Na ShemsiaKhamis, Pemba
UJENZI wa mradi mkubwa wa kiwanda cha sukari katika kijiji cha Kiuyu Mbuyuni wilaya ya Micheweni kisiwani Pemba, utatumia shilingi bilioni 30.
Mkurugenzi wa kampuni ya Talon Sugar Group kutoka India, Dk. Hamza Hussein Sabri, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua eneo ambalo mradi huo utajengwa.
Alisema kiwanda hicho cha kisasa kitawanufaisha wananchi wote wa Pemba, ambapo kampuni itawapatia miche ya miwa na pembejeo zote kwa ajili ya kilimo hicho na baadae miwa yao wataiuza kwa kampuni hiyo.
Aidha alisema ujenzi wa mradi huo utaanza Oktoba na na utaanza uzalishaji wa sukari mwaka ujao.
Aidha alisema kiwanda kitatoa fursa za ajira kwa vijana wa Pemba na kusaidia kupunguza pengo la ajira linalowaandamana vijana.
“Kiwanda chetu hakitalima mua,kitakachofanya ni kuwapa wakulima fursa ya kulima miwa na baadae kiwanda kitanunua miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari,” alisema.
Kwaupande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho,Satish Purandare, alisema kiwanda hicho hakina uhusiano wowote na kiwanda cha sukari Mahonda kilichopo wilaya ya kaskazini B Unguja.
Nae, Ofisa kutoka Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA),Ali Shaaban Suleiman, alisema ujio wa wawekezaji hao wataleta faraja kwa wananchi wa Pemba .
Hicho kitakuwa kiwanda cha pili cha sukari Zanzibar kikitanguliwa na kile cha Mahonda na kitakapoanza uzalishaji kitaondoa uagizaji wa sukari kutoka nje.