Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Hotuba ya maoni ya Kamati ya Maendeleo ya wanawake na ustawi wa Jamii BLW

$
0
0

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA MAENDELEO YA WANAWAKE NA USTAWI WA JAMII KUHUSIANA NA TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA HAKI NA USTAWI WA WATOTO KWA MWAKA 2013/2014 NA MAADHIMISHO YA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA YANAYOFANYIKA KILA MWAKA IFIKAPO TAREHE 16 JUNI.

Mheshimiwa Spika,
Kila sifa njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu aliyetujaalia afya na uzima na kutuwezesha wajumbe wa Baraza lako Tukufu kuendelea kutekeleza majukumu tuliokabidhiwa; kwa niaba ya wananchi tunaowawakilisha kupitia nafasi mbali mbali katika Baraza lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwako, kwa kunipa nafasi hii ya  kuwasilisha maoni ya Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii, kuhusiana na Taarifa ya Utekelezaji wa Haki na Ustawi wa Watoto kwa mwaka 2013/2014 iliyowasilishwa na Mhe. Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa jamii, Vijana, Wanawake na Watoto.
Mheshimiwa Spika,
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii, inaunga mkono taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Waziri, ambayo ilikusanya mambo muhimu yanayoelekeza katika kuendeleza ustawi na upatikanaji wa haki za watoto. Pia  inayoonesha namna gani nchi yetu inavyochukua jitihada kupitia Wizara zake mbali mbali katika kuyafanyia kazi mapendekezo na maazimio yaliyotolewa na Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika n.k ili kuhakikisha kuwa, utekelezaji wa mipango ya Wizara hizo inazingatia maazimio hayo kwa lengo la kuleta ustawi na upatikanaji wa haki za watoto katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Licha ya Kamati yangu kuunga mkono taarifa iliyowasilishwa na Mhe.Waziri lakini Kamati imegundua kuwa, katika taarifa hiyo kumekosekana uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji kwa mwaka uliopita wa 2012/2013 ambapo imekuwa ni vigumu kwa wajumbe wa Baraza lako tukufu, wasikilizaji au wasomaji wengine wa taarifa hiyo kuweza kufahamu na kulingalisha hatua zilizofikiwa za utekelezaji wa haki na ustawi kwa mwaka uliotangulia na muelekeo wa mwaka ujao. Hivyo Kamati inaishauri Wizara, pindi itakapokuwa inawasilisha taarifa ya utekelezaji katika Baraza lako tukufu, ni vyema ikazingatia kuingiza taarifa ya utekelezaji wa mwaka uliotangulia ili iwe rahisi kwa wajumbe wa Baraza, wasikilizaji na wasomaji wengine kuweza kulingalisha hatua zilizofikiwa za utekelezaji wa haki na ustawi wa watoto.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya Utangulizi huo napenda kuchukua fursa hii kwa kuwatambua wajumbe wa Kamati pamoja na makatibu wake kama hivi ifuatavyo:-
  1. Mhe. Mgeni Hassan Juma                                               Mwenyekiti
  2. Mhe. Hassan Hamad Omar                                            M/Mwenyekiti
  3. Mhe. Ali Salum Haji                                                           Mjumbe
  4. Mhe. Abdi Mosi Kombo                                                   Mjumbe
  5. Mhe. Farida Amour Mohamed                                      Mjumbe
  6. Mhe. Mwanaid Kassim Mussa                                        Mjumbe
  7. Mhe. Mohamed Mbwana Hamad                               Mjumbe
  8. Ndg. Maryam Rashid Ali                                                  Katibu
