupungua kwa maambukizi mapya kwa makundi hayo kwa yale mataifa yanayozingatia Mkakati wa Upatikanaji wa Huduma kwa Wote (The Universal Access) na programmu za mpango wa huduma kwa watumiaji wa dawa za kulevya wanaojidunga sindano (Comprehensive Package for Injecting Drug Users) ambao ulipitishwa na Jamii ya kimataifa kupitia Mkutano wa Ngazi ya Juu wa UKIMWI wa Mwaka 2006 . Shirika la Umoja wa Mataifa la Dawa za Kulevya na Uhalifu ( UNODC) kwa kushirikina na Shirika la Afya Duniani ( WHO) zimefanya tafiti mbali mbali zinazoenyesha upunguaji wa maambukizi ya virusi vya UKIMWI kupitia mpango wa programu hizo.
Ndugu Wananchi,
Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa kufuatia utafiti uliofanywa hapo Zanzibar zinaonyesha kuwepo kwa jumla ya watumiaji elfu tatu (3,000) wa dawa za kulevya, ikijumuisha wale wanaotumia dawa hizo kwa njia ya kujidunga sindano. Aidha maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa watumiaji wa dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano yamepungua kutoka asilimia kumi na sita (16%) kwa mwaka 2007 na kufikia asilimia kum na tatu (13%) kwa mwaka 2012. Aidha huduma kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya kupitia nyumba za Marekebisho zilizoanza karibu miaka minne iliyopita maarufu Sober House Unguja na Pemba zimekuwa chachu ya mafanikio kwa vijana katika kujivua na matumizi ya dawa hizo. Kwa kipindi cha 2009-2013 jumla ya vijana elfu moja mia tano na arobaini (1,540) waliweza kupatiwa huduma katika makaazi hayo na asilimia thethalini ( 30%) waliweza kujivua na matumizi ya dawa hizo na kuendelea na harakati zao za kimaisha. Huduma na juhudi hizo ambazo zimekuwa mfano wa kuigwa katika baadhi ya nchi za jirani zinapaswa kupongezwa na kupewa kila aina ya msukumo.
Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais kupitia Tume ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya itaendelea kutoa kila aina ya msukumo katika kuendeleza mbele huduma za makaazi kwa vijana wanaoacha matumizi ya dawa za kulevya maarufu Sober Houses zinazoendeshwa na taasisi zisizo za kiserikali Unguja na Pemba.
Ndugu Wananchi,
Wengi wetu ni mashahidi wa athari mbalimbali zinazotokana na matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo ongezeko la vitendo vya uhalifu, kutokuwepo kwa amani, magonjwa ya akili, kupotea kwa rasilimali watu ya vijana na hata vifo na hivyo hatupaswi kufumbiwa macho harakati na vitendo vya uuzaji wa dawa za kulevya katika maeneo yetu hasa ikizingatiwa kwamba waathirika wakubwa ni vijana ambao ni rasilimali na nguvu kazi kuu ya taifa lolote duniani, na wanahitaji kuenziwa kwa kila hali. Maendeleo ya taifa lolote hutegemea zaidi nguvu ya vijana wenye mwelekeo makini na hivyo hatma ya nchi yetu ya kufikia Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya 2020 na Malengo ya Dunia ya Melenia (Millennium Development Goal) kamwe hayataweza kufikiwa iwapo vijana wataendelea kujitumbukiza katika janga la utumiaji wa mihadharati.
Ndugu Wananchi
Kwa mnasaba wa kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku hii naomba nichukue nafasi hii adhimu ya kuviomba vyombo vya habari nchini kuchukua juhudi za makusudi kwa kushirikina na taasisi husika katika kuelimisha jamii kwa kutoa makala na taarifa mbali mbali sahihi zenye lengo la kuikinga jamii na hususan vijana katika kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya. Aidha familia na jamii kwa ujumla kuwa karibu na vijana wao na kufuatilia nyendo na harakati zao na kuwapatia maadili memo kwa lengo la kuwanusuru na kuwakinga katika kujiingiza kwenye vitendo viovu ikiwemo matumizi ya dawa za kulevya.
Ndugu Wananchi,
Pia Napenda kutoa shukurani zangu za dhati kwa mashirika mbalimbali ya nje na ndani kwa misaada yao ya hali na mali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya hapa Zanzibar,baadhi ya mashirika hayo ni UNODC ,AIHA,ICAP,FHI na CDC. Aidha, shukurani za dhati ningependa kuziwasilisha kwa Jumuiya zisizo za kiserikali hapa Zanzibar (NGO’s) kwa juhudi zao katika kuunga mkono mwitiko wa Serikali katika vita Dhidi ya Dawa za Kulevya nchini.
Ndugu Wananchi,
Mwisho ningependa tufahamu kwamba kila mmoja wetu kwa nafasi yake ikijumuisha, taasisi zisizo za kiserikali, elimu, Jumuiya za kidini, wafanyabiashara kwa ujumla kuunganisha nguvu zetu ikiwa ni sehemu ya Maadhimsho haya adhimu na pia katika kuongeza kasi ya Mapambano Dhidi ya Dawa za Kulevya nchini na kuwanusuru vijana wetu ambao ni tegemeo la taifa letu.
“ZANZIBAR BILA YA DAWA YA KULEVYA INAWEZEKANA”
Ahsanteni kwa kunisikiliza na Inshaallh Mwenyezi Mungu Awabariki