Na Hasaan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, ameelezea kuridhishwa kwake na uwepo wa vyakula na matunda yenye viwango kwa ajili ya mwezi mtuku wa Ramadhani.
Hata hivyo amesema bei zake bado ziko juu ikilinganishwa na kipato cha wananchi, na kwamba wananchi walio wengi wanashindwa kumudu kununua bidhaa hizo.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo katika ziara yake ya kutembelea masoko mbali mbali ya manispaa ya mji wa Zanzibar, kuangalia hali ya upatikanaji wa bidhaa na matunda, ambayo hutumika sana katika mwezi wa Ramadhan.
Amewashauri wakulima na wafanyabiashara kuzingatia hali za maisha ya wananchi, na kuangalia uwezekano wa kupunguza bei, ili wananchi waweze kumudu kununua bidhaa hizo.
“Sitaki niwambie kuwa wauze kwa hasara, lakini wapunguze kuingiza faida nyingi ili kila mwananchi aweze kumudu kununua, na wakifanya hivyo inaweza kuwa sadaka nzuri kwao katika mwezi huu wa Ramadhan”, alisisitiza Maalim Seif na kuongeza,
“Nashkuru katika bidhaa nilizoziona ziko katika kiwango cha kuridhisha, na sijaona dalili ya ndizi au matunda mengine yaliyochomwa moto”, alisema.
Amesema Serikali imetoa fursa ya soko huria kwa wafanyabiashara, na kwamba upandaji wa bei kwa bidhaa hizo unayokana na wakulima na wafanyabiashara wenyewe.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa vitoweyo, Maalim Seif amesema hali hairidhishi, kwa vile samaki waliopo ni wachache, na hivyo kuuzwa kwa bei ya juu.
Kuhusu uvumi wa kuwepo kampuni inayotaka kuingiza samaki kutoka nje ya Tanzania na kuuzwa kwa bei nafuu, na kuwepo madai kuwa kampuni hiyo imezuiwa na Serikali, Maalim Seif amesema yeye hana taarifa hiyo, lakini ikiwa kuna ukweli wowote inawezekana kuwepo sababu za msingi kwa Wizara inayohusika kufanya hivyo.
Aidha Maalim Seif ameelezea kuridhishwa na maendeleo ya soko la Mombasa ambalo linaendelea kufanyiwa matengenezo makubwa ambayo yatasaidia kutunza hadhi ya soko hilo la matunda.
Hata hivyo ameelezea kutoridhishwa na hali ya usafi katika soko la samaki Malindi, na kuliagiza Baraza la Manispaa kuweka utaratibu mzuri wa kulitunza eneo hilo la kuuzia samaki, ili liwe katika hali ya usafi wakati wote.
Baadhi ya wafanyabiashara wameiomba serikali kuwawekea mazingira bora ya kufanya biashara zao, sambamba na kulalamikia baadhi ya wafanyabiashara waliorejea soko la Mwanakwerekwe baada ya kuhamishiwa katika soko la Mombasa.
Katika ziara hiyo Maalim Seif ametembelea soko la matunda Mombasa, soko Kuu la Mwanakwerekwe, Kituo cha biashara Saateni na Soko Kuu la Darajani.
Wakati huo huo Mhe. Maalim Seif amewatembelea na kuwafariji watoto yatima wanaolelewa na jumuiya ya Muzdalifat katika eneo la Amani mjini Zanzibar.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Sheikh Abdallah Hadhir Abdallah ameishukuru serikali kwa mashirikiano waliyonayo kwa jumuiya hiyo, na kuiomba kuongeza misaada yake ili kuwaendeleza watoto yatima wanaolelewa katika vituo mbali mbali vya Zanzibar.