Na Kauthar Abdalla
SHIRIKA la Umeme Zanzibar (ZECO) linaendelea kuchukua hatua za kuimarisha huduma zake ili kuwapunguzia usumbufu wateja wake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Msaidizi Ofisa Uhusiano wa shirika hilo,Haji Juma Chapa, alisema utaratibu ambao ulikuwepo mwanzo umeshapitwa na wakati na shirika linafanya kila jitihada kuhakikisha linarekebisha hitilafu zilizopo ili wananchi wapate huduma bora na kwa wakati.
Akizungumzia ununuzi wa umeme kupitia simu ya mkononi, alisema huduma hiyo haijaanza kutumika kwa sababu taratibu bado hazijakamilika kwa sababu mfumo unaotumika kuuzia umeme umeshapitwa na wakati.
Alisema shirika limeona ipo haja kwa mara ya kwanza kuanza kutoa huduma kwa kutumia mtandao wa Zantel kwa sababu wanannchi wengi wa Zanzibar wanatumia huduma za kampuni hiyo na baadae watafikiria kujiunga na mitandao mengine ya simu.
Aidha alisema kabla ya huduma hiyo kuanza kutumika kutakuwa na kipindi cha majaribio ambapo kuna idadi ya watu watatumiwa kuanza kutumia huduma hiyo kabla ya kuingizwa sokoni.