  9. Ndg. Asha Said Mohamed                                             Katibu
Mheshimiwa Spika,
Siku ya Mtoto wa Afrika ni siku muhimu ambayo inaadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 16 Juni na katika siku hiijamii inapata fursa ya kufahamu hatua zilizofikiwa na Wizara katika kutekeleza haki za watoto na hatua zilizopendekezwa kuchukuliwa kwa nia ya kuimarisha huduma zinazolenga watoto pamoja na kuimarisha mashirikiano baina ya wazazi, walezi, sekta zinazohudumia mama na mtoto pamoja na washirika wa  maendeleo.
Mheshimiwa Spika,
Maoni ya Kamati yangu yatagusa maeneo mbali mbali yanayohusiana na Wizara hii ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo ya taarifa iliyowasilishwa na Mhe. Waziri na Kamati itatoa ushauri kwa Serikali, Wizara na Jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika
KINGA DHIDI YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA WATOTO.
Itakumbukwa kuwa, katika kikao cha Disemba cha 2013, Mhe Mwenyekiti wa Kamati hii, Mgeni Hassana Juma aliwasilisha hoja binafsi inayohusiana na kutoa Maazimio Dhidi ya Vitendo vya Udhalilishaji wa Watoto na Wanawake Zanzibar ambapo hoja hiyo ilitolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 27(1)(n), 27(3), 49(1) na Kanuni ya 50 ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi toleo la 2012).
Mheshimiwa Spika,
Katika hoja hiyo kulikuwa kuna mambo ya msingi ambayo yalihitaji kushughulikiwa kwa haraka na miongoni mwa mambo hayo ni kuitaka Serikali kuanzisha mkakati wa Kitaifa wa Kupambana na kutokomeza udhalilishaji wa watoto utakaojumuisha wawakilishi kutoka makundi mbali mbali na pia Serikali iweke kipaumbele katika bajeti zake kuanzia bajeti ya mwaka 2014/15 na bajeti zinazofuata juu ya kupambana na kutokomeza udhalilishaji wa watoto. Hivyo Kamati inaitaka Serikali kutoa tamko juu ya hatua iliyofikiwa katika hoja hiyo kwani Serikali haijaleta tamko lolote katika Baraza lako tukufu tokea kupitishwa kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa Spika,
MALALAMIKO YA VITENDO VYA UDHALILISHAJI WA WATOTO NA NAMNA KESI ZINAVYOSHUGHULIKIWA.
Kamati imekuwa ikishuhudia jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na Wizara hii, katika kupinga vitendo vya udhalilishaji wa watoto kwa  kuanzishwa  kwa Vituo vya Mkono kwa Mkono Unguja na Pemba, Kamati za Shehia za Kupinga vitendo vya udhalilishaji n.k. Kamati inaipongeza Wizara na inaziunga mkono jitihada hizo lakini kwa upande mwengine Kamati yangu imekuwa inasikitishwa sana na uchache wa kesi zinazohukumiwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kipindi cha Julai 2013 hadi Machi 2014, jumla ya malalamiko 2,337  (Unguja 2,239 na Pemba 98) yameripotiwa katika vituo vya Mkono kwa Mkono lakini katika malalamiko hayo, 87 tu ndio yaliyowasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka. Kamati imebaini kuwa idadi hiyo ni ndogo sana ukilinganisha na malalamiko yaliyopo huku waathirika wakubwa katika vitendo hivyo wakiwa ni watoto wenye ulemavu hasa hasa wenye ulemavu wa akili. Hivyo Kamati inaiomba Serikali kuangalia kuna matatizo gani yanayopelekea kukwamisha kesi hata ikawa kuna kesi chache tu ambazo zinasilishwa mahakamani na baadae kuchukua hatua za haraka ili kuondoa mrundikano wa kesi za watoto mahakamani. Kufanya hivyo kutapelekea watoto kupatiwa haki yao ya msingi ya kuishi na kuhifadhiwa kutokana na vitendo vya udhalilishaji.

