Na Hassan Hamad, OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad ameonya kuwa vitendo vya hujuma dhidi ya raia na wageni, vinaweza kuathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa Zanzibar.
Amesema Zanzibar ambayo imekuwa ikitegemea zaidi sekta ya Utalii kuendeleza uchumi wake na kukuza pato la taifa, imekuwa ikiguswa na matukio hayo ya hujuma, na kwamba yanaathiri uchumi, ustawi wa jamii na sifa ya ukarimu kwa Zanzibar.
Mhe. Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika mahojiano maalum na kituo cha televisheni cha ITV, Mikocheni Dar es Salaam.
Amesema katika kukabiliana na vitendo hivyo, serikali inakusudia kutekeleza mpango wake wa kuweka kamera za CCTV katika maeneo muhimu ya utalii likiwemo eneo la Mji Mkongwe, ili kuweza kuwabaini kwa urahisi wahusika wanafanya vitendo hivyo.
Kuhusu zao la karafuu kwa maendeleo ya uchumi wa Zanzibar, Maalim Seif amesema serikali imefanikiwa kudhibiti magendo ya karafuu baada ya kuongeza bei ya zao hilo na kuwashinda wanunuzi wengine wa Afrika Mashariki ambako karafuu hizo zilikua zikipelekwa.
Aidha amesema katika kuhakikisha kuwa ubora wa karafuu za Zanzibar unalindwa na kudhibiti wauzaji wengine, Serikali kupitia Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, itaweka nembo maalum “brand”, kuweza kuzitofautisha karafuu za Zanzibar na maeneo mengine.
Akizungumzia dawa za kulevya, Maalim Seif ambaye ofisi yake ndiyo inayohusika na udhibiti wa dawa hizo, amesema bado kuna kazi kubwa ya kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa hizo kutokana na jiografia ya visiwa vya Zanzibar.
Amefahamisha kuwa vita hiyo pia ni ngumu kutokana na uwezo mkubwa wa wafanyabiashara wa dawa hizo ambao wanaweza kuwarubuni watendaji kwa pesa nyingi na kuacha kutekeleza wajibu wao.
Amesema katika kupiga vita dawa hizo, ni lazima kuwepo na mashirikiano pamoja na uadilifu miongoni mwa watendaji, hasa wale wanaofanya kazi katika viwanja vya ndege, bandarini na vyombo vya ulinzi.
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, amesema Serikali ya Umoja wa Kitaifa GNU itaendelea kuwepo hata baada ya uchuguzi mkuu wa mwaka 2015, kwa vile suala hilo ni la kikatiba na limewekewa misingi maalum.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Maalim Seif amesema bado serikali ina jukumu la kuhakikisha kuwa katiba mpya inapatikana, ili kuendeza ustawi wa Taifa na kukidhi mahitaji ya wananchi.
Amesema tayari serikali imeshatumia fedha nyingi za wananchi, na kwamba kushindwa kukamilisha mchakato huo kwa wakati, itakuwa ni hasara kwa serikali na taifa kwa ujumla.
Hivyo amesema hakuna budi kwa serikali kutafuta njia mbadala za mazungumzo, kuhakikisha kuwa mchakato huo unaendelea na unafanikiwa kwa maslahi ya Taifa.