Na Mwandishi wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amesema kamwe Tanzania haitatumia nguvu kumaliza mvutano kati yake na Malawi kuhusu mpaka kati ya nchi hizo.
Aidha, Rais Kikwete alisema Tanzania haioni matinki ama busara yoyote kuingia vitani na nchi yoyote jirani kwa sababu yoyote ile.
Alitoa uhakikisho huo wakati alipohutubia mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wananchi kwenye uwanja wa michezo wa mjini Mbamba Bay, mji mkuu wa wilaya mpya ya Nyasa.
Aliwambia wananchi hao: "Nataka kuwatoeni wasiwasi. Hakuna sababu ya vita. Laleni usingizi bila wasiwasi, kuleni samaki wenu kwa sababu Tanzania haioni busara ya vita."
"Tanzania haiwezi kutumia nguvu kupata suluhisho la mvutano wa mpaka.Tuna uwezo wa kupata jawabu la tatizo hilo bila kutumia njia ya vita.Tanzania haioni busara hiyo ya vita. Tuna uwezo wa kupata ufumbuzi kwa njia ya madiliano. Na wala msimamo huo siyo kwa mpaka wetu na Malawi pekee bali kwa mipaka yote ya Tanzania," alisema.
Rais Kikwete pia aliwaelezea wananchi juhudi ambazo zimekuwa zinafanywa na Tanzania kutatua tatizo la mpaka ikiwa ni pamoja na kuliomba jopo la Marais wastaafu kusaidia kutafuta jawabu la mpaka kati ya nchi hizo mbili.
Marais hao Joachim Chissano wa Msumbiji, Festus Mogae wa Botswana na Thabo Mbeki wa Afrika Kusini wanasaidiwa na jopo la kimataifa la mabingwa wa sheria katika kazi yao hiyo.
Rais pia aliwahakikishia wananchi wa wilaya ya Nyasa kuwa ahadi na mpango wa serikali kununua na kuweka meli mpya katika Ziwa Nyasa uko pale pale na kwamba mipango inafanywa ya kuhamisha chelezo cha kujengea meli kutoka Mwanza kwenye Ziwa Victoria kuipeleka Itungi, Kyela, Mbeya ili kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Katika kampeni ya uchaguzi mkuu mwaka 2010 aliahidi ununuzi wa meli tatu za kutoa huduma katika maziwa makuu ya Tanzania ya Victoria, Tanganyika na Nyasa.
Alisema kiasi cha shilingi bilioni 23 zimetengwa tayari kwa ajili ya kuanza ujenzi wa meli hiyo.
Alisema michoro ya meli ya Ziwa Nyasa imelazimishwa kubadilishwa kidogo kwa sababu ya ukweli kuwa Ziwa hilo lina mawimbi makali na huchafuka mara kwa mara tofauti na Maziwa Victoria na Tanganyika.
Aliwaambia wananchi kuwa serikali inaendelea na mipango ya kujenga reli kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay ili kuzidi kufungua ukanda wa Mtwara na kuweza kubeba chuma na makaa ya mawe kutoka Liganga na Mchuchuma.
Kabla ya kuhutubia mkutano wa hadhara, Rais Kikwete ambaye alikuwa katika siku ya pili ya ziara yake ya siku sita katika mkoa wa Ruvuma, alikuwa na shughuli nyingi katika wilaya ya Nyasa ambako alizindua daraja la Ruhekei lililoko kijiji cha Mkalole, kilomita nane kutoka mjini Mbamba Bay.
Alisema ujenzi wa daraja hilo ambalo lina sehemu tatu limejengwa kisasa kabisa ikiwa ni maandalizi ya ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga, wilaya ya Mbinga kwenda Mbamba Bay,wilaya ya Nyasa.
"Ni kweli mwaka 2005 wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu nilishindwa kuvuka hapa kwa sababu daraja lilivunjika lakini ujenzi huu wa kisasa ni kwa sababu tunajiandaa kujenga barabara ya lami kuunganisha Mbinga na Mbamba Bay," alisema.
Wakati huo huo serikali imekiomba Chama cha Mapinduzi (CCM) kuipangia upya malengo ya kusambaza umeme kwa wananchi kwa sababu malengo yaliyopangwa katika ilani ya uchaguzi mkuu wa 2010 yamefikiwa na kupitwa hata kabla ya kumalizika kipindi cha miaka mitano.
Aidha, imesema upo uwezekano mkubwa kwamba usambazaji wa umeme unaweza kufikia asilimia 50 ya wananchi wote wa Tanzania ifikapo mwakani kwa sababu umeme sasa unasambazwa kwa kasi kubwa.
Ombi hilo limetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospter Muhongo, wakati alipozungumza katika mkutano wa hadhara ambao ulihutubiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, mjini Mbamba Bay, Wilaya ya Nyasa.