Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Balozi Seif afungua maonyesho ya 38 ya biashara ya kimataifa

$
0
0
Na Othman Khamis Ame, OMPR
 
Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania inakusudia kuongeza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Viwanda ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoelekeza azma ya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati na unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
 
Matumaini ya kufikiwa kwa malengo hayo yaliyowekwa na Serikali yatatokana na kuimarika kwa uzalishaji pamoja na uwekezaji katika viwanda vya msingi.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati akiyafungua maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya saba saba vya Mwalimu J. K. Nyerere Jijini Dar es salaam.
 
Balozi Seif alisema  juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii zinaendelea kuonesha mafanikio kutokana na kukua kwa pato la Taifa kutoka asilimia 6.4 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka 2013. 
 
Alisema  kiasi hiki cha ukuaji wa uchumi kimeiwezesha Tanzania kuongoza kwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika { SADC }  zilizokua kwa wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2012 na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilizokua kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2012.
 
Balozi Seif alifahamisha kwamba kwa Tanzania, ukuaji wa Sekta ya Viwanda umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 1998 hadi asilimia 7.7 mwaka 2013, wakati sekta ya kilimo inakua kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mwaka.
 
“ Ukuaji huu umechangiwa kwa kiwango kikubwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani, hususan viwanda vya vinywaji, saruji, bidhaa za chuma na usindikaji wa mazao ya kilimo “. Alifafanua Balozi Seif.
 
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema kwamba  mwenendo wa mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kwa kipindi rejea umeongezeka kwa asilimia kutoka asilimia 8.37 mwaka 1998 hadi asilimia 9.92 mwaka 2013.
 
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {TanTrade} kwa mpango wake wa kuwekeza katika miundombinu mipya ya kisasa ya maonesho unaokwenda sambamba na mahitaji ya nafasi ya kuoneshea. 
 
“ Nimefahamishwa kuwa idadi ya washiriki wote wa ndani na nje ya nchi imeongezeka kutoka makampuni ya ndani 1,601 mwaka 2013 kufikia makampuni 1,690 mwaka 2014, na makampuni kutoka nje 460 mwaka 2013 hadi 490 mwaka huu wa 2014 “. Alisema Balozi Seif.
 
Alisisitiza kuwa Ongezeko hili ni ishara inayoonyesha kwamba  maonesho hayo ya saba saba  yanakidhi viwango vya kimataifa na kudhihirisha kwamba yanaendelea kupata umaarufu. hivyo sasa ni kipindi muafaka kwa wazalishaji wazalendo kutangaza bidhaa zao kwa walaji wa ndani na nje ya nchi.
 
Balozi Seif alitoa wito kwa waandaaji kutumia maonesho hayo kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini kwa lengo la kuvutia wawekezaji kutembelea Maonesho haya kwa nia ya kujionea fursa hizo na hatimaye kupata ushawishi wa kuwekeza miradi yao.
 
Nimefahamishwa kuwa katika maonesho haya kuna nchi ambazo zinashiriki.  Aliwashauri washiriki wa ndani kwenye maonyesho hayo ya saba saba kutenga muda wa kutembelea mabanda na makampuni ya nchi wanachama wa EAC na SADCkuzungumza nao kwa ajili ya kujifunza.
 
Alisema hatua hiyo wapa muda wa kutengeneza mtandao wa pamoja ambao utawasaidia kutangaza bidhaa zao katika masoko hayo ya Kikanda na baadaye kuwa na nguvu za pamoja kwenda kwenye masoko makubwa ya Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Asia.
 
B kalozi Seif aliwaasa wale wote watakaopata oda wazifanyie  kazi ili malengo yao ya sasa na yale ya muda mrefu yaweze kutimia.
 
Zingatieni kuwa mmetumia muda mwingi na rasilimali nyingi katika maandalizi, hivyo ni vyema juhudi zenu hizi zikawa zenye manufaa endelevu.  Epukeni urasimu usiokuwa na faida, kwani urasimu siku zote unarefusha mchakato na kufikia makubaliano ya kibiashara “. Balozi Seif liwatahadharisha washiriki hao wa Maonyesho ya saba saba dar.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aidha aliushukuru Uongozi wa  Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {Tan-Trade} kwa ubunifu wao wa kuanzisha maonesho maalum yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka yakiwemo Tamasha la Biashara, Maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Maonesho ya Bidhaa za Utamaduni na Uhuru.
 
Balozi Seif alielezea matumaini kwamba Mamlaka hiyo itaendelea kuanzisha maonesho mengine kama hayo katika Mikoa mengine hapa nchini ili kuhakikisha maonesho ya Biashara yanatumika kikamilifu kama chombo cha kukuza biashara kwa nchi nzima.
 
Mapema Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Abdulla Kigoda aliwashukuru washirika wa maendeleo pamoja na Wananchi kwa ushiriki wao uliosaidia kufanikisha maonyesho hayo.
Mh. Kigoda alisema Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania{ Tan Trade } itaendelea kuimarisha  miundo mbinu itakayotoa fursa kwa mikoa mbali mbali NchininTanzania kufanya maonyesho ya biashara kila mwaka.
 
Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara ya SMT imeandaa mpango maalum wa uwekezaji katika eneo hilo muhimu la maonyesho linalochangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa Taifa.
 
Waziri wa Viwanda na Biashara Mh. Kigoda alifahamisha kwamba utafiti uliofanywa na Taasisi za uchumi Kimataifa zimethibitisha kwamba maonyesho ni ni nyenzo inayoongoza katika kukuza uchumi na utoaji wa huduma muhimu za kijamii.
 
Washiriki wapatao 1,690 kutoka makampuni mbali mbali ya ndani na nje ya nchi wamehudhuria maonyesho hayo ya 38 ya Kimataifa  mwaka huu  idadi ambayo imeongezeka zaidi ikilinganishwa na makampuni 1,601  yaliyoshiriki mwaka jana.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>