Na Kadama Malunde,Shinyanga
Kauli iliyotolewa na Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba,kwamba Tanzania inahitaji rais kijana mwenye fikra mpya katika uchaguzi mkuu ujao, imechafua hali ya hewa ndani ya Chama cha Mapinduzi.
Makamba alitoa kauli hiyo hivi karibuni nchini Uingereza.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mwenezi wa CCM wilaya ya Shinyanga mjini, Charles Shigino, alipinga vikali kauli ya Makamba na kusema anataka kuleta siasa za kibaguzi ndani ya chama hicho.
Alisema CCM inapiga vita ubaguzi wa aina yoyote na kuongeza kuwa kauli ya Makamba inaweza kuleta hatari kwa mustakabali wa chama na inaweza kuleta nyufa ya mshikamano uliopo.
Aidha alisema Makamba amelenga kuwabagua wazee na kwamba fikra zao hazifai na kuongeza kiwa ni matusi ya kiungwana wanayotukanwa wazee hao na alipaswa kuwaomba radhi.
“Namwomba Makamba atambue kuwa ujana sio kigezo cha kuiongoza jamii ya kitanzania na hasa katika nafasi nyeti ya urais , kisiasa kijana huyu bado ni mdogo ni bora akajifunza kutoka kwa wazee waliokwishawahi kuiongoza nchi ambao yeye amekuwa akiwadharau,” alisema.
Alimtaka kujipima kama ana uwezo wa kuongoza nchi kabla ya kutamani kuwaongoza Watanzania.
Alisema alisema CCM ni chama kikongwe chenye wanachama wa kila rika hivyo alipaswa kuwaheshimu badala ya kuwakejeli.