Na Mwandishi wetu
IDARA ya Uhamiaji itabadilisha tena hati za kusafiria kutokana na kuwepo kwa matumizi mabaya yanayofanywa na baadhi ya wananchi.
Akizungumza kwenye banda la uhamiaji katika viwanja vya maonesho ya 38 ya kimataifa ya biashara ya sabasaba yanayofanyika Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa idara hiyo, Tatu Buruhani, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika wananchi wengi wanafanya udanganyifu.
Alisema, wananchi wengi wamekuwa wakiwatumia mawakala maarufu kama vishoka wa idara hiyo kwa nia ya kupatiwa huduma hiyo kwa haraka na hivyo kuwasababishia wengi wao kutapeliwa ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa vyeti vyao.
“Kinachotokea hapa ni kwamba, mwingine anachukua ile pasipoti anakwenda kuweka rehani, mwingine anauza, halafu anakuja kukwambia kwamba imeibiwa. Katika uchunguzi tuliofanya tumebaini kuwa haziibiwi bali wanazitumia vibaya pasipo kutambua umuhimu wake,” alisema.
Alisema utaratibu wa kubadilisha hati za kusafiria ulianza mwaka 1961 kutokana na changamoto kama na mabadiliko mengine yalifanywa mwaka 1992 na ya mwisho kufanywa ilikuwa mwaka 2005.