HOTUBA YA MHE. BALOZI SEIF ALI IDD, MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, WAKATI WA UFUNGUZI WA MAONESHO YA 38 YA BIASHARA YA KIMATAIFA YA DAR ES SALAAM, 2 JULAI, 2014
Mhe. Dkt. Abdallah Kigoda (Mb), Waziri wa Viwanda na Biashara,
Waheshimiwa Mawaziri,
Mhe. Raymond Mushi, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa,
Waheshimiwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar,
Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara, Bwana Uledi A. Mussa,
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Bibi Sabetha Mwambenja,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania, Bibi Jacqueline Mneney Maleko,
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama vya Siasa nchini,
Ndugu Wanahabari,
Washiriki wa Maonyesho,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana hapa tukiwa wazima na wenye furaha, kushuhudia ufunguzi rasmi wa maonyesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam. Aidha, napenda kuchukua fursa hii adhimu kuishukuru kwa dhati Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania – Tan Trade kwa heshima mliyonipa ya kuwa mgeni rasmi.
Waswahili wanasema “mcheza kwao hutunzwa”. Kwa hivyo, sina budi nami kuitunza kwa pongezi Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko ya Zanzibar pamoja na Taasisi mbali mbali za Serikali na sekta binafsi kwa kushiriki kwao ili kufanikisha maonesho haya.
Kwa namna ya pekee pia niwashukuru wageni waalikwa, Washiriki wa Maonesho haya pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kuitikia wito wa kushiriki na kutembelea Maonesho haya makubwa, ambayo yanafanyika kila mwaka. Nawapongeza waandaaji wa maonyesho haya ya sabasaba kuwa endelevu. Kauli Mbiu ya maonesho ya mwaka huu ni “Unganisha Uzalishaji na Masoko”. Kauli mbiu hiiinawataka wazalishaji wa mazao na bidhaa kutoa kipaumbele kwa mahitaji ya soko ikiwa ni pamoja na kujitangaza.
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa,
Nimefahamishwa kuwa idadi ya washiriki wote wa ndani na nje ya nchi imeongezeka kutoka makampuni ya ndani 1,601 mwaka 2013 kufikia makampuni 1,690 mwaka 2014, na makampuni kutoka nje 460 mwaka 2013 hadi 490 mwaka huu wa 2014. Ongezeko hili ni ishara kuwa maonesho haya yanakidhi viwango vya kimataifa na hivyo ni kipindi muafaka kwa wazalishaji wetu kutangaza bidhaa kwa walaji wa ndani na nje. Ongezeko hili la washiriki, linadhihirisha ni kwa kiasi gani maonyesho yameendelea kuwa maarufu ndani na nje ya nchi.
Ni matarajio yangu kuwa maonesho haya yataendelea kuwa maarufu na jukwaa kubwa kupita yote katika nchi za Afrika Mashariki na Kati la kutangaza biashara kwa bidhaa na huduma. Natoa wito kwa waandaaji kutumia maonesho haya kutangaza pia fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini na hivyo kuvutia pia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutembelea Maonesho haya kwa nia ya kujionea fursa hizo na hatimaye kuwekeza. Nawapongeza pia TanTrade kwa mpango wa kuwekeza katika miundombinu mipya ya kisasa ya maonesho unaokwenda sambamba na mahitaji ya nafasi ya kuoneshea. Suala la msingi hapa ni kupanga mradi huu wa ujenzi uwe kwa awamu ili kuhakikisha maonesho yanaendelea wakati wote wa ujenzi bila kuleta usumbufu kwa waoneshaji.
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa,
Umuhimu wa kuendeleza maonesho kama fursa ya kutangaza na kutafuta masoko ya bidhaa unatokana na ongezeko la ushindani katika uzalishaji wa bidhaa za kilimo na bidhaa za viwandani ndani na nje ya nchi. Kwa Tanzania, ukuaji wa Sekta ya Viwanda umeongezeka kutoka asilimia 5.5 mwaka 1998 hadi asilimia 7.7 mwaka 2013, wakati sekta ya kilimo inakua kwa wastani wa asilimia 4.5 kwa mwaka.
Ukuaji huu umechangiwa kwa kiwango kikubwa na kuimarika kwa uzalishaji viwandani, hususan viwanda vya vinywaji, saruji, bidhaa za chuma na usindikaji wa mazao ya kilimo. Aidha, mwenendo wa mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kwa kipindi rejea umeongezeka kwa asilimia kutoka asilimia 8.37 mwaka 1998 hadi asilimia 9.92 mwaka 2013.
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa,
Moja ya bidhaa za Tanzania ambazo zimekuwa zikivutia watu wengi kwenye maonesho haya ni bidhaa za ngozi. Hii inatokana na jitihada za Serikali ikishirikiana na sekta binafsi ambapo Mkakati wa Kufufua na Kuendeleza Sekta na Viwanda vya Ngozi nchini umeendelea kutekelezwa na kwa sasa Sekta Ndogo ya Usindikaji wa Ngozi imeongeza viwanda kutoka vitatu (3) vya awali hadi viwanda tisa (9) mwaka 2013/2014. Viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa (installed capacity) wa kusindika vipande vya ngozi milioni 13.2 kwa mwaka kufikia hatua ya awali (wetblue). Uwekezaji katika viwanda vilivyo chini ya Maeneo Maalum ya Kuzalisha Bidhaa za Kuuza Nje (Export Processing Zones- EPZ) na Maeneo Maalum ya Uwekezaji Kiuchumi (Special Economic Zones-SEZ) nao vile vile umechangia katika ukuaji wa sekta ya viwanda. Mathalani, katika mwaka 2013/2014, makampuni 31 yamepewa leseni za kujenga viwanda chini ya Mamlaka ya EPZ na makampuni 8 yameanza uzalishaji. Makampuni hayo yanatarajia kuwekeza mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 458 na kuajiri watu 10,276. Idadi hiyo inafanya jumla ya makampuni yanayozalisha chini ya SEZ na EPZ kufikia 98, jumla ya mtaji uliowekezwa kufikia Dola za Marekani Bilioni 1.5 na jumla ya ajira za moja kwa moja kufikia 27,000.
Ndugu Wananchi,
Serikali inakusudia kuongeza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Viwanda ili kuakisi malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo inayoelekeza azma ya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati na unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025. Matumaini ya kufikiwa kwa malengo tuliyojiwekea yanatokana na kuimarika kwa uzalishaji na uwekezaji katika viwanda vya msingi.
Aidha, juhudi za Serikali katika kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii zinaendelea kuonesha mafanikio. Pato la Taifa limeendelea kukua kutoka asilimia 6.4 mwaka 2011 kufikia asilimia 7.1 mwaka 2013. Kwa kiasi hiki cha ukuaji Tanzania inaongoza kwa nchi za SADC zilizokua kwa wastani wa asilimia 4.3 mwaka 2012 na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zilizokua kwa wastani wa asilimia 5.1 mwaka 2012.
Kasi nzuri ya ukuaji wa Pato la Taifa ilichangiwa pia na sekta zinazokua kwa haraka na zenye mtaji mkubwa hususan sekta ya mawasiliano iliyoongoza kwa ukuaji wa asilimia 20.6 kwa mwaka 2013, sekta ya huduma ya fedha asilimia 13.2, ujenzi, madini asilimia 7.8, biashara asilimia 7.7 na uchukuzi asilimia 7.1.
Hata hivyo, sekta ya kilimo ambayo inayoajiri watu wengi zaidi imekua kwa kiwango cha asilimia 4.3 kwa mwaka 2013. Pamoja na ukuaji mdogo wa sekta hii, mchango wake kwa Pato la Taifa bado ungali mkubwa. Mathalani, mwaka 2013, sekta hii ilichangia asilimia 24.7 ya pato hilo na asilimia 10.7 ya mapato ya fedha za nje.
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa,
Kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka 5 (2011/12 – 2015/16), malengo yetu ni ukuaji wa wastani wa asilimia 8 wa Pato la Taifa. Ili tufikie huko, Serikali yetu kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 ilianzisha Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now). Mpango huu unalenga maeneo ya kipaumbele katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka 5 ambayo ni Miundombinu, Kilimo, Maendeleo ya Viwanda, Rasilimali Watu, Utalii, Biashara na Huduma za fedha. Ni matumaini yangu kuwa tutaanza kuona matokeo makubwa katika sekta za uchumi kutokana na ukuaji wa sekta ya biashara ya ndani na nje.
Ndugu Washiriki na Wageni Waalikwa,
Ukuaji wa sekta ya biashara unategemea mifumo ya soko la ndani pamoja na mikakati ya kuyafikia masoko ya nchi jirani. Hivyo, ili kunufaika na fursa za masoko zilizoko katika nchi jirani ni muhimu kutangaza na kuuza bidhaa zetu katika masoko hayo.
Nchi jirani ambazo pia ni Wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na SADC zimeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kuondoa vikwazo visivyokuwa vya lazima na hivyo biashara baina ya nchi yetu na nchi hizo imeongezeka. Napenda niipongeze Serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kurahisisha biashara za mipakani kwa kuanzisha Kamati za Pamoja za Mipakani na kujenga majengo yatakayowezesha ukaguzi wa mipakani kufanyika kwa pamoja.
Nimefahamishwa kuwa katika maonesho haya kuna nchi wanachama wa EAC na SADC ambazo zinashiriki. Nawashauri washiriki wa ndani mtenge muda kutembelea mabanda na makampuni ya nchi hizi, muongee nao kwa ajili ya kujifunza na kutengeneza mtandao wa pamoja ambao utawasaidia kutangaza bidhaa zenu katika masoko haya ya Kikanda na baadaye muweke nguvu ya pamoja kwenda kwenye masoko makubwa ya Ulaya, Marekani, Mashariki ya Kati na Asia.
Naomba nitumie pia fursa hii kuwaasa wote mtakaopata oda, zifanyieni kazi ili malengo yenu ya sasa na ya muda mrefu yaweze kutimia. Zingatieni kuwa mmetumia muda mwingi na rasilimali nyingi katika maandalizi, hivyo ni vyema juhudi zenu hizi zikawa zenye manufaa endelevu. Epukeni urasimu usiokuwa na faida, kwani urasimu siku zote unarefusha mchakato na kufikia makubaliano ya kibiashara bila ya sababu.
Naomba pia niwapongeze Tan-Trade kwa kuwa wabunifu kwa kuanzisha maonesho maalum yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka yakiwemo Tamasha la Biashara, Maadhimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Maonesho ya Bidhaa za Utamaduni na Uhuru. Natumaini mtaendelea kuanzisha maonesho mengine kama haya kwenye Mikoa mingine hapa nchini ili kuhakikisha maonesho ya Biashara yanatumika kikamilifu kama chombo cha kukuza biashara kwa nchi nzima. Ni muhimu pia msimamie kikamilifu jukumu la kusimamia uandaaji wa Maonesho ya Kimataifa ili kuhakikisha kuwa Maonesho yote yanakidhi vigezo na masharti yaliyowekwa na Serikali.
Kwa kutambua mchango wa biashara katika uchumi wa nchi yetu, Serikali kupitia Wizara na Taasisi zake husika itaendelea kuunga mkono juhudi za sekta binafsi kwa kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Ndugu Wananchi,
Mwisho, napenda kwa mara nyingine kuushukuru uongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na ule wa Tan-Trade kwa kuandaa maonyesho haya ambayo yamefana sana. Najua kuwa wamefanya kazi usiku na mchana ili kuyafanikisha maonyesho haya. Nawapongeza sana.
Lakini pia naupongeza uongozi huo kwa heshima hii adhim walionipa ya kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonesho haya. Heshima niliyopewa kwa mara ya pili, nitaendelea kuitunza, kuienzi na kuithamini siku zote.
Mabibi na Mabwana,
Baada ya kuyasema hayo, napenda kutamka kuwa Maonesho ya 38 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam sasa yamefunguliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.