Na.Abdi Suleiman na Sada Ali, Pemba
HUDUMA za upasuaji katika hospitali ya wilaya Chake Chake zimesitishwa kutokana na kuharibika mashine ya kuwawekea dawa ya usingizi wagonjwa wanaohitaji kufanyia upasuaji (anaesthetic machine).
Mashine hiyo iliharibika tokea Juni 20 mwaka huu na kusababisha wagonjwa waliokuwa wamelazwa kusubiri kufanyiwa upasuaji kuhamishiwa hospitali za Wete na Abdalla Mzee Mkoani.
Kuharibika kwa mashine hiyo ni pigo kwa wagonjwa wanaofikishwa hospitalini hapo kufanyiwa upasuaji.
Baadhi ya madaktari, walisema mashine hiyo iliyoharibika ni kongwe na ililetwa tokea mwaka 1992 wakati hospitali hiyo ikianzishwa.
Aidha aliwasema mashine hiyo imeshafaniwa matengenezo zaidi ya mara tano.
Akizungumzia suala hilo, Daktari bingwa wa masuala ya upasuaji katika hospitali hiyo, Shaban Issa, alisema kuharibika kwa kifaa hicho kumesababisha kuzorota kwa huduma za upasuaji.
Alisema tayari wameshaandika barua mara kwa mara kuhusu ubovu wa mashine hiyo lakini bado juhudi za kutafutwa nyengine hazijachukuliwa.
Alisema hospitali hiyo imekuwa ikifanya upasuaji mkubwa kwa wagongwa kati ya watatu na wanne kwa wiki, mbali ya wanawake wajawazito wanaozaa kwa upasaji.
Nae daktari dhamana wa hospitali hiyo,Yussuf Hamad, alithibitisha kuharibika kwa mashine hiyo, huku akisema suala hilo liko kwenye mikono ya Ofisa Mdhamini wa wizara hiyo.
Naye Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Afya Pemba, Dk. Mkasha Hija Mkasha, aliwataka wananchi kuwa na subra katika kipindi hiki ambacho wizara inatafuta mbinu ya kupata mashine mpya.