Hakuna huduma za maji, wananchi wajisaidia fukweni
Na Mwandishi wetu
Na Mwandishi wetu
Uharibifu mkubwa wa mazingira umezikumba fukwe zote ambazo zinafanywa biashara ya upikaji na uanikija dagaa hasa maeneo ya kaskazini Unguja na eneo la Maruhubi mkoa wa mjini magharibi.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa maeneo ya Fungu refu Mto wa Pwani, Bwekunduni, Muwanda na eneo la Maruhubi kwa kiasi kikubwa kumekuwa na uharibifu wa mazingira unaotokana na kumwaga maji ya moto ya kuchemshia dagaa na hata mabaki ya dagaa waliooza.
Sambamba na hilo l pia imebainika kukatwa kwa mikoko mingi ili kutoa nafasi ya uanikaji wa dagaa katika maeneo hayo.
Aidha mashamba kadhaa ya maeneo ya Bwekunduni na Mto wa pwani yamevamiwa na maji chumvi baada ya kukatwa mikoko hiyo.
Mbali na hayo,gazeti hili pia limebaini kuwa hakuna huduma za vyoo katika maeneo ya bishara hizo jambo ambalo linasababisha watu wanaojishughulisha na biashara hiyo, kujisaidia pembeni mwa fukwe au sehemu za mikoko.
Pia katika eneo hilo kumekosekana maji safi na salama na kusababisha wanaoishi maeneo hayo kutumia maji ya kuokota.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakulima wa Mto wa pwani,eneo la Fungurefu kwa masharti ya kutotajwa majina yao waliliambia gazeti hili kuwa eneo kubwa la mashamba limevamiwa na maji chumvi na hivyo kusitisha shughuli za kilimo.
“Kwa kweli nilikuwa nalima, mpunga viazi vitamu lakini kwa sasa nusu ya shamba langu limevamiwa na maji ya chumvi”, alisema.
Aidha alisema wakulima wanaolima karibu na eneo hilo wamekuwa hawapati mavuno mazuri kutokana na kuingiliana na maji chumvi.
Akizungumza na gazeti hili, Katibu wa Kamati ya Mazingira ya Mkoa wa Kaskazini Unguja (MECA), Hadia Ali Makame, alikiri kuwepo kwa uchafuzi wa mazingira na kwamba taratibu zote za kuiarifa Idara husika zimefanywa lakini hakuna hatua iliyochukuliwa.
Aidha alisema k baada ya kuona hali mbaya katika eneo hilo walilazimika kupanda mikoko ili kurejesha uhalisia wake lakini wamevunjika moyo kutokana na miti yote kuhujumiwa.
Nae Msimamizi wa eneo hilo, Kaite Mwadini Haji, alisema hakuna uharibifu wa mazingira katika eneo hilo lakini alibainisha kukosekana kwa huduma za kijamii ikiwa ni pamoja na vyoo na maji safi na salama.
“Tunajaribu kudhibiti mazingira sana lakini nikiri kuwa watu wanajisaidia katika mikoko na maji safi hayapo mpaka tununue barabarani,” alisema.
Aidha mmoja wa waanikaji wa madagaa, Asha Nuru, alisema serikali lazima iwawekee mazingira mazuri kwani wamekuwa wakipata shida ya vyoo na maji.
Pia Fatma Ali na Mtumwa Ali, ambao wameajiriwa kwa ajili ya kazi ya kupika dagaa katika eneo la Maruhubi walikiri kuwa maji ya kuchemshia dagaa wanalazimika kumwaga maeneo yoyote tu kwa kuwa hakuna udhibiti wa mazingira sambamba na kwenda haja kubwa na ndogo.
Mkuu wa Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Riziki Juma Simai, alikiri kuwepo kwa uharibifu mkubwa wa mazingira katika eneo la Mto wa pwani fungu refu.
“Tayari tumekutana na wavuvi, matajiri, wapikaji na waanikaji wa madagaa wa maeneo yote na kukubaliana kupunguza eneo hilo utaratibu ambao kwa sasa uko mbioni na utakamilika hivi karibuni,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira, Sheha Mjaja, alikiri uharibifu huo na kwamba walifanya ziara ya makusudi katika maeneo yote ya uanikaji wa madagaa.