Mheshimiwa Spika,
KUHUSU MISAADA NA USTAWI WA WATOTO
Kamati inaipongeza Wizara kupitia Idara ya Ustawi wa Jamii kufanya zoezi la  utambuzi  kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi katika Wilaya 5  za Unguja (Mjini, Kati, Kusini, Kaskazini A na Kaskazini B) na Wilaya 3 za Pemba (Mkoani, Chake Chake na Micheweni) na kubaini kuwa, kuna watoto wapatao 698 (332 wanawake na 366 wanaume) wanaoishi katika mazingira magumu zaidi.
 Mheshimiwa Spika,
 Kamati yetu inatambua kuwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi wanahitaji kusaidiwa lakini ukweli ni kuwa Wizara haijatengewa bajeti maalum na ya kutosha  kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi. Hivyo Kamati inatoa wito kwa Serikali kutenga bajeti maalum kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu zaidi, kuzingatia masuala ya watoto katika mipango na bajeti na pia kuitaka jamii kuchukua jukumu la kuwahudumia watoto wao na kusaidia familia ambazo zinaishi katika mazingira magumu kwa wale wenye uwezo wa kufanya hivyo.
KUHUSU MAENDELEO YA ELIMU KWA WATOTO ZANZIBAR.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imekuwa ikishuhudia juhudi za Serikali katika kuwapatia elimu wa watoto wetu, kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali imekuwa ikijitahidi kuboresha elimu ya Maandalizi na kuifanya kuwa ni elimu ya lazima ili kuwapatia watoto wetu msingi bora kabla ya kujiunga na elimu ya Msingi, aidha ni imani ya Kamati yangu kuwa ile program ya ECD (Early childhood development) itaanza kufanya kazi kwa mashirikiano ya wizara tatu zinazohusika ambazo ni pamoja na Wizara ya Elimu, Wizara ya kilimo na Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto ambapo katika program hii itajumuisha elimu ya makuzi ya awali ya mtoto ambayo itajumuisha masuala ya lishe bora katika kumjenga mtoto katika ukuaji wake kiakili na kimaadili ambao utasaidia ufahamu wa mtoto katika maendeleo yake ya elimu.
Mheshimiwa Spika,
Aidha Katika kuboresha maendeleo ya elimu kwa watoto katika nchi yetu Serikali kupitia Wizara ya elimu katika bajeti ya mwaka 2014/2015 imeazimia kuanzisha mradi wa kuwapatia chakula wanafunzi wa Skuli za maandalizi, Kamati inaunga mkono azma hii ya Serikali na inachukua fursa hii kuwashajihisha wananchi kuzallisha kwa wingi mazao ambayo yatatumika katika kuwapatia chakula watoto katika maeneo yao mazao hayo ni pamoja na mahindi mtama, viazi vitamu nk ili kuunga mkono juhudi za Serikali yetu.
KUHUSU USHIRIKISHWAJI WA WATOTO KATIKA MASUALA MBALI MBALI.
Mhe. Spika,
Miongoni mwa haki muhimu ya mtoto ni kushirikishwa katika mambo mbali mbali yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana,Wanawake na Watoto kwa muda mrefu sasa imekuwa ikiendelea kuanzisha na kuyaendeleza mabaraza ya watoto katika ngazi za Shehia na Wilaya. Hivi sasa kuna mabaraza ya watoto ya Wilaya matatu (3), mawili (2) Unguja na moja (1) Pemba na mabaraza ya Shehia 218 (Unguja 139 na Pemba 79) ambapo kupitia mabaraza hayo watoto hupata fursa ya kubadilishana mawazo na kushiriki katika shughuli mbali mbali za kijamii. Aidha kupitia mabaraza hayo mafunzo mbali mbali yamekuwa yakitolewa kwa watoto juu ya kufahamu haki zao na jinsi ya kujithamini na kujilinda.


Mheshimiwa Spika,
Mwisho nachukua tena nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi hii kuwasilisha maoni ya Kamati juu ya Hotuba ya siku ya mtoto duniani 2014, aidha napenda kumshukuru Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana, Wanawake na Watoto pamoja na watendaji wake wote kwa mashirikano yao makubwa wanayotupatia.
Mhe. Spika,
Baada ya kuyasema hayo kwa naiba ya Kamati yangu naomba kuwasilisha.


Ahsante,

………………………….
Mgeni Hassan Juma,
Mwenyekiti,
Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii,
Baraza la Wawakilishi,

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>