Khamis Amani na Mwanajuma Mmanga
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeonya kuwa haitakuwa na stahamala wa muhali kwa mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuchezea amani.
Aidha imesema italinda amani ya nchi na wananchi wake kwa gharama yoyote ile.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi alitoa onyo hilo jana wakati akifunga mkutano wa 12 wa Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar.
Alisema Zanzibar haina mgongano wa dini na kwa hivyo serikali haitakubali kuona kiongozi wa dini anafanya mahubiri ya uchochezi yanayoweza kusababisha mifarakano badala ya mshikamano uliopo.
Alisema serikali inalaani mahubiri yoyote ya kichochezi na kwamba haitahofu kulaumiwa kwa hatua itakazochukua dhidi ya wachochezi.
Aliwataka wananchi kutowaunga mkono viongozi wa aina hiyo kwani hawaitakii mema nchi na wanataka kuwarejesha katika hali ya uadui na uhasama miongoni mwa jamii.
Kuhusu kikundi cha watu kinachopita maeneo mbali mbali Unguja na Pemba kuwahoji wananchi kuwa ni wafuasi wa chama gani, alisema serikali haina habari zozote na hilo na wala haijatoa agizo la kufanywa sensa hiyo.
Alikionya kikundi hicho kuacha kufanya hivyo kwa sababu serikali haiendeshi sensa ya aina hiyo na kuwaagiza Masheha kuwalifuatilia suala hilo.
Kuhusu nishati ya umeme, alisema serikali imetoa kipaumbele katika kutafuta chanzo mbadala cha umeme wa uhakika badala ya kutegemea chanzo kimoja.
Alisema serikali inaendelea na utafiti yakinifu wa kupata nishati mbadala na baada ya utafiti huo Zanzibar itapata chanzo chengine cha umeme na hatimae uzalishaji kuanza.
Kuhusu mabadiliko ya katiba mpya, aliwataka wananchi kuendelea kutoa maoni yao kwa uhuru na uwazi bila ya woga.
Kwa upande wa daftari la kudumu la wapiga kura, Balozi Seif alitoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo huku wakikumbuka kudumisha amani na utulivu.
Baraza la Wawakilishi limeahirishwa hadi siku ya Jumatano ya Oktoba 9 mwaka huu, baada ya kumaliza mkutano wake wa bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka wa fedha 2013/2014.