Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi limeimarisha ulinzi kwenye maeneo ya ibada, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo mengine yote yatakayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu wakati wa sherehe za sikukuu ya Eid el Fitri.
Taarifa ya polisi iliyosainiwa na msemaji wa jeshi hilo, SSP Advera Senso, pia imewataka wananchi kuwa makini na kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uhalifu.
Alisema katika taarifa hiyo kuwa uzoefu unaonesha kuwa baadhi ya watu hutumia kipindi cha sikukuu kama mwanya wa kufanya uhalifu kutokana na mikusanyiko watu.
Alisema polisi kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi limejipanga vizuri kuhakikisha wananchi wanasherekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu, pasipo vitendo ama viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani.
Katika kuhakikisha usalama kwenye kumbi za starehe, aliwataka wamiliki wa kumbi hizo wazingatie uhalali na matumizi ya kumbi zao katika uingizaji wa watu kulingana na uwezo wa kumbi hizo, badala ya kuendekeza tamaa ya fedha kwa kujaza watu kupita kiasi.
Pia amewataka wazazi wawe makini na watoto wao na hasa disko toto, ili kuepuka ajali na matukio mengine yanayoweza kusababisha madhara.
Aliwatahadharisha wananchi kuwa makini na matapeli yanayotumia majina ya viongozi, watu maarufu na wafanyabiashara wakubwa kujipatia pesa na vitu mbalimbali.
Alisema matapeli hao wamekuwa wakitumia ujumbe mfupi wa simu za mkononi kupata taarifa za mtu binafsi hatimae mtu huyo kuibiwa.
Kuhusu agizo la Rais Kikwete la kuwataka wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kusalimisha silaha zao, Senso alisema baadhi ya watu hao tayari wameanza kusalimisha silaha hasa katika mikoa ya Kagera na Kigoma.
Kuhusu wajamiaji haramu, alisema tayari wameanza kurudi makwao na kusema hiyo ni hatua nzuri.
Alitoa wito kwa watu hao kuendelea kutekeleza agizo la serikali kabla ya operesheni kabambe kuanza itakayoendeshwa na polisi kwa kushirikiana na vyombo vyengine vya ulinzi na usalama.