Quantcast
Channel: ZanziNews
Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Dkt Bilal afanya mazungumzo na Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza

$
0
0
 




Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Rais wa Burundi Mhe. P. Nkurunziza alipomtembelea Ofisini kwake Ikulu jijini Bujumbura jana Julai 02-2014.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na waandishi wa Habari wa Vyombo mbalimbali vya Burundi Ikulu jijini Bujumbura jana ambapo alizungumzia kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya Nchi mbili hizi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na baadhi ya  Viongozi wa Serikali ya Burundi kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura jana baada ya kuhudhuria maadhimisho ya miaka 52 ya Uhuru wa nchi hiyo.      (Picha na OMR)
 
Julai 02, 2014: Bujumbura
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal, leo Jumatano Julai Pili, 2014 amekutana na Rais wa Burundi Mheshimiwa Pierre Nkurunzinza na kufanya naye mazungumzo. Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ya Rais Nkurunzinza iliyopo katikati ya jiji la Bujumbura.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walipata fursa ya kubadilishana mawazo kuhusu uhusiano baina ya Tanzania na Burundi ambapo Mheshimiwa Makamu wa Rais alitumia nafasi hiyo kumpongeza Rais Nkurunzinza na watu wa Burundi kwa sherehe zilizofana za kutimiza miaka 52 ya uhuru. Pia alitumia nafasi hiyo kumtakia kila la heri Mheshimiwa Rais Nkurunzinza pamoja na  watu wa Burundi kufuatia kupiga hatua kubwa za kimaendeleo sambamba na kuweza kuwafanya wananchi wa Burundi kuwa wamoja.
Pia alimueleza Rais Nkurunzinza kuhusu umuhimu wa kuzidi kuifanya Burundi kuwa nchi moja kwa kuwaunganisha watu wake na akaeleza kuwa, Tanzania inafurahi kuona hatua kubwa za kimaendeleo zikipigwa nchini Burundi na kwamba ili hatua hizo ziwe madhubuti, upo umuhimu wa kuwafanya wananchi wa Burundi kubakia wamoja na wanaoshirikiana katika kuiendeleza nchi yao.
“Burundi ikifanya vizuri maana yake ni kuwa Afrika Mashariki imefanya vizuri. Tanzania tutafurahi na nchi zote za ukanda wetu zitafurahi,” alisema Mheshimiwa Makamu wa Rais na kuongeza kuwa lengo la Tanzania siku zote ni kuona jirani zake wakiishi kwa utulivu na wakifanya mambo yao ya maendeleo katika hali ya amani.
Katika mazungumzo hayo Rais Nkurunzinza aliendelea kuishukuru Tanzania kwa uhusiano wake wa karibu na Burundi na akaongeza kuwa wananchi wa nchi yake wamefurahishwa sana kwa Tanzania kushiriki katika sherehe za miaka 52 ya Uhuru wa Burundi, sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Prince Louis Rwagasore jana. Pamoja na Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Tanzania, sherehe hizo pia zilihudhuriwa na Makamu wa Rais wa Somalia na Waziri Mkuu wa Chad.
Msafara wa Mheshimiwa Makamu wa Rais umeondoka leo jijini Bujumbura na kurejea jijini Dar es Salaam tayari kabisa kuendelea na majukumu mengine ya kitaifa. Katika msafara huo, Mheshimiwa Makamu wa Rais aliambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Zanzibar, Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim.
 
Imetolewa na:              Ofisi ya Makamu wa Rais
Julai 2, 2014 Bujumbura: Burundi


Viewing all articles
Browse latest Browse all 35043

